Athari za Makundi Tofauti ya Damu kwenye Ujauzito (Rhesus Incompatibility)

5 Min Read

Ni muhimu sana kwa wachumba kufahamu makundi yao ya damu kabla ya kuamua kutengeneza familia, au kutafuta ujauzito.

Kuna baadhi ya vipimo ambavyo wote kwa pamoja wanaweza kufanya ili kujiweka tayari kuanzisha familia mpya.

Katika vipimo hivyo, utambuzi wa makundi ya damu ni jambo la msingi. Makundi ya damu hayana athari zozote za moja kwa moja kwenye kurahisisha upatikanaji wa ujauzito.

Isipokuwa, makundi haya huchochea kutokea kwa baadhi ya changamoto kubwa kwa afya ya mtoto.

Muingiliano wa Makundi ya Damu

Kila binadamu huwa na aina fulani ya kundi la damu linaloweza kuwa chanya au hasi.

Kwa mujibu wa tafiti, karibia asilimia 85 ya binadamu wote duniani huwa na makundi chanya ya damu.

Changamoto kubwa za kiafya na uzazi hutokea kwa kundi dogo la wanawake ambao aina za makundi yao ya damu huwa ni hasi.

Ikitokea mwanamke mwenye kundi lolote hasi la damu mfano A-, B-, AB- na O- akapata ujauzito wa mwanamme mwenye kundi lolote chanya la damu mfano A+, B+, AB+ au O+ kisha mtoto akarithi kundi chanya la damu kutoka kwa baba, mwili wa mwanamke hutengeneza kinga mwili ambazo huanza kumshambulia mtoto zikidhani ni kitu hatari kwa afya.

Kinga Mwili Hutengenezwa Vipi?

Wakati wa ujauzito, damu ya mama na mtoto huwa hazichanganyikani.

Lakini kuna baadhi ya nyakati ambazo damu hizi zinaweza kuungana hasa wakati wa kujifungua.

Inaweza kutokea kutokana na ajali yoyote wakati wa ujauzito, mama mjamzito kuvuja damu mara kwa mara wakati wa ujauzito, baada ya kutoa au kuharibika kwa ujauzito pamoja na harakati zozote zile za kubadili mkao wa mtoto akiwa kwenye mji wa uzazi. (1,2)

Tatizo hili linaweza pia kutokea ikiwa mwanamke atapokea damu ya mtu mwingine yeyete yule mwenye kundi chanya la damu wakati wa ujauzito.

Madhara Huonekana Lini?

Ujauzito wa kwanza hautaathiriwa kwa kuwa hutokea kabla mwili wa mwanamke haujazalisha kinga mwili za damu hiyo.

Hata hivyo, pamoja na kutokuonesha madhara kwa wakati huo, mwili wa mwanamke huachwa ukiwa umeandaliwa kikamilifu kupambana na hali hii kwenye ujauzito wa pili na kuendelea. (3)

Hii haimaanishi hadi mwanamke ajifungue mtoto kamili, bali kuharibika kwa ujauzito au utoaji wa ujauzito unatosha pia kusababisha madhara husika kwenye ujauzito wa pili na kuendelea.

Madhara

Madhara haya huwa hayatokei kwa mama. Mtoto ndiye mhanga mkuu.

Hufanya chembechembe nyekundu za damu ya mtoto zianze kuharibika kabla ya muda wake halisi.

Madhara ya jumla ni kusababisha upungufu mkubwa wa damu, manjano, kuharibika kwa ini pamoja na magonjwa ya moyo.

Kutokana na uharibifu huu mkubwa wa chembechembe nyekundu za damu, watoto wengi hufia tumboni kutokanana kukosa damu na hewa ya kutosha. (4,5,6)

Aidha, baadhi ya tafiti zinadai kuwa athari za tatizo hili hasa kwa watoto wa jinsia ya kiume wanaobahatika kupona kisha wakawa watu wazima huwa ni kuongezeka kwa nafasi ya kuugua magonjwa ya akili.

Kinga

Hauna haja ya kuogopa ikiwa kwenye uhusiano wenu mwanamke ana aina ya kundi la damu ambalo ni hasi huku mwanamme akiwa na aina ya kundi la damu ambalo ni chanya.

Baada ya kushika ujauzito, mwanamke hupaswa kuchomwa sindano ya kumlinda ili mwili usitengeneze kinga mwili kwenye wiki ya 28 ya ujauzito.

Sindano hii hutolewa pia ndani ya masaa 72 baada ya kujifungua kwa mwanamke. (7)

Huwa na lengo la kumfanya mwanamke asitengeneze kinga mwili ambazo zitaathiri ujauzito wake wa baadae, kuanzia mtoto wa pili na kuendelea.

Muhtasari

Jambo hili linaonesha umuhimu wa wapenzi kufahamu makundi ya damu zao kabla ya kuamua kupata ujauzito.

Kupitia ufahamu huo, itawasaidia kuepukana na changamoto hii ambayo ikitokea haijatibiwa vizuri inaweza kumfanya mwanamke awe anapoteza watoto kwenye kila ujauzito atakaopata baadae.

Hii siyo kwa wanawake waliojifungua tu, bali hata wale waliotoa mimba au mimba zao kuharibika kwa namna yoyote ile ni lazima wapate sindano hii ndani ya masaa 72 ili kujilinda.

Share This Article