Maziwa: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

4 Min Read

Wanyama wanaozaa hutengeneza maziwa ili kuwapatia chakula watoto wao.

Ng’ombe, mbuzi, ngamia na kondoo ni baadhi ya wanyama wa kufugwa wanaozalisha maziwa mengi.

Virutibisho

Maziwa ni chanzo bora sana cha protini, calcium na vitamini D.

Huwa pia na madini ya potassium, phosphorus, sodium, zinc, magnesium, virutubisho vya choline, riboflavin, vitamini A, vitamini B6 na B12 pamoja na folate.

Maziwa ya ng’ombe huwa na faida zifuatazo kwa afya.

1. Mifupa

Kwa mujibu wa Idara ya Chakula ya Marekani (USDA), kila gramu 100 za maziwa halisi huwa na kiasi cha 123 mg za madini ya calcium.

Madini haya huhusika na utengenezaji wa meno na mifupa imara. (1,2,3)

Huwa pia na vitamini D ambayo hushirikiana na calcium kwenye kuongeza ujazo wa mifupa.

2. Usingizi

Maziwa huwa na kampaundi mbili zinazosaidia kuleta usingizi, zinaitwa tryptophan na melatonin.

Kampaundi hizi zinaweza kuboresha usingizi hasa kwa watu wenye changamoto hiyo. (4)

Unaweza kuyatumia jioni au usiku, muda mchache kabla ya saa za kulala.

3. Sonona

Serotonin ni vichocheo vya mwili vinavyoongoza hali, hamu ya kula na usingizi.

Tafiti zinaonesha kuwa vichocheo hivyo vikifanya kazi kwa pamoja na vitamini D husaidia kutibu changamoto ya sonona, pamoja. (5,6,7)

Maziwa ni chanzo kizuri cha vitamini D.

4. Protini

Maziwa ni chakula chenye utajiri mkubwa sana wa protini.

Huusaidia mwili kwenye kurekebisha sehemu za misuli, seli na viungo vyake baada ya kupata majeraha. Protini ndiyo mjenzi mkuu wa tishu na viungo vyote vya mwili.

Hufaa sana kwa watu wanaofanya kazi ngumu, wafanya mazoezi pamoja na watu wanaopatwa na ajali.

5. Mifumo ya Mwili

Maziwa yamebeba virutubisho vinavyotumiwa na mifumo karibia yote ya mwili. Protini huratibu mfumo wa homoni na ukuaji wa mwili.

Virutubisho vya choline huboresha mijongeo ya misuli ya mwili, hali na kutunza kumbukumbu. (8,9)

Madini ya potassium huhitajika kwenye kuboresha mfumo wa mzunguko wa damu na moyo. Husaidia kuzuia magonjwa ya moyo, shinikizo kubwa la damu na kiharusi. (10)

Vitamini D huongeza uimara wa mfumo wa kinga mwili hasa katika kupambana na aina mbalimbali za saratani.

6. Uzito

Maziwa ni chakula bora sana kinachofaa kwenye kutunza uzito sahihi wa mwili, pamoja na kuondoa tatizo la uzito mkubwa kwa watu ambao tayari wameathirika na changamoto hii.

Huongeza uzalishwaji wa vichocheo ambavyo huufanya mwili ujisikie umeshiba. (11,12)

Hupunguza pia uzalishwaji wa vichocheo vya njaa mwili.

Aidha, huongeza uwezo wa mwili kwenye kutumia nishati zake vizuri.

Tahadhari

Maziwa siyo chakula kizuri kwa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja.

Pia, baadhi ya watu huwa na mzio wa maziwa ambao huwafanya wapatwe na maumivu makali ya tumbo, kuhara, ngozi kutokwa na mabaka, kupiga chafya pamoja na kutapika.

Changamoto hii ambayo husababishwa na uwepo wa aina ya protini inayoitwa alpha S1-casein kwa kiasi kikubwa hutokea kwa watoto chini ya umri wa miaka 6, lakini inaweza pia kutokea kwa watu wazima. (13,14)

Umakini mkubwa unahitajika kwa watu wanaoonesha tatizo hili kila wanapokunywa maziwa.

Wafike hospitalini kwa uchunguzi na matibabu.

Share This Article