Muda Sahihi wa Kushiriki Tendo la Ndoa Baada ya Kujifungua

4 Min Read

Ni salama kushiriki tendo la ndoa wakati wa ujauzito?

Ndio. Ni salama ikiwa hakuna sababu zozote za kitabibu zinazoweza kuzuia kufanyika kwake.

Swali jipya linaloibuka muda huu likihitaji majibu ni lini hasa mwanamke aliyejifungua kawaida, au aliye fanyiwa upasuaji asubiri kabla ya kuanza tena kushiriki tendo la ndoa.

Twende taratibu, utapata majibu

Mabadiliko Kimwili

Baada ya kujifungua, mwili wa mwanamke hupitia kipindi cha uponaji wa sehemu mbalimbali ambazo ziliumizwa wakati wa kujifungua.

Ni muda ambao mlango wa kizazi hutumia pia kujifunga kikamilifu. (1,2)

Aidha, mwili wa mwanamke huzalisha kiasi kidogo sana cha vichocheo vya estrogen wakati huu. 

Jambo hili husababisha ukavu wa uke na wengine huwapunguzia hamu ya kushiriki tendo la ndoa. (3,4,5)

Walau asilimia 83 ya wanawake hupitia changamoto ya kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa, ukavu wa uke, kubana au kutanuka sana kwa uke, kukosa hamu ya kushiriki tendo la ndoa pamoja na kupatwa na miwasho au maumivu baada ya kufika kileleni, au baada ya kumaliza kushiriki tendo la ndoa. (6)

Kutokana na uwepo wa changamoto hizi, kushiriki tendo la ndoa mapema sana huongeza nafasi ya kutoka kwa damu kwenye via vya uzazi, maumivu makali, kutonesha majeraha pamoja na kusababisha maambukizi makubwa.

Muda Sahihi

Wataalam wa afya hushauri kusubiri kwa walau wiki 4-6 kabla ya kushiriki tena tendo la ndoa.

Hii haijalishi mwanamke amejifungua kwa njia ya kawaida, au kwa upasuaji.

Ikiwa majimaji yenye uchafu wa uzazi yatakuwa yamekoma kutoka, saikolojia ya mama itakuwa imekaa vizuri na yeye mwenyewe atakuwa yupo tayari, tendo hili linaweza kufanyika.

Tahadhari

1. Ikiwa Kajifungua kwa Upasuaji

Mtindo mzuri wa kushiriki tendo hili unapaswa kutafutwa ili mshono usiumizwe.

Hii itasaidia kupunguza maumivu, pamoja na kumfanya mwanamke awe huru zaidi kushiriki pasipo uoga wa kupata maumivu.

2. Ukavu wa Uke

Unakumbuka tulisema kuwa wakati huu wanawake wengi hukabiliwa na tatizo la ukavu wa uke?

Najua umekumbuka.

Tendo la ndoa linapaswa kufanyika taratibu pasipo pupa, maandalizi ya kutosha yafanyike ili uke uzalishe majimaji yake pamoja na kutumia vilainishi ikiwa mbinu tajwa mwanzoni hazitasaidia.

Ni muhimu kukumbuka na kutambua mabadiliko mengi ambayo mwili wa mwanamke umepitia. 

Mabadiliko haya hayakuuacha salama uke wake. Fanyeni taratibu, baadae atazoea.

3. Kupata Ujauzito

Utafiti mmoja unaonesha kuwa baadhi ya wanawake wasio nyonyesha hupata hedhi yao ya kwanza baada ya wiki 6 tu tangu wajifungue. (7)

Hii itoshe kuwa taa nyekundu kwa kila mwanamke kwa kuwa baadhi ya wanawake hutumia muda mchache zaidi kuliko wiki 6.

Ni hakika kuwa mwanamke anaweza kupata ujauzito kabla hata hajaona hedhi yake ya kwanza baada ya kujifungua. (8,9)

Ni muhimu kuzungumza na wahudumu wa afya ili kuona namna gani utajikinga na ujauzito usio tarajiwa.

Njia za kisasa za uzazi wa mpango kama kitanzi, vijiti au majira vinaweza kutumika kwa kadri ambayo mtashauriana na mtoa huduma wa afya.

Muhtasari

Wanandoa hukutanishwa pamoja kimwili kupitia tendo la ndoa.

Wao wenyewe wanapaswa kuelewana juu ya lini washiriki tendo hili muhimu kwa ndoa yao.

Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia usalama wa mama kwa wakati huu. 

Matamanio ya kimwili yasizidi uhalisia.

Share This Article