Idadi ya wanawake wanaojifungua kwa njia ya upasuaji imekuwa inaongezeka kila mwaka.
Utafiti mmoja uliofanyika nchini Iran unaeleza kuwa wanawake wengi huchagua kujifungua kwa upasuaji kwenye ujauzito wa kwanza kutokana na sababu za uoga wa kujifungua kwa njia ya kawaida, au kutokana na kushauriwa na madaktari wao. (1)
Utafiti mwingine uliofanyika nchini Ufaransa unaonesha kuwa kutokana na uwepo wa sera za kuwezeshwa kwa wanawake, wengi wamekuwa hawataki kujifungua kwa njia ya upasuaji kwa kuwa huwafanya wasiridhike, pia huwafanya wajione dhaifu. (2)
Mazingira haya yanatoa picha inayo kinzana kwenye uchaguzi wa njia ya kujifungua miongoni mwa wanawake.
Sababu za Upasuaji
Chaguo la kwanza la njia ya kujifungua kwa mwanamke yeyote huwa ni kupitia mfereji wa uzazi, yaani uke.
Hata hivyo, sababu za kitabibu zinaweza kutumika kubadili njia hii ya asili hivyo kumfanya mwanamke ajifungue kwa upasuaji.
Baadhi ya sababu hizo ni kutokufunguka kwa mlango wa kizazi, uwepo wa matatizo kwenye kondo la uzazi, kuwa na watoto zaidi ya mmoja tumboni, kuwa na mtoto mkubwa sana, mtoto kutanguliza matako pamoja na mtoto hapati hewa ya kutosha.
Pia, sababu zingine ni kuwa na matatizo ya kiafya mfano shinikizo la juu la damu, kisukari au magonjwa ya moyo, kuwa na magonjwa ya zinaa yanayoweza kuambukizwa kwa mtoto, kutokupanuka kwa nyonga, au kuwa na nyonga ndogo, kuwa na mtoto mwenye changamoto za utengenezwaji wa viungo pamoja na kuwa na historia ya kujifungua kwa njia hii.
Kunapokuwa na changamoto kama hizi, uhai wa mama na mtoto huwa ni kipaumbele cha kwanza.
Upasuaji wa haraka huwa ni lazima ufanywe ili kuokoa uhai.
Kujifungua Kawaida Baada ya Upasuaji
Kilio cha wanawake wengi huwa kipo hapa.
Tafiti zinaonesha kuwa zoezi la kujifungua kawaida baada ya upasuaji huwa na ufanisi wa wastani kati ya asilimia 60-80. (1,2)
Mwanamke anaweza kabisa kujifungua kwa njia ya kawaida ikiwa sababu zilizopelekea ajifungue kwa njia ya upasuaji hazikuwa endelevu.
Mwanamke anapaswa kusubiri walau miezi 18-24 ndipo apate ujauzito mwingine. Hii itafanya kovu la mwanzo liweze kupona vizuri.
Aidha, mtoto anapaswa kuwa na uzito wa kawaida, awe na mkao mzuri tumboni pia kichwa kiwe kimegeuka.
Ili maamuzi sahihi yaweze kufanyika, mama mjamzito anapaswa kuzungumza na daktari wake mapema kabla ya siku ya uchungu ili waweze kushauriana na kuamua pamoja.
Kujifungua kwa njia ya kawaida baada ya upasuaji inawezekana kabisa, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa siyo kila mwanamke hufaulu kuingia kwenye nafasi hii.
Hivyo, ikitokea daktari wako kaamua vinginevyo usilaumu.
Athari Zake
Ikiwa mama atalazimisha kujifungua kawaida, kuna hatari kubwa ya kushindwa kusukuma mtoto hadi mwisho.
Aidha, maambukizi makubwa ya damu, kuchanika kwa mji wa uzazi pamoja na kupoteza damu nyingi kunaweza kutokea. (3)
Mambo haya ni hatari kwa uhai wa mama na mtoto, yanaweza pia kusababisha kifo.
Faida za Kujifungua Kawaida Baada ya Upasuaji
Wanawake hupitia kipindi kigumu cha maumivu ya mshono pamoja na changamoto zingine za kimwili na kiakili.
Kujifungua kawaida baada ya upasuaji huwa na faida za kutokuongeza maumivu ya mshono wa mwanzo, hurahisisha uponaji wa haraka, hupunguza nafasi ya kupatwa na maambukizi pamoja na kupoteza damu nyingi.
Hata hivyo, bado tunasisitiza kuwa siyo jambo rahisi, na daktari anaweza asiruhusu jambo hili kutonana na hatari tulizotaja awali.
Njia Bora ya Kujifungua
Linapokuja suala la kujifungua, hakuna njia iliyo bora kuzidi nyingine.
Njia zote hulenga kuuleta uhai mpya duniani huku usalama wa mama ukitunzwa.
Ni imani na dhana potofu kudhani kuwa mwanamke aliyejifungua kawaida ni bora kuliko yule aliyejifungua kwa njia ya upasuaji.
Kama mama na mtoto wapo salama, inakuwaje njia dhaifu?
Muhtasari
Mwanamke aliyejifungua kwa njia ya upasuaji anapaswa kufika kliniki mara kwa mara ili aweze kupata ushauri sahihi pamoja na kuandaliwa vizuri anapokuwa anaelekea kwenye kipindi cha kujifungua.
Kuna tabia ya kupata ushauri mitaani, pamoja na wanawake wengine ambao waliwahi pia kupitia hali hii mwanzoni. Hii ni tabia mbaya na haifai.
Huwafanya wanawake wachukue maamuzi ambayo mara nyingi huwa siyo mazuri kwao. Hali ya mwanamke mwingine haiwezi kufanana na hali yako.
Tuwaamini watumishi wetu wa afya, tuwasikilize na kufuata miongozo wanayotupatia.