Ugonjwa wa Umanjano kwa Watu Wazima (Jaundice)

3 Min Read

Ni ugonjwa unaofanya rangi ya ngozi na macho iwe ya njano.

Kama ambavyo watoto hupata ugonjwa huu, watu wazima pia wanaweza kuupata. 

Katika hali ya kawaida, kila baada ya siku 120 chembechembe nyekundu za damu huharibiwa, na hupaswa kutolewa mwilini kupitia ini ambalo huingiza mabaki haya kwenye choo.

Mabaki haya ya damu kwa kiingereza huitwa bilirubin, huwa na rangi ya njano.

Hivyo, ugonjwa wa umanjano hutokea baada ya kujikusanya mwilini kwa kiasi kikubwa cha mabaki ya chembechembe nyekundu za damu (bilirubin) kuliko kiasi cha kawaida ambacho ini linaweza kukitoa nje kwa wakati huo.

Ugonjwa huu huwa hautokei sana kwa watu wazima, lakini kuna baadhi ya mambo yanayoweza kuchangia utokee kama vile uwepo wa homa ya ini unaosababishwa na maambukizi ya virusi, kuharibika kwa ini kunakosababishwa na unywaji wa pombe nyingi pamoja na kujiziba kwa mrija unaotoa nyongo ambako mara nyingi husababishwa na saratani, mawe kwenye figo au changamoto mbalimbali kwenye ini.

Aidha, saratani ya kongosho, matumizi makubwa ya baaadhi ya dawa mfano paracetamol, maambukizi makali ya baadhi ya magonjwa hasa malaria, seli mundu na uwepo wa changamoto kwenye utengenezwaji wa damu mwilini vinaweza kusababisha kutokea kwa hali hii.

    Dalili

    Dalili ya kwanza kabisa ni kuwa na umanjano wa rangi ya ngozi na macho.

    Huanzia usoni, kisha kifua, tumbo na miguu.

    Hufuatiwa na maumivu makali sehemu ya chini ya tumbo, homa, kupungua uzito wa mwili, kujisaidia choo na mkojo mweusi pamoja na kukosa hamu ya kula.

    Ugunduzi

    Njia nyepesi ni kutazama rangi ya ngozi na macho.

    Inaweza pia kugunduliwa kwa kuchunguza damu, au kupitia vipimo vingine vya kemikali za ini.

    Tiba

    Kwa watu wazima, ugonjwa wa umanjano huwa hautibiwi, bali chanzo kinachofanya hali hii itokee ndiyo hutibiwa.

    Daktari anaweza kushauri mgonjwa atulie na kuondoa wasiwasi ikiwa atagundua changamoto hii itapona nyenyewe.

    Baadhi ya dawa za kutibu virusi zinaweza kutolewa ikiwa chanzo ni uwepo wa homa ya ini, na upasuaji unaweza kufanywa ikiwa ugonjwa wa umanjano unasababishwa na kuziba kwa baadhi ya mishipa ya mfuko wa nyongo.

    Ubadilishaji wa damu unaweza kufanyika kwa watu ambao changamoto hii hutokea kutokana na uwepo wa mapungufu kwenye utengenezwaji wa damu mwilini.

    Muhtasari

    Baadhi ya watu hupatwa na changamoto hii baada ya kuugua malaria kali.

    Mgonjwa atatibiwa kwa kufuata utaratibu sahihi kwa watu wa aina hii.

    Aidha, matumizi ya pombe, sigara na baadhi ya madawa hukatazwa kwa watu ambao pengine tatizo lao limesababishwa na uwepo wa tabia hizi.

    Share This Article