Dalili za Hedhi: Hasira, Kuwashwa Matiti na Zingine

3 Min Read

Umewahi kuwaza kwa nini baadhi ya wanawake huwa na hasira sana wakati wa hedhi?

Huu ni mfano mmoja tu.

Wastani wa siku 7 kabla ya kutokea kwa hedhi, namba kubwa ya wanawake huingia kwenye kipindi kinachotawaliwa na mabadiliko makubwa ya kimwili na kihisia.

Mabadiliko haya kitaalam huongozwa na kitu kinachoitwa premenstrual syndrome.

Dalili Zake

Kipindi hiki huambatana na dalili za kuvimba matiti na kuwasha kwa matiti, maumivu ya kiuno na mgongo, hasira, kukosa hamu ya kula, kukosa usingizi, wasiwasi pamoja na msongo wa mawazo.

Dalili zingine ni choo kigumu au kuhara, tumbo kujaa gesi, kiungulia na kichefuchefu, kufumuka kwa chunusi, mkazo pamoja na kupungua kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa. (1,2,3)

Siyo kila mwanamke hupitia changamoto hizi lakini ni ukweli ulio wazi kuwa namba kubwa ya wanawake huzikabili.

Kwanini Hutokea?

Walau asilimia 48 ya wanawake duniani hupatwa na changamoto hizi huku asilimia 20 kati yao wakishindwa kabisa kutimiza majukumu yao ya kila siku kutokana na kuathiriwa sana na changamoto hii.

Pamoja na ukweli kuwa adha hizi husumbua wanawake wengi, hakuna taarifa za uhakika zinaoelezea kwanini hali hii hutokea.

Hata hivyo, mabadiliko kwenye kemikali na vichocheo vya mwili yanayotokea wakati huu yakihusisha hasa serotonin, norepinephrine, dopamine pamoja na acetylcholine huhusishwa ha kutokea kwa hali hii.

Aidha, kupungua mwilini kwa vichocheo vya estrogen na progesterone baada ya ovulation pamoja na muda unaokaribia hedhi huongeza ukubwa wa changamoto hizi.

Tumeshuhudia baadhi ya wanawake wakipatwa na hedhi bila kutanguliwa na dalili wala ishara yoyote. Hali zote hizi ni sawa, binadamu hawawezi kufanana kwa kila kitu.

Ushauri

Namna bora ya kupunguza uwepo wa dalili na changamoto zinazoambatana na hedhi ni kufanya mazoezi mara kwa mara ili kutunza utimamu wa mwili, kupunguza matumizi ya vyakula na vinywaji vyenye caffeine nyingi, sukari pamoja na chumvi nyingi walau wiki mbili kabla ya kutokea kwa hedhi, kupata muda mwingi wa kupumzika, kutokuvuta sigara, kuondoa mkazo pamoja na kutumia matunda na mboga za majani kwa wingi.

Ongeza matumizi ya virutubisho vyenye madini ya calcium.

Tiba

Dawa zenye homoni zinaweza kutumika katika kutibu hali hii.

Dawa zingine kama ibuprofen, naproxen, paracetamol pamoja na zingine husaidia sana kuondoa hali hii.

Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa dawa zote hizi huwa na athari kwa afya ya mtumiaji, zungumza na daktari au mfamasia kabla ya kuzitumia ili usijiingize kwenye matatizo makubwa yasiyo ya lazima.

Share This Article