Ugonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell Disease)

6 Min Read

Seli mundu kwa lugha ya kiingereza huitwa Sickle Cell Disease.

Ni kundi kubwa la magonjwa ya kurithi yanayoathiri chembechembe nyekundu za damu.

Wastani wa watu milioni 20 duniani wanakabiliwa na tatizo hili.

Kwa Tanzania, wastani wa watoto 11000 kila mwaka huzaliwa wakiwa na ugonjwa huu.

Kupata Ugonjwa

Huu ni ugonjwa wa kurithi, hutokea kwa mtoto baada ya kupokea taarifa za ugonjwa kutoka kwa wazazi wakati wa kutungwa kwa ujauzito.

Ili ugonjwa huu uweze kuonekana kwa mtu, ni lazima wazazi wake wote wachangie nusu ya taarifa zake.

Mfano, wewe unayesoma makala hii unaweza kuonekana kuwa mgonjwa wa seli mundu ikiwa baba yako atachangia asilimia 50 ya taarifa za ugonjwa na mama atachangia asilimia 50 pia.

Watu wanaopokea taarifa nusu za ugonjwa huu kutoka kwa mzazi mmoja pekee huwa hawawezi kuonesha uwepo wake kwa nje, japo kwa ndani huwa na chembechembe za uwepo wake.

Watu hawa wanaweza kuzaa mtoto mwenye ugonjwa baada ya kukutana na wenza walio pia na taarifa nusu.

Ugonjwa Upoje?

Kwa muundo wake, chembechembe nyekundu za damu huundwa na aina moja ya protini inayoitwa hemoglobin.

Protini hii ndiyo hubeba hewa na kuisafirisha kwenda sehemu mbalimbali za mwili.

Kwa watu wenye afya nzuri, hemoglobin huwa ni laini, ina umbo la duara na huwa inaweza kubadilika umbo lake kirahisi.

Tabia hizi ndiyo huruhusu iweze kupenya kirahisi na kusafiri kila sehemu ya mwili pasipo uwepo wa pingamizi lolote.

Kwa watu wenye ugonjwa huu hali haipo hivyo. Hemoglobin huwa ngumu, ina umbo la mwezi mchanga au herufi C na huwa haibadiliki kirahisi.

Dalili

Watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu mara nyingi huanza kuonesha dalili zake baada ya kufikia umri wa miezi 5 na kuendelea.

Baadhi ya dalili za ugonjwa huu ni hizi:

1. Udumavu

Watoto wenye ugonjwa wa seli mundu huwa na ukuaji hafifu kuliko wale wasio na ugonjwa huu.

Muda wa kukaa, kuongea, kutembea pamoja na hatua zingine za ukuaji zinaweza kwenda kwa hatua ndogo kuliko kawaida.

2. Upungufu wa Damu

Chembechembe nyekundu za damu huwa na wastani wa kuishi kwa siku 120.

Kwa wagonjwa wa seli mundu, chembechembe hizi hufa baada ya siku 10-20 pekee hivyo kusababisha upungufu mkubwa damu kwa wagonjwa.

Hali hii pia huambatana na uchovu mkubwa.

3. Umanjano

Watoto na watu wazima huwa huonesha hali ya uwepo wa umanjano.

Sababu kubwa ni kuwa chembechembe nyekundu za damu huharibika mapema kwa kiasi kikubwa sana kuliko kile ambacho mwili unaweza kuzitoa nje.

4. Maumivu

Muundo wa seli za damu kwa wagonjwa huwa upo tofauti hivyo husababisha kuziba kwa mishipa midogo ya damu.

Madhara ya jambo hili ni kutokea kwa maumivu ya kifua, sehemu ya chini ya tumbo, maungio pamoja na mifupa.

Kwa wanaume huenda mbali zaidi kwa kusababisha maumivu ya uume hasa unapokuwa umesimama.

5. Uvimbe

Kuziba kwa mishipa ya damu huzuia kusafiri vizuri kwa damu kuelekea kwenye miguu na mikono.

Ni chanzo kikubwa ch kuvimba kwa sehemu hizi.

6. Maambukizi

Watu wenye ugonjwa huu hupatwa na maambukizi ya mara kwa mara hasa yale yanayohusisha bakteria.

Hutokana na kuharibika kwa wengu ambalo huhusika katika kuhifadhi na kutoa kinga mwili zinazopambana na magonjwa.

7. Macho

Wengi huanza kupungukiwa na uoni wa macho.

Inasababishwa na kuziba kwa mishipa midogo ya damu inayo safiri kuelekea kwenye macho.

Ugunduzi

Uwepo wa tatizo hili hugunduliwa kwa kuchukua historia ya mgonjwa, muonekano wake pamoja na kuchunguza damu ya mhusika ili kuthibitisha maumbo ya seli za damu.

Kipimo cha Hemoglobin electrophoresis kinaweza kutumika ili kuchunguza kama mtu amebeba chembechembe za urithi za ugonjwa huu.

Tiba

Hutegemea umri pamoja na dalili husika zinazoonekana kwa wakati huo. 

Matumizi ya dawa za foliki asidi ili kuongeza damu, antibayotiki na chanjo mbalimbali ili kuzuia maambukizi, dawa za maumivu ili kupunguza maumivu pamoja na vidonge vya hydroxyurea hufaa sana kwa wagonjwa hawa.

Aidha, wagonjwa hushauriwa wanywe maji mengi kila siku ili kuongeza wingi wa vimiminika mwilini.

Kuongezewa damu nyingine hufaa ikiwa mhusika atakuwa na upungufu wa damu, pia upandikizaji wa uboho mpya hushauriwa kwa baadhi ya watu.

Muhtasari

Ugonjwa huu huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa kiharusi, upungufu wa nguvu za kiume, maambukizi ya mara kwa mara, kuharibika kwa figo pamoja na upofu.

Ni muhimu sana kwa wagonjwa kupata tiba sahihi pale wanapogundulika kuwa na tatizo hili.

Hata hivyo, upimaji wa chembechembe za urithi wa ugonjwa kwa wachumba kabla ya ndoa kunaweza kusaidia kutoa mwelekeo wa baadae wa afya za watoto watakaozaliwa.

Seli mundu ni ugonjwa wa kudumu, hausababishwi na kurogwa.

Share This Article