Siyo kila mwanamke hupata idadi sawa ya siku za hedhi kila mwezi.
Utofauti wa kuwahi au kuchelewa kwa siku mbili kwenye baadhi ya mizunguko ya hedhi ni sawa, japo haipaswi kutofautiana kwa kiwango kikubwa.
Hedhi huamuliwa na mambo mengi sana ambayo huonesha athari za moja kwa moja kwenye utaratibu wake.
Mfano wa mambo yanayoweza kusababisha hedhi ibadilike mara kwa mara ni vyakula, mazingira, baadhi ya makundi ya dawa mfano dawa za kutibu kifafa na p2, maradhi mfano maambukizi ya sehemu ya juu ya mfumo wa uzazi, maarufu kama PID, matatizo kwenye vifuko vya uzazi, vinywaji, mfano pombe, tumbaku na bidhaa zake, msongo wa mawazo, Kisukari na kazi ngumu.
Pia, mambo kama Kiribatumbo, Mvurugiko wa homoni, Matatizo katika tezi za thyroid, Unyonyeshaji pamoja na uwepo wa Uvimbe wa aina yoyote kwenye kizazi yanaweza kusababisha hali hii.
Ni jambo la kawaida kabisa kwa mwanamke kupata mabadiliko ya hedhi anapohama kutoka sehemu moja aliyoizoea kwenda sehemu nyingine mpya au hata pale anapo badilisha utaratibu wa mlo, vinywaji, kazi pamoja na sababu zingine zilizotajwa hapo juu.
Hedhi inapobadilika ni vyema ukakaa chini kutafakari ili uweze kuona jambo gani geni umefanya, au limetokea kwenye maisha yako ambalo hukulizoea kabla.
Athari
Changamoto hii inaweza kumfanya mwanamke apitie kipindi kigumu katika kupata ujauzito pamoja na kujilinda ili asipate ujauzito usio tarajiwa.
Kila mzunguko wa hedhi huwa na siku zake maalum za kutungisha ujauzito. Kutokana na kubadilika huku, mwanamke anaweza kushindwa kufahamu siku sahihi za kupata ujauzito pamoja na siku salama za kujilinda ikiwa atatumia kalenda kama njia ya kupanga uzazi.
Ushauri
Mizunguko hii iendelee kufuatiliwa walau kwa kipindi cha miezi 3, kama tofauti kubwa itazidi kuonekana ni busara msaada wa daktari ukatafutwa.
Kubadilika kwa hedhi kunakosababishwa na mambo haya huwa hakudumu, ni jambo la miezi michache tu kisha hedhi hurejea kwenye mzunguko uliouzoea