Ujauzito unaweza kuharibika wakati wowote ule.
Tafiti za afya zinathibitisha kuwa kadri ujauzito unavyozidi kuwa mkubwa ndivyo uwezekano wa kuharibika kwake unavyozidi kupungua.
Kwa ujumla wake, asilimia 80 ya mimba zote zinazoharibika hutokea kabla hazijafikia umri wa wiki 13. (1)
Takwimu
Kitendo cha kujishikiza kwa yai lililo rutubishwa kwenye mji wa uzazi ili mimba ianze kulelewa hutokea kati ya siku ya 8-10 baada ya kutokea kwa ovulation. (2)
Muda huu ni wastani wa wiki 3 baada ya siku ya kwanza ya hedhi ya mwisho. Uwezekano wa kuharibika kwa ujauzito kwenye wiki ya 3-4 ni asilimia 50-75. (3)
Hii inamaanisha kuwa wanawake wengi hupoteza ujauzito pasipo kufahamu, kabla hata hawajaanza kuonesha dalili zake.
Wiki ya 5 huwa ni asilimia 21, wiki ya 6-7 asilimia 5, wiki ya 8-13 asilimia 2-4 huku wiki ya 14-20 ikiwa ni chini ya asilimia 1. (4)
Kuna sababu nyingi zinazofanya ujauzito uharibike. Baadhi yake ni hizi;
1. Sababu za Urithi
Chembeuzi au kromosomu ni vipande vidogo vyenye umbo la njiti za viberiti, au nyuzi ambavyo hupatikana kwenye seli za binadamu.
Ndicho kiini cha seli ambacho hubeba taarifa za urithi za kiumbe husika. (5)
Binadamu hubeba chembeuzi 46 ambazo kila mzazi huchangia kiasi cha chembeuzi 23 wakati wa kutungwa kwa ujauzito.
Ikiwa yai au shahawa zitabeba chembeuzi zaidi ya 23 wakati wa urutubishaji, au ikiwa chembeuzi hizi zitakuwa na mapungufu yoyote, uwezekano wa kuharibika kwa ujauzito ni mkubwa sana.
Asilimia 50-60 ya mimba zote zinazoharibika husababishwa na mapungufu kwenye chembeuzi. (6)
Ifahamike kuwa tabia zote za binadamu, jinsia, rangi ya ngozi na kundi la damu vyote huamuliwa na chembeuzi.
2. Maambukizi
Maambukizi makali ya vimelea vya magonjwa hasa bakteria na virusi yanaweza kuharibu ujauzito.
Maambikizi ya vimelea vya magonjwa huchangia asilimia 15 ya kuharibika kwa ujauzito wenye umri chini ya wiki 12 na asilimia 66 ya ujauzito wenye umri zaidi ya wiki 12. (6)
Ikiwa maambukizi haya hayatatibiwa vizuri, uwezekano wa kuendelea kuharibika kwa ujauzito ujao ni asilimia 4. (7)
3. Mfumo wa Vichocheo
Mvurugiko wa homoni ni kitendo cha vichocheo vya mwili kuwa vichache au vingi kuliko kiwango cha kawaida kinachotakiwa.
Vichocheo vya mwili ndiyo kemikali zinazotumiwa na mwili kwenye kuratibu shughuli zote zinazohusu afya ya uzazi.
Vichocheo vya prolactin, mapungufu kwenye tezi za thyroid, kisukari pamoja na magonjwa yanayosababisha kutokea kwa uvimbe kwenye baadhi ya viungo vya mfumo wa uzazi mfano polycystic ovarian syndrome huchangia kuharibika kwa ujauzito. (8,9,10)
4. Mlango wa Kizazi
Mlango wa kizazi hupaswa kubaki umejifunga siku zote za ujauzito hadi muda wa kujifungua.
Kitendo chochote kitakachofanya mlango huu ufunguke pasipo uwepo wa dalili za uchungu, au kabla ya muda sahihi hufanya ujauzito uwe mashakani. (11,12)
Ni wastani wa ujauzito mmoja tu kati ya 100 ndiyo huharibika kutokana na changamoto hii. (13)
5. Mtindo wa Maisha
Uvutaji wa sigara au kuvuta moshi unaotolewa na mtu anayevuta sigara, matumizi ya pombe pamoja na madawa ya kulevya vinaweza kuwa chanzo cha kuharibika kwa ujauzito.
Mazao ya kemikali za bidhaa hizi huwa ni hatari kwa afya. (14)
Yanaweza kuharibu ujauzito pamoja na kusababisha mapungufu makubwa ya kimwili kwa mtoto atakaye zaliwa.
6. Mji wa Mimba
Mji wa mimba ni kiungo muhimu kwenye afya ya uzazi wa mwanamke.
Huutunza ujauzito kwa zaidi ya siku 280 na hufanya kazi kubwa ya kufanikisha hedhi kwa wanawake wasio na ujauzito. (15,16)
Wastani wa asilimia 24 ya wanawake wote ambao hupatwa na tatizo la kuharibika mara kwa mara kwa ujauzito huwa na mapungufu kwenye mji wa uzazi ambayo yanaweza kuwa na asili ya kuzaliwa nayo, au huyapata baada ya kuzaliwa. (17)
Vihatarishi
1. Umri
Umri pia huchukua nafasi kubwa kwenye kuamua hatma ya ujauzito.
Wanawake wenye umri wa miaka 35 huwa na asilimia 35 ya kuharibika kwa ujauzito, miaka 35-46 asilimia 20-35 na miaka zaidi ya 45 wana hadi asilimia 50.
2. Historia
Wanawake wenye historia ya kuharibika kwa ujauzito wa awali wana hadi asilimia 25 za kuharibika kwa ujauzito mwingine mpya.
3. Magonjwa
Shinikizo kubwa la damu, kisukari pamoja na ugonjwa wa figo, tezi za thyroid na moyo huongeza nafasi ya kuharibika kwa ujauzito.
4. Dawa
Siyo kila dawa ni salama kutumika wakati wa ujauzito.
Kuna baadhi ya dawa hufahamika kuwa na kazi ya kuzuia kutungwa kwa ujauzito, mfano ni tembe za dharura. Lakini, dawa kama isotretinoin ambayo hutumika kutibu tatizo la chunusi sugu huwa ni hatari sana.
Zinaweza kuharibu ujauzito pamoja na kusababisha changamoto kubwa za viungo kwa mtoto.
5. Lishe
Uimara wa afya ya mtoto hutegemea kwa kiasi kikubwa hali ya uthabiti wa lishe ya mama.
Upungufu mkubwa wa virutubisho muhimu kwa mama mjamzito unaweza kusababisha kuharibika kwa ujauzito. (18)
6. Sumu ya Chakula
Baadhi ya vimelea vya magonjwa huzaliana kwenye vyakula na kusababisha kuhara, maumivu makali ya tumbo, homa kali, kiungulia na kutapika. (24)
Sumu hii inaweza kusababishwa na upikaji hafifu wa vyakula, au pia kwa kula vyakula vichafu.
Bidhaa za maziwa, nyama na mayai ndiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa sumu ya chakula. (19)
Inaweza kuwa chanzo cha kuharibika kwa ujauzito.
7. Ajali na Vipigo
Ajali yoyote inayoweza kusababisha mwanamke apoteze damu nyingi, au mji wa uzazi upate changamoto zozote inaweza kusababisha kuharibika kwa ujauzito.
Hali ipo hivyo pia kwa vipigo.
Ni ngumu kuzuia ajali kwa kuwa baadhi yake hutokea kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa kibinadamu, lakini vipigo vinazuilika kabisa kwa asilimia 100.
Muhtasari
Stress, msongo wa mawazo pamoja na kufanya kazi au mazoezi ni baadhi ya mambo ambayo hayawezi kuharibu ujauzito. (20)
Aidha, ikiwa mwanamke hatakuwa na sababu zozote za kitabibu zinazotishia kuharibika kwa ujauzito, tendo la ndoa pia ni salama kabisa kufanyika muda wote na halina uhusiano wowote na kuharibika kwa ujauzito. (21)
Wanawake wanaopatwa na tatizo la kuharibika kwa ujauzito wasiwe na wasiwasi.
Ni asilimia moja pekee kati yao ndio huwa na uwezekano wa kupatwa tena na tatizo hili kwenye ujauzito wa mbele.