Inaaminika kuwa asili ya machungwa ni nchi ya China ambako matunda haya yalianza kulimwa miaka mingi sana iliyopita.
Kwa mujibu wa Idara ya Chakula ya marekani (USDA), katika kila gramu 100 za chungwa, gramu 86.7 kati yake huwa ni maji.
Huwa pia na nishati, protini, wanga, nyuzilishe, madini ya calcium, magnesium, phosphorus, potassium, sodium, zinc, copper, selenium na kiasi kidogo cha sukari.
Aidha, huwa na vitamini C, citric acid, vitamini B12, vitamini A, folate pamoja na viondoa sumu vya carotene, vitamini E, Hesperidin na Naringenin.
Mjumuiko wa virutubisho hivi huleta faida zifuatazo kwa afya;
1. Huongeza Damu
Madini ya chuma huhitajika kwenye kutengeneza damu mwilini.
Unaweza kuyapata kupitia mlo au kwa kutumia virutubisho na dawa zenye madini haya.
Ili mwili uweze kufyonza vizuri madini ya chuma kutoka kwenye vyakula, vitamini C na citric acid huhitajika ili kurahisisha zoezi hilo. (1,2,3)
Tunda hili huusaidia mwili kutengeneza damu.
2. Saratani
Kampaundi za Naringenin zinazopatikana kwenye chungwa huhusisishwa na kuzuia pamoja na kupambana na aina mbalimbali za saratani mwilini. (4,5)
Hufanya hivyo kwa kuingilia ukuaji wa seli za saratani, kudhibiti ukuaji wake pamoja na kuingiza taarifa kinzani ambazo huzifanya seli husika zijiue zenyewe.
3. Kinga
Mwili huwa na askari wake wanaosaidia kwenye kuulinda kila siku, mchana na usiku.
Askari hawa hupaswa kuwa tayari muda wote kukabiliana na mashambulizi ya vimelea vya magonjwa.
Kwa kuwa hufanya kazi hii pasipo kupumzika, ni lazima nguvu ya ziada itumike kwenye kuwapatia msaada wa nguvu za ziada.
Chungwa ni tunda lenye zinc na vitamini C nyingi ambayo hutumiwa na mifumo ya mwili katika kuimarisha kinga yake kwenye kupambana na magonjwa. (6,7)
Ongeza kinga ya mwili wako kwa kutumia tunda hili.
4. Kiharusi
Vyakula vyenye kiasi kikubwa cha flavonoids huwa na sifa kubwa ya kuukinga mwili dhidi ya shambulio la kiharusi.
Ugonjwa huu unaosababishwa na kuganda kwa damu, au kupasuka kwa mishipa ya damu husababisha kupooza kwa mwili.
Hufanya hivyo kwa kuzuia shinikizo la juu la damu, kuimarisha mishipa ya damu pamoja na kuzuia kuganda kwa damu kwenye mishipa yake. (8)
Husaidia pia kwenye kupambana na magonjwa ya mfumo wa damu na moyo.
5. Presha
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), walau watu bilioni 1.28 wanakabiliwa na tatizo la shinikizo la juu la damu.
Watu hawa wana wastani wa umri kati ya miaka 30-79.
Baadhi ya tafiti zinaelezea uwezo wa chungwa kwenye kuzuia ongezeko la shinikizo la damu mwilini. (9)
Hata hivyo, tafiti nyingi zaidi zinahitajika kuthibitisha madai haya.
6. Uzito
Kuna nadharia nyingi mtaani zinazoelezea uwezo wa chungwa kwenye kupunguza uzito wa mwili.
Hata hivyo, ni ukweli kuwa hakuna tafiti pamoja na majaribio mengi yaliyofanyika kwa binadamu kuthibitisha madai haya. (10,11)
Ili madai haya yaweze kupata mashiko kisayansi ni lazima tafiti za ziada zifanyike ili kuweka sawa taarifa hizi.
7. Ini
Ini la binadamu hufanya kazi zaidi ya 500 mwilini.
Aina mbalimbali za vimelea vya magonjwa hasa virusi pamoja na baadhi ya vinywaji hasa pombe husababisha kuharibika kwa kiungo hili muhimu kwa afya ya binadamu.
Utafiti uliofanyika unaonesha kuwa juisi ya chungwa inaweza kutibu athari za ini lililoharibiwa kwa pombe. (12)
8. Figo
Figo ni mashine za mwili zinazochuja damu na kutengeneza mkojo.
Zikiharibika hufanya mhusika augue ugonjwa wa figo ambao usipopata tiba sahihi kwa haraka, huwa sugu na kufanya mhusika aishi kwa kutegemea mashine ya nje ya kufanya kazi za figo.
Hatua hii ni mbaya, hatari na huongeza uwezekano wa kupoteza maisha ya mgonjwa.
Changamoto nyingine ya viungo hivi ni kutengenezwa kwa mawe ndani yake ambayo huathiri ufanisi wa kazi zake, na kuongeza uwezekano wa kuugua ugonjwa wa figo.
Kemikali za citric acid na naringenin zimebainishwa na tafiti kuwa na uwezo wa kuongeza ubora wa afya ya figo, kupunguza athari za magonjwa ya kisukari na presha kwenye kiungo hiki pamoja na kuzuia utengenezwaji wa mawe kwenye figo. (13,14)
Linda figo zako kwa kula chungwa, au pia kunywa juisi yake.
9. Kisukari
Aina kuu ya nyuzilishe zinazopatikana kwenye chungwa huitwa pectin.
Miongoni wa faida za pectin ni kuboresha mfumo wa chakula na kupunguza matumizi ya sukari na wanga mwilini.
Ni tunda zuri sana kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari. (15,16,17)
Hata hivyo, ili uipate pectin hii inafaa ule sehemu nyeupe ya tunda hili inayofuata baada ya magada yake ya nje.
10. Urembo
Pengine umewahi kuona aina nyingi za lotion, mafuta au sabuni zilizo na kipeperushi kinachoonesha kuwa zimetengenezwa kwa kutumia vitamini C.
Hawakuwa wanakudangaya.
Hutumika kuboresha afya ya ngozi kwa kuongeza mng’ao wake, kuponya majeraha na makovu pamoja na kuondoa chunusi. (18,19,20)
Vitamini hii ipo kwa wingi kwenye chungwa.
Muhtasari
Chungwa ni tunda lenye faida nyingi sana kwa afya, halina gharama kubwa pia hupatikana karibia kila sehemu.
Jitahidi utumie tunda hili mara kwa mara, kitakufaa sana.