Vitamini A: Vyanzo, Uhitaji na Faida kwa Binadamu

4 Min Read

Ni vitamini inayoweza kuunganika na mafuta.

Hupatikana kwenye aina nne ambazo ni retinal, retinoic acid na retinyl ester.

Asilimia 80-90 ya vitamini A hutunzwa kwenye ini.

Aina Zake

Kuna aina kuu mbili za vitamini A ambazo hupatikana kutokana na uasili wake.

Aina hizo ni vitamini A inayotokana na mazao ya wanyama ambayo kitaalamu huitwa preformed vitamin A pamoja na ile inayopatikana kutoka kwenye mazao ya mimea ambayo huitwa provitamin A.

Vitamini A inayotokana na mazao ya wanyama hupatikana kwenye mfumo wa retinol huku ile inayotokana na mazao ya mimea ikipatikana kwenye mfumo wa carotenoid, au kwa upekee kabisa kama beta carotene.

Vyanzo

Unaweza kuipata kupitia vyakula vya asili, au kwa kutumia virutubisho maalum vyenye vitamini hii.

Ini, samaki, mayai, bidhaa za maziwa, mboga zenye rangi ya chungwa, manjano na kijani, matunda pamoja na mafuta ya mbegu za mimea ni vyanzo vizuri vya vitamini hii.

Aidha, inaweza kupatikana pia kwenye karoti, viazi ulaya, hoho nyekundu pamoja na nyanya.

Uhitaji

Kwa mujibu wa taasisi ya NIH, wanaume huhitaji kiasi cha 900 mcg kwa siku na wanawake huhitaji 700 mcg kwa siku.

Wanawake wajawazito huhitaji kiasi cha 770 mcg huku wale wanaonyonyesha wakihitaji 1300 mcg.

Kazi Zake

Vitamini A hutoa mchango mkubwa katika kuimarisha afya ya binadamu.

Huhitajika kwenye kuboresha afya ya macho, kutunza ngozi, afya ya uzazi, mfumo wa kinga mwili pamoja na kuboresha utendaji kazi wa viungo vya mwili hasa figo, moyo, kibofu, sikio la ndani na mapafu.

Kwa kuwa huwa na kiasi kikubwa cha viondoa sumu, huusaidia mwili katika kuzuia na kuoambana na magonjwa sugu mfano kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani. (1,2)

Huusaidia mwili kwenye kutengeneza askari wake wa kupambana na magonjwa wanaofahamika zaidi kama T helper cells, aina ya seli nyeupe za damu.  (3)

Hufanya pia kazi ya kuwasambaza askari hawa sehemu mbalimbali za mwili.

Upungufu

Upungufu wa vitamini hii husababisha kupungua kwa uoni wa macho hasa nyakati za usiku, pamoja na sehemu zenye giza.

Aidha, husababisha udumavu wa watoto, kuzeeka kwa ngozi pamoja na udhaifu wa kinga ya mwili. (4,5)

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), upungufu mkubwa wa vitamini A ni chanzo namba moja cha upofu duniani kwa watoto ambapo wastani wa watoto 250,000-500,000 kila mwaka hukumbwa na upofu, huku nusu yao wakifariki miezi 12 baadae.

Tahadhari

Hakuna kitu kizuri kisicho na madhara.

Matumizi ya vitamini A kupita kiasi yanaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya kama vile kiungulia na kutapika, kifafa, maumivu ya mifupa, kunyonyoka kwa nywele, kukauka kwa ngozi, manjano pamoja na kuathirika kwa ini. (6)

Kwa mama mjamzito, huongeza nafasi ya kuharibika kwa ujauzito pamoja na kujifungua mtoto mwenye changamoto nyingi za utengenezwaji wa viungo vyake.

Muhtasari

Unaweza kujikinga na madhara ya upungufu wa vitamini A kwa kutumia vyakula vyenye utajiri wa vitamini hii.

Unaweza pia kununua virutubisho maalumu vinavyopatikana madukani ambavyo huwa na vitamini A ya nyongeza.

Share This Article