Ni vitamini inayoweza kuunganika na mafuta. Hufahamika pia kwa jina lingine la calciferol.
Kwa mujibu wa taasisi ya National Institutes of Health, uhitaji wa kila siku wa mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 13 hadi 70 ni 15 mcg.
Watu wenye zaidi ya miaka 70 huhitaji kiasi cha 20 mcg kila siku.
Ni vyakula vichache sana vya asili ndivyo hubeba vitamini D. Baadhi ya vyakula hivyo ni samaki, maini, kiini cha mayai na cheese.
Mwanga wa jua umekuwa unazalisha pia vitamini D ya asili kwa zaidi ya miaka 5000 iliyopita.
Zifuatazo ni faida za vitamini D kwa afya ya binadamu:
1. Mifupa
Vitamini D huusaidia mwili kuongeza ufyonzaji na matumizi ya madini ya calcium ambayo kwa hutumika kutengeneza mifupa na meno kwa asilimia 99.
Ni muhimu katika kuongeza ubora wa mifupa, kuongeza ujazo wake pamoja na kuifanya isipinde na kuvunjika kirahisi. (1,2,3)
Pasipo uwepo wa vitamini hii, madini ya calcium na phosphate huwa hayawezi kuboresha afya ya mifupa.
2. Sonona
Kwa mujibu wa WHO, sonona ndiyo ugonjwa wa akili unaoongoza kwa kuathiri watu wengi zaidi duniani, kiasi cha milioni 280.
Ni ugonjwa mbaya unaosababisha hali ya kukata tamaa, kutokujikubali, kujiona mkosefu pamoja na kupoteza matumaini ya kuishi kiasi cha kutamani kujiua.
Tafiti zinabainisha kuwa matumizi ya vitamini D husaidia kutibu tatizo hili. (4,5,6)
Zaidi ya watu 700,000 duniani hujiua kila mwaka kutokana na changamoto hii hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari.
3. Kinga Mwili
Husaidia kuongeza kinga za mwili kwa kupambana na magonjwa sugu kama kisukari, saratani, magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu. (6,7,8)
Magonjwa haya huchangia zaidi ya nusu ya vifo vyote duniani kila siku.
Tafiti za siku za hivi karibuni zinathibitisha kuwa upungufu wa vitamini D husababisha maambukizi makubwa ya mafua ya kawaida pamoja vifo vitokanavyo na ugonjwa wa UVIKO-19. (9,10)
Upungufu
Changamoto kubwa ya upungufu wa vitamini D ni kusababisha matege kwa watoto.
Tatizo hili husababisha kudhoofika na kupinda kwa mifupa ya miguu kama upinde wa mshale.
Aidha, huwaongezea watoto nafasi ya kupatwa na aina mbalimbali za mizio pamoja na kuugua shinikizo la juu la damu.
Kwa wanawake wajawazito, huongeza uwezekano wa kujifungua kabla ya wakati pamoja kupatwa na kifafa cha mimba.
Aidha, huongeza nafasi ya kuugua kisukari cha ujauzito pamoja na maambukizi ya fangasi wa uke. (11,12,13)
Muhtasari
Matumizi makubwa sana ya vitamini D yanaweza kutengeneza sumu mwilini.
Hufanya madini ya calcium yawe mengi sana mwilini, kitendo ambacho huharibu mifupa, mishipa ya damu, figo, mapafu na misuli ya moyo.
Tatizo hili ni hatari, linapaswa kushughulikiwa kwa uzito mkubwa.
Dalili za kawaida za uwepo wa vitamini D iliyozidi ni kupoteza hamu ya kula, kutapika, kukauka kwa midomo pamoja na choo kigumu.
Aidha, watu weusi sana, wajawazito, wazee, wenye uzito mkubwa pamoja na wale wasiopata mwanga wa jua wa kutosha wanaweza kupata upungufu wa vitamini hii.
Ni muhimu kama watatumia virutubusho vya ziada.