Mgawanyiko wa Makundi ya Damu, Kutoa na Kupokea

4 Min Read

Hadi sasa, kuna aina 33 tofauti za miongozo ya kugawanya makundi ya damu.

Hata hivyo, utaratibu wa kugawa makundi ya damu kwa kutumia mfumo wa kundi mama ABO uliogunduliwa mwaka 1901 na Karl Landsteiner ndiyo unakubalika zaidi.

Kwa mujibu wa utaratibu huu, kuna makundi makuu manne ya damu ambayo ni kundi A, B, AB na O.

Ili kundi la damu liwe A ni lazima ukuta wa chembechembe nyekundu za damu ubebe taarifa za antijeni A, kundi B liwe na antijeni B, kundi AB liwe na antijeni zote mbili yaani A na B kwa pamoja na kundi O huwa halina antijeni yoyote.

Antijeni ni kitu chochote kile ambacho huamsha msisimko wa kinga za mwili katika kupambana.

Hasi na Chanya

Tumeona aina zote za makundi ya damu ambazo ni A, B, AB na O lakini bado kuna kitu kimoja ambacho kinapelea.

Makundi ya damu huwa hayaishii hapo tu, ni lazima pia yawe chanya au hasi.

Ukiachia taarifa za antijeni A au B ambazo huwepo kwenye ukuta wa chembechembe nyekundu za damu, sehemu hii hubeba pia aina moja ya protini inayoitwa Rh factor D, au maarufu zaidi kama RhD.

Ikitokea protini hii ipo kwenye chembechembe nyekundu za damu, kundi husika la damu litakuwa chanya, na ikitokea protini hiyo haipo basi kundi husika litakuwa hasi.

Karibia asilimia 85 ya binadamu wote huzaliwa na protini hii, hivyo huwa na makundi chanya ya damu. (1)

Ndio maana kupata mtu mwenye kundi lolote chanya la damu ni rahisi zaidi kuliko kupata mtu mwenye kundi lolote hasi la damu.

Kutoa na Kupokea

Kwa sasa utakuwa unaelewa kuwa aina kuu nne za makundi ya damu ni A, B, AB na O.

Kutokana na uwepo au kutokuwepo kwa protini za RhD, makundi haya yanaweza kugawanywa zaidi kwenye aina nane tofauti ambazo ni A+, A-, B+, B-, AB+, AB-, O+ na O-

Kwa mujibu wa takwimu, kundi O+ huchukua asilimia 35 ya makundi yote ya damu, O- asilimia 13, A+ asilimia 30, A- asilimia 8, B+ asilimia 8, B- asilimia 2, AB+ asilimia 2 na AB- asilimia 1.

Ili uweze kupokea damu, ni lazima kundi lako husika lifanane na kundi la mtu anayechangia damu hiyo.

Madhara

Kuna madhara makubwa ya kiafya yanaweza kutokea ikiwa mtu atapokea kundi la damu lisilo endana naye.

Mwamsho wa kinga mwili hutokea ambao hupelekea damu iliyopokelewa ichukuliwe kama adui anayepaswa kuuliwa.

Hivyo, chembechembe za damu huanza kupasuka, shinikizo la damu hushuka, figo hufeli kufanya kazi na damu mwilini huanza kuganda. Tatizo hili ni hatari na linaweza kuua.

Ili suala la kuchangia damu liwe na manufaa kwa afya, ni wahudumu wa afya ni lazima wahakikishe kuwa kundi la mchangiaji na yule anayepokea lipo sawa.

Muhtasari

Binadamu hurithi makundi ya damu kutoka kwa wazazi wao.

Kila mtoto anayezaliwa kwenye familia huwa na sifa ya kuwa na kundi la damu jumuishi linalofanana na wazazi wake.

Kama ilivyo kwa tabia zingine zilizo kwenye vinasaba vya urithi, kundi la damu haliwezi pia kubalika kwa namna yoyote ile baada ya kutungwa kwa ujauzito.

Share This Article