Watoto wenye ugonjwa wa umanjano huwa na macho na ngozi yenye rangi ya njano.
Katika hali ya kawaida, kila baada ya siku 120 chembechembe nyekundu za damu huharibiwa, na hupaswa kutolewa mwilini kupitia ini ambalo huingiza mabaki haya kwenye choo.
Mabaki haya ya damu kwa kiingereza huitwa bilirubin, huwa na rangi ya njano.
Ini la watoto huwa bado halijakomaa vizuri kuondoa mabaki haya na kuyaingiza kwenye mfumo wa chakula kama ilivyo ini la watu wazima.
Hivyo, ugonjwa wa umanjano hutokea baada ya kujikusanya mwilini kwa kiasi kikubwa cha mabaki ya chembechembe nyekundu za damu (bilirubin) kuliko kiasi cha kawaida ambacho ini linaweza kukitoa nje kwa wakati huo.
Dalili
Dalili ya kwanza kabisa ni mtoto kuwa na umanjano wa rangi ya ngozi na macho.
Huanzia usoni, kisha kifua, tumbo na miguu.
Dalili zingine za uwepo wa tatizo hili ni mtoto kusinzia sana kila wakati, kuwa na hasira pamoja na kupata changamoto kwenye kunyonya.
Kwa watoto wenye rangi nyeusi inaweza kuwa changamoto kidogo kutambua uwepo wake, lakini unaweza kugundua kwa kubonyeza ngozi ya pua au paji la uso.
Kama ana manjano, ngozi ya eneo hilo itabadilika rangi kuwa ya manjano baada ya kuondoa vidole vyako.
Kuonekana Kwa Tatizo
Baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na hali hii.
Kwa kuwa masalia ya chembechembe nyekundu za damu huongezeka sana mwilini baada ya siku 2-7, namba kubwa ya watoto huanza kuonesha uwepo wa tatizo hili muda huo.
Vihatarishi
Tumeona kuwa chanzo kikubwa kinachofanya changamoto hii itokee ni kujikusanya kwa kiasi kikubwa cha mabaki ya chembechembe nyekundu za damu mwilini.
Lakini, mambo gani hasa huongeza hatari ya kutokea kwa hali hii?
1. Watoto Njiti
Watoto waliozaliwa kabla ya muda sahihi huwa na nafasi kubwa ya kupatwa na changamoto hii kwa kuwa ini lao huwa bado changa sana, halina uwezo wa kuondoa masalia yote ya chembechembe nyekundu za damu. (1,2,3)
2. Mtoto Asiyenyonya Vizuri
Hii hutokea wiki ya kwanza ya kuzaliwa kwa mtoto.
Inaweza kuchangiwa na uchache wa maziwa ya mama, au uwepo wa changamoto fulani zinazofanya mtoto asinyonye vizuri. (4,5)
3. Makundi ya Damu
Kama mama na mtoto wana makundi tofauti ya damu, hasa ikiwa mama ana kundi O huku mtoto ana kundi A au B. (6,7)
Inaweza kutokea pia ikiwa mama ana kundi lolote hasi la damu huku mtoto ana kundi chanya la damu. (8)
Mambo haya husababisha mama azalishe kinga mwili ambazo hushambulia chembechembe nyekundu za damu ya mtoto hivyo kufanya masalia yake yawe mengi kuliko kiasi cha kawaida ambacho mwili wake unaweza kutoa.
4. Jenetiki
Baadhi ya watoto huzaliwa na matatizo ya kijenetiki ambayo hufanya chembechembe nyekundu za damu ziwe na tabia ya kupasuka kirahisi kuliko kawaida.
Changamoto hii isiyo onekana sana kitaalamu huitwa G6DP deficiency. (9)
5. Damu Nyingi
Ikiwa mtoto atazaliwa na tatizo linalofanya azalishe kiasi kikubwa sana cha damu, anaweza kuwa kwenye hatari ya kupatwa na changamoto hii. (10)
Ugunduzi
Njia nyepesi ni kutazama rangi ya ngozi na macho.
Inaweza pia kugunduliwa kwa kuchunguza damu, au kupitia mashine maalumu ya mionzi.
Tiba
Hutegemea umri wa mtoto, ukubwa wa tatizo pamoja na sababu iliyofanya tatizo litokee.
Ugonjwa wa umanjano wa kawaida hupona wenyewe tu baada ya wiki 1-2 na huwa hauna madhara kwa afya.
Kwa watoto ambao husababishwa na upungufu wa maziwa, daktari anaweza kushauri mama aongeze unyonyeshaji zaidi, na ikiwa haitasaidia maziwa mbadala yanaweza kuongezwa kama sehemu ya tiba.
Ikiwa ugonjwa wa umanjano unasababishwa na mambo mengine, tiba zifuatazo hufanywa;
- Kuongeza vimimika kwa mtoto
- Mionzi
- Kubadilisha damu yake
- Kuwekewa immunoglobulin (kinga mwili) ambazo hulinda chembechembe za damu ili zisiharibiwe kirahisi, hasa ikiwa chanzo chake ni utofauti wa makundi ya damu kati yake na mama.
Muhtasari
Katika mazingira machache sana, ugonjwa wa umanjano unaweza kusababishwa na kuvuja kwa damu ndani ya mwili, ugonjwa wa ini pamoja na uwepo wa maambukizi makali mwilini.
Mtoto anapaswa kuchunguzwa vizuri na kupata tiba sahihi.
Katika hali ya kawaida, umanjano huisha wenyewe tu baada ya wiki 1-2.
Njia nyingine mbadala ya kutibu tatizo hili ni kutumia mwanga wa jua la asili linalochomoza. (11,12)
Mzazi anapaswa kuwa makini ili asimuunguze mtoto pamoja na kuleta athari nyingine kubwa kwa afya.
Aidha, watumishi wa afya wawakague watoto kama wanao ugonjwa huu kabla hawajaruhusiwa kutoka hospitalini.