Ni kitendo cha meno kuanza kuchomoza kwenye fizi.
Umri wa kuota meno kwa watoto hutofautiana sana. Kwa kiasi kikubwa, watoto wengi huanza kuota meno wakiwa kwenye umri wa kati ya miezi 4-7.
Kwa kuwa ukuaji wa watoto huwa haufanani, mwanao anaweza kuwahi au kuchelewa zaidi ya muda huu, hivyo usiwe na wasiwasi.
Dalili
Watu wengi huamini kuwa dalili ya kwanza ya mtoto kuanza kuota meno ni homa kali na kuhara. Hii siyo sawa.
Kuota kwa meno kwa mtoto hakuna uhusiano wowote na kuhara.
Kuhara na homa kali ni matokeo ya uwepo wa ugonjwa mwingine au uwepo wa mazingira yasiyo salama kwa mtoto.
Ifahamike kuwa wakati huu watoto huwa na hamu ya kula kila kitu, pamoja na kusugua fizi zao maana huwasha.
Wakati huu wanaweza kula uchafu wa aina mbalimbali ambao kwa mantiki nyepesi ndiyo huwafanya waanze kuhara.
Baadhi ya dalili za mtoto kuota meno ni kuvimba na kulainika kwa fizi, hasira na kulia, kuongezeka kidogo kwa joto la mwili, kulazimisha kula kila kitu, kikohozi, kusugua fizi pamoja na kuweweseka.
Aidha, kukataa kula, kuvuta masikio, kukosa usingizi na kung’ata na kuvuta chuchu wakati wa kunyonya ni dalili zingine za mtoto kuota meno.
Kuota kwa meno kunaweza kusababisha maumivu makali kwa mtoto, lakini hakupaswi kuwa chanzo cha kuhara au kupata homa kali.
Hizi siyo dalili za kawaida. Apelekwe hospitalini haraka.
Meno na Umri
Meno mawili ya chini ndio huanzia kuota yakifuatiwa na meno manne ya juu.
Baada ya hapo huanza kuota kwa namna tofauti.
Katika ukuaji wake, tunategemea kuona mfuatano huu wa uotaji wa meno.
- Meno 4 baada ya miezi 11
- Meno 8 baada ya miezi 15
- Meno 12 baada ya miezi 19
- Meno 16 baada ya miezi 23
Ikitokea kuwa utaratibu huu haufuatwi usipate wasiwasi.
Tunaendelea kusisitiza kuwa ukuaji wa watoto hutofautiana, sio lazima wote wafuate mfumo mmoja.
Muhtasari
Unaweza usiamini, lakini baadhi ya watoto huzaliwa wakiwa na meno. Mtoto huyu anapaswa kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi wa kina.
Ikiwa daktari atajiridhisha kuwa meno hayo yapo imara na mizizi yake haichezi, yataachwa.
Lakini ikiwa yatakuwa hayapo imara au yanaleta changamoto zozote kwenye ulaji, upumuaji au ukuaji wa mtoto, daktari anaweza kushauri yatolewe kwa upasuaji.