Binadamu huwa na figo mbili. Viungo hivi vyenye kazi kubwa ya kuchuja damu mwilini huwa na umbo linalofanana na maharage.
Huondoa maji na uchafu wa kwenye damu kisha kuvitoa nje ya mwili kupitia mkojo hivyo figo zinapoharibika uchafu huu hubaki mwilini na kuleta athari kwa afya.
Aidha, hufanya kazi za kuweka uwiano sawa wa tindikali na alkali za damu, kutengeneza sukari kwenye nyakati ambazo mwili wa binadamu huwa na upungufu mkubwa wa sukari, hutengeneza protini inayoitwa renin ambayo hutumiwa na mwili kwenye kuongeza shinikizo la damu pamoja na kuzalisha vichocheo vya calcitriol na erythropoietin ambavyo huusaidia mwili kufyonza vizuri madini ya calcium pamoja na kutengeneza damu mtawalia.
Aina Zake
Tunaweza kuugawa ugonjwa huu kwenye aina mbili.
- Ugonjwa wa figo wa muda mfupi
- Ugonjwa wa figo wa muda mrefu (sugu)
Ugonjwa wa figo wa muda mfupi ni ule ambao hutokea ghafla, huwa haudumu kwa zaidi ya miezi 3.
Mara nyingi husababishwa na ajali, kuvimba kwa tezi dume, kupoteza kwa damu na maji mengi, matumizi ya dozi fulani za dawa, kifafa cha mimba pamoja na uwepo wa maambukizi makubwa ya damu. (1,2)
Ikiwa ugonjwa wa figo wa muda mfupi utadumu kwa zaidi ya miezi 3, utabadilika kuwa ugonjwa wa figo wa muda mrefu (sugu).
Visababishi vikubwa ni ugonjwa wa kisukari pamoja na shinikizo kubwa la damu. Inaweza pia kusababishwa na maambukizi ya muda mrefu ya virusi, kuvimba kwa vichujio vidogo vya figo, magonjwa ya kurithi ya figo, maambukizi ya mara kwa mara ya figo pamoja na saratani ya figo. (6,7)
Ugonjwa wa figo wa muda mfupi hutibika kabisa.
Ikiwa kwa hatua hii ya awali mgonjwa atashindwa kutambulika kwa kutokuonesha dalili, kwenda hospitalini kupata matibabu au pengine kupuuzia tiba anazopatiwa, ugonjwa huu utaendelea kuziharibu figo.
Hugeuka kuwa sugu na hatimaye huzifanya figo zishindwe kabisa kufanya kazi.
Hii ndiyo hatua ya mwisho ya ugonjwa wa figo ambayo ndiyo kubwa, hatari na mbaya zaidi.
Dalili
Dalili za awali za ugonjwa wa figo ni kuongezeka sana kwa uzito wa mwili pamoja na kuvimba kwa mwili hasa sehemu za miguu, uso na mikono.
Hii husababishwa na ukweli kuwa mwili huwa hauwezi tena kutoa uchafu na maji.
Dalili zingine ni kupungua kwa hamu ya kula, kiungulia, kutapika, uchovu, degedege, kuzimia pamoja na kujisaidia kiasi kidogo sana cha mkojo ambacho mara nyingi huwa na harufu kali pamoja na rangi nyeusi. (3)
Kwenye hatua ya mwisho kabisa ya ugonjwa huu, mgonjwa huanza kupungua uzito wa mwili, kubadilika kwa rangi ya ngozi kuwa manjano, kuuma kwa misuli ya mwili, kutetemeka kwa miguu, kwikwi, kujisaidia choo chenye damu, kukosa usingizi pamoja na kupungua kwa uwezo wa kuhimili tendo la ndoa kwa jinsia zote.
Ugunduzi
Uwepo wa moja kwa moja wa dalili zilizo wazi unaweza kutumika kama njia ya kwanza ya ugunduzi wa uwepo wa tatizo hili.
Aidha, daktari atachukua historia ya mgonjwa pamoja na kufanya vipimo kadhaa vya mkojo na damu.
Vipimo vya kuchukua sehemu ndogo ya figo pamoja na ultrasonography vinaweza pia kufanyika.
Tiba
Hakuna njia yoyote inayoweza kutumika kutibu tatizo la ugonjwa sugu wa figo.
Msaada wa matibabu hutolewa ili kupunguza athari za tatizo pamoja na kuboresha maisha ya mgonjwa.
Aidha, kudhibiti vyanzo vya tatizo hili mfano kisukari na shinikizo la juu la damu kupita dawa huwa ni sehemu ya tiba muhimu ya ugonjwa huu.
Hatua ya mwisho kabisa ya matibabu ya ugonjwa huu ni huduma ya kuchuja damu kupitia mashine maarufu kama dialysis au upandikizwaji wa figo mpya.
Mambo Muhimu
Mgonjwa anapaswa kubadili mtindo wa maisha yake.
Anapaswa kufanya mazoezi, kupunguza matumizi ya pombe, sigara na matumizi ya dawa pasipo kupata ushauri wa daktari.
Vyakula lazima visiwekewe chumvi nyingi pamoja na kupunguza ulaji wa vyakula vyenye protini nyingi, mafuta pamoja na madini ya potassium.
Ni muhimu pia kuhakikisha kuwa uzito wa mwili umetunzwa vizuri. Maji ni kitu cha thamani kubwa sana kwenye afya ya binadamu, lakini kwa mgonjwa wa figo hupaswa kupunguzwa.
Mgonjwa asinywe maji mengi.
Muhtasari
Upandikizaji wa figo siyo jambo rahisi kutokana na uwepo wa wachangiaji wachache wa kiungo hiki ambao wamekuwa wanapungua idadi kila mwaka.
Huduma ya dialysis ni ghali sana, inafikia hadi milioni moja kwa wiki na hupaswa kufanywa kwenye kipindi chote cha maisha.
Ni muhimu kufuata mtindo bora wa maisha kwa kufanya mazoezi, kutunza vizuri uzito wa mwili, kutumia vizuri dawa kwa kufuata dozi sahihi na kupunguza uvutaji wa sigara.
Watu wenye kisukari na shinikizo la juu la damu wapo kwenye taa nyekundu ya kupatwa na ugonjwa huu.
Wanapaswa kufuata masharti sahihi ya matumizi ya dawa zao pamoja na kuhakikisha kuwa afya zao zinabaki salama muda wote.