Kichaa cha mbwa ni ugonjwa hatari sana unaoweza kuua.
Hata hivyo, ungonjwa huu unazuilika kabisa kwa asilimia 100 kupitia chanjo.
Uambukizaji
Ni ugonjwa unaosababishwa na virusi.
Humpata binadamu kupitia mate ya mnyama aliyeathiriwa na virusi vya ugonjwa huu.
Inaweza kuwa kwa kung’atwa, kupitia mkwaruzo wa meno utakao husisha mate ya mnyama au kwa mate hayo kuingia mwilini kupitia vidonda, macho, pua na mdomo.
Virusi vya ugonjwa huu huitwa Rabies.
Takwimu
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaoweza kukingwa kupitia chanjo. Umesambaa duniani kote isipokuwa kwenye bara la Antarctica.
Mbwa ndiye mnyama anayeongoza kwa kusababisha vifo na maambukizi mengi duniani. Zaidi ya asilimia 99 ya visa vyote hutokana na mnyama huyu.
Ikiwa matibabu sahihi yatatolewa mapema, mhusika atakuwa salama, lakini ikitokea kuwa uzembe wa aina yoyote umefanyika hadi mgonjwa akaanza kuonesha dalili za ugonjwa huu, uhakika wa kifo huwa ni 100%
Wanyama Husika
Wanyama wote duniani wanayo sifa ya kubeba virusi wa kichaa cha mbwa.
Samaki, ndege na nyoka hawana sifa ya kubeba virusi hawa.
Linapokuja suala la kuambukiza, mbwa, popo na farasi ndiyo wanyama wanao ongoza kwa kusababisha kutokea kwa ugonjwa huu. (1,2)
Lakini kwa sababu za kiusalama, ni muhimu kupata msaada wa matibabu haraka inapotokea umeng’atwa na mnyama wa aina yoyote ile.
Ugunduzi wa Mnyama Mwenye Virusi
Hakuna namna yoyote unayoweza kufanya ili kugundua kuwa mnyama husika amebeba virusi vya kichaa cha mbwa.
Hata hivyo, baadhi ya wanyama hasa mbwa na farasi huanza kuonesha dalili mbaya za kubweka bila sababu, kuwa na nia ya kumng’ata kila mtu anayeonekana mbele yake pamoja na wanyama wengine au kwa kutokwa na mate mazito ambayo wakati mwingine huonekana kama mapovu.
Hata hivyo, sio kila mnyama aliye athirika huonesha dalili hizi.
Ni muhimu kuwa makini pasipo kujali anaonesha dalili au la.
Dalili
Hatukutaka kuandika dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa kwa kuwa siyo nia yetu kwa mtu aliyeathirika kufikia huku.
Ni kwamba, ikitokea mtu ameanza kuonesha dalili za ugonjwa huu kwa kuwa hakutibiwa ni dhahiri kuwa uwezekano wa kupona utakuwa unakaribia asilimia sifuri.
Kwa manufaa ya ufahamu, dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni Mafua, homa kali, maumivu ya kichwa, kuweweseka, wasiwasi, maumivu yanayochoma kama sindano endo la jeraha husika, kuogopa maji pamoja na kufeli kwa mfumo wa hewa.
Pia, dalili nhyingine ni ufeli kwa mfumo wa fahamu hali ambayo husababisha kifo.
Muda wa kuonekana kwa dalili huchukua wiki kadhaa, miezi au kwa baadhi ya watu huchukua hata mwaka mzima. (3,4)
Hutumia muda mrefu kwa sababu virusi hupaswa kusafiri kwanza hadi kwenye ubongo ili dalili zianze kuonekana.
Hutegemea pia umbali uliopo kati ya eneo la jeraha na ubongo, aina ya virusi husika pamoja na uwepo wa kinga ya awali kwa mhusika.
Kinga
Kinga ya kwanza kabisa ya ugonjwa huu ni kuchanja mbwa kwa kuwa ndio wanyama wanaoongoza kwa kusababisha visa vingi vya ugonjwa huu.
Watu wanaofanya kazi kwenye hifadhi za wanyama, au wanaoishi kwenye maeneo hatarishi wanaweza pia kupatiwa chanjo.
Ikiwa itatokea mtu amekutana na kadhia iliyo na mazingira hatarishi ya kuambukizwa ugonjwa huu anapaswa kufanya mambo yafuatayo;
- Kama ameng’atwa, anapaswa kusafisha kidonda kwa sabuni na maji tiririka kwa dakika 15
- Kama atakuwa karibu na famasi anunue 10% povidone kwa ajili ya kusafisha kidonda na kuzuia maambukizi ya bakteria
- Apate chanjo 5 za ugonjwa huu kuanzia siku 0, 3, 7, 14 na 28
- Siku 0 inamaanisha siku ya tukio au ajali husika
- Ikiwa daktari ataona inafaa, anaweza kumuongezea tiba ya rabies immunoglobulin (RIG)
Haya ni mambo ya msingi yanayopaswa kufanywa haraka, siku ya kwanza tu tangu tukio husika litokee.
Muhtasari
Uking’atwa na myama, au ukipatwa na mazingira yoyote hatarishi yanayoweza kukufanya uambukizwe ugonjwa huu fika hospitalini haraka.
Linapokuja suala la kichaa cha mbwa, kinga ni bora kuliko tiba. (5)
Msaada wa haraka huokoa maisha, uzembe wa aina yoyote ile hugharimu maisha.
Tuamke.