Sababu, Athari na Matibabu ya Tatizo la Kukosekana kwa Hedhi

3 Min Read

Hedhi ya mwanamke hukoma pale tu mwanamke anapokuwa mjamzito, muda fulani baada ya kujifungua na pale anapofikia umri wa ukomo wake.

Wastani wa kawaida wa umri wa ukomo wa hedhi ni miaka 51, japo inaweza kuwahi zaidi au kuchelewa pia kutokana na umri wa mwanamke mwenyewe ambapo hedhi yake ya kwanza ilianza.

Hizi ni sababu za asili ambazo huwa ni lazima zitokee, hazisababishwi na uwepo wa shida yoyote kwenye afya ya mhusika.

Sababu Zingine

Sababu zingine ni matumizi ya njia za uzazi wa mpango hasa vijiti, majira, kitanzi na sindano za depo provera, uwepo wa changamoto za kiafya zinazopelekea mhusika atumie dozi ya dawa kali hasa zile za saratani, kifafa, shinikizo la damu pamoja na dawa mbalimbali za mizio.

Mtindo wa maisha huchukua nafasi kubwa katika kuchangia uwepo au kutokuwepo kwa hedhi.

Baadhi ya mambo kama uzito mdogo, kushiriki mazoezi na kazi ngumu pamoja na mkazo vinaweza kuathiri uwepo wa hedhi.

Mara nyingi mtindo wa maisha hupelekea kutokea kwa mvurugiko wa homoni ambao pia huchangia kukosekana kwa hedhi.

Sababu zingine ni;

  • Uvimbe kwenye kizazi
  • Matatizo kwenye vifuko vya mayai ya uzazi
  • Kuzaliwa bila uwepo wa baadhi ya viungo vya uzazi
  • Mapungufu kwenye utengenezwaji wa tundu la uke

Athari Zake

Kukosekana kwa hedhi kunaweza kusababisha mwanamke asipate ujauzito, pia husababisha kupungua kwa ujazo wa mifupa hasa ikiwa chanzo chake kikubwa ni mvurugiko wa homoni unaopekelea vichocheo vya estrogen visizalishwe katika viwango vinavyotakiwa.

Jambo hili huongeza hatari ya kuugua mara kwa mara na kupata maumivu makali kwenye maungio ya mwili, kiuno, mgongo, miguu pamoja na kuteguka au kuvunjika kwa mifupa ya mwili.

Ni vizuri uchunguzi wa haraka ukafanyika, hasa katika nyakati ambazo kukosekana kwa hedhi kunakuwa hakujasababishwa na ujauzito, unyonyeshaji pamoja na kukoma kwake kutokana na kufikia umri sahihi.

Tiba

Hutokana na chanzo chake kwa wakati huo.

Kubadili mtindo wa maisha pamoja na matumizi ya baadhi ya dawa hasa zile zenye homoni ndani yake husaidia kutibu tatizo hili.

Aidha, baadhi ya virutubisho hasa vile vya calcium na vitamini D vinaweza kujumlishwa kama sehemu ya tiba kwa mgonjwa.

Ni muhimu kuonana na daktari ambaye baada ya mazungumzo na uchunguzi, atashauri njia sahihi ya kulikabili tatizo hili.

Share This Article