Ukuaji pamoja na tabia mbalimbali za watoto hutofautiana sana.
Mfano, mtoto mmoja anaweza kuwahi kukaa, kutembea au pia kuongea kuliko mtoto mwingine mwenye umri sawa na yeye.
Hali hii ni sawa, haimaanishi kuwa lazima watoto wote wafuate mfumo mmoja wa hatua za makuzi na tabia zao.
Linapokuja swala la kunyonyesha, kuna miongozo mingi inayotoa ushauri wa namna gani mama afanye ili kuhakikisha kuwa mtoto anapata virutubisho vya kutosha.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na UNICEF, mtoto anapaswa kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwenye kipindi cha miezi 6 ya mwanzo pasipo kupewa maji au vyakula vingine mbadala.
Nyongeza ya mlo hufaa kutolewa baada ya kufikisha miezi 6, na anapaswa kuendelea kunyonya hadi afikie umri wa miezi 24.
Anyonye Mara Ngapi?
Hili ni swali muhimu sana.
Kwa mujibu wa CDC, utaratibu huu unaweza kutumika kama mwongozo wa unyonyeshaji.
Siku za Mwanzo
Tumbo la mtoto bado ni dogo sana, hahitaji kiasi kikubwa sana cha maziwa pamoja na kujaza tumbo lake kila mara.
Anaweza kunyonyeshwa kila baada ya masaa 1-3 ili kumsaidia mama azalishe kiasi kikubwa cha maziwa pamoja na kumpa ujuzi mtoto kwenye kunyonya na kumeza
Kama anayo tabia ya kulala kwa muda mrefu, ni vizuri akiamshwa baada ya muda huo ili apate haki yake ya kunyonya.
Mwezi 1-6
Ni muda ambao mtoto huanza kukua kwa kasi.
Hii inatoa maana kuwa tumbo lake pia huanza kupanuka, hivyo huhitaji maziwa mengi zaidi.
Anaweza kunyonya kila baada ya masaa 2-4.
Ndani ya saa 24 za kila siku, mtoto anapaswa kunyonyeshwa walau mara 8-12.
Miezi 6-12
Unyonyaji huanza kupungua kwa kuwa usaidizi wa chakula mbadala huanza kutolewa.
Mama anapaswa kufuatilia kwa ukaribu uhitaji wa kunyonya wa mtoto.
Ikiwa ataanza kuonesha tabia ya kuchukia maziwa ya mama baada ya kuanza kupewa vyakula mbadala, inashauriwa anyonyeshwe kwanza kabla ya kumpa kitu kingine chochote.
Kumbuka, maziwa ya mama huwa na virutubisho muhimu zaidi kwa ajili ya ukuaji wa mtoto kuliko hivyo vyakula vingine.
Miezi 12-24
Baadhi ya watoto huanza kukataa kabisa kunyonya, na wengine hunyonya mara chache sana kwa siku.
Kwa mfano, watoto wengi hupenda kunyonya asubuhi baada ya kuamka, na usiku kabla ya kulala.
Mfuatilie kwa ukaribu na hakikisha ananyonya kila inapobidi.
Faida za Kunyonyesha
Maziwa ya mama huwa na faida kubwa kwa afya ya mtoto.
Humfanya mtoto asiungue magonjwa ya kuhara, uti wa mgongo, maambukizi ya sikio la kati, kisukari, pumu na vifo vya ghafla.
Kwa mama mwenyewe, unyonyeshaji humsaidia kupunguza nafasi ya kuugua magonjwa ya moyo, kisukari, presha pamoja na saratani ya matiti na vifuko vya mayai.
Muhtasari
Unyonyeshaji hauwezi kuharibu urembo wa mama.
Watoto wanapaswa kunyonyeshwa vizuri ili wakue wakiwa na afya bora ya mwili na akili.