Presha: Sababu, Aina, Kinga na Tiba

6 Min Read

Shinikizo la damu ni nguvu, mgandamizo au msukumo unaotengenezwa na damu kwenye kuta za mishipa ya damu mwilini.

Ikitokea mgandamizo au msukumo huu umekuwa mkubwa sana kuliko kiasi cha kawaida, ugonjwa wa shinikizo la juu la damu hutokea.

Shinikizo la damu huandikwa kwa kutumia utaratibu wa tarakimu mbili.

Namba ya kwanza (ya juu) huwekwa kuwakilisha shinikizo la damu kwenye mishipa ya damu linalotengenezwa baada ya kusinyaa kwa kuta za moyo, au pale ambapo moyo unakuwa unatengeneza mapigo yake.

Kwa lugha ya kiingereza huitwa systolic blood pressure au SBP.

Namba ya pili (ya chini) husimama kuwakilisha shinikizo la damu kwenye mishipa ga damu linalotengenezwa baada ya kupumzika kwa moyo kati ya pigo moja na lingine.

Kwa lugha ya kiingereza huitwa diastolic blood pressure au DBP.

Jedwali hili linaonesha hatua za ugonjwa huu kwa undani wake;

AinaSBPDBP
KawaidaChini ya 120 mm HgChini ya 80 mm Hg
Juu kidogo120-129 mm HgChini ya 80 mm Hg
Ugonjwa hatua ya 1 130-139 mm Hg80-89 mm Hg
Ugonjwa hatua ya 2Zaidi ya 140 mm HgZaidi ya 90 mm Hg
DharuraZaidi ya 180 mm HgZaidi ya 120 mm Hg

Undani wake

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), shinikizo la juu la damu huongeza hatari ya kuugua magonjwa ya moyo, ubongo na figo.

Wastani wa watu bilioni 1.28 duniani wenye umri kati ya miaka 30-79 wanakabiliwa na tatizo hili.

Ni ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vya mapema duniani.

Aina Zake

Kuna aina kuu mbili za shinikizo la juu la damu.

  • Aina ya kwanza ya shinikizo la juu la damu
  • Aina ya pili ya shinikizo la chini la damu

Aina ya kwanza ya shinikizo la damu ni ile ambayo sababu za kutokea kwake huwa hazipo wazi. (1)

Aina hii ya shinikizo la damu inaweza kuhusishwa na sababu za urithi, mtindo wa maisha kama pombe, ulaji wa chumvi nyingi na sigara, uwepo wa magonjwa hasa kisukari, mafuta mengi kwenye mishipa ya damu pamoja na unene uliozidi.

Walau wastani wa asilimia 95 ya wagonjwa wote wa shinikizo la juu la damu huwa kwenye kundi hili. (2,3)

Aina ya pili ya shinikizo la damu ni ile ambayo huhusishwa na ugonjwa wa figo au moyo, mfumo wa vichocheo vya mwili au mapungufu kwenye changamoto zingine za viungo vya mwili. Inaweza pia kutokea wakati wa ujauzito.

Dalili

Shinikizo la juu la damu ni muuaji wa kimyakimya.

Wagonjwa wengi huwa hawaoneshi dalili zozote za uwepo wake hadi pale ambapo athari kadhaa zitaanza kuonekana kwenye baadhi ya viungo na mifumo ya mwili.

Baadhi ya dalili zake ni kizunguzungu, kupauka kwa rangi ya uso, maumivu ya kichwa, kuvuja kwa damu puani, kubadilika kwa mapigo ya moyo pamoja na kutokea kwa milio isiyoeleweka kwenye masikio.

Pia, dalili zingine za kupungua kwa uoni wa macho, uchovu bila sababu, kuweweseka na maumivu ya kifua na kutetemeka kwa misuli ya mwili zinaweza kuonekana.

    Shinikizo la juu la dharura huleta athari kubwa kwa afya hasa kwenye mfumo wa mzunguko wa damu na moyo, mfumo wa neva za mwili pamoja na kuharibu baadhi ya viungo vya mwili hasa figo.

    Athari

    Athari kubwa za shinikizo la juu la damu hutokea kwenye mishipa ya damu na moyo.

    Hufanya mishipa ya damu iwe dhaifu pamoja na kupunguza usafirishwaji wa hewa na damu kwenye moyo.

    Athari za kudumu za changamoto hii ni kupatwa na tatizo la maumivu makali ya kifua, shambulio la moyo, kusimama kwa moyo pamoja na kubadilika kwa mapigo ya moyo. (4,5,6)

    Ugonjwa huu huharibu figo na usipo dhibitiwa unaweza kupasua mishipa ya damu hivyo kusababisha tatizo la kiharusi.

    Tiba

    Msingi wa matibabu ya shinikizo la juu la damu huhusisha mambo yafuatayo;

    • Kupuguza uzito na kufanya mazoezi
    • Kupunguza unywaji wa pomba na matumizi ya sigara
    • Kuongeza ulaji wa matunda na mboga za majani huku ukidhibiti ulaji wa chumvi nyingi zaidi ya gramu 5 kwa siku
    • Matumizi ya dawa

    Matumizi ya dawa hulenga kudhibiti shinikizo la juu la damu pamoja na magonjwa mengine nyemelezi, au yale yanayoongeza ukubwa wa tatizo hili kwa mgonjwa.

    Kinga

    Unaweza kujikinga dhidi ya ugonjwa huu kwa kupunguza matumizi ya chumvi, kula matunda na mbogamboga nyingi pamoja na kufanya mazoezi ya mwili.

    Kupunguza matumizi ya pombe na sigara pamoja na kupunguza ulaji wa vyakula vinavyoongeza lehemu mbaya mwilini ni miongoni pia mwa njia zinazoweza kutumika kama kinga. Ni muhimu kujikinga na ugonjwa huu ambao huua zaidi ya watu milioni 7.5 duniani kila mwaka.

    Share This Article