Sababu, Athari na Matibabu ya Kifafa cha Ujauzito

3 Min Read

Ni imani yetu kuwa leo siyo mara yako ya kwanza kusikia mada hii.

Ni tatizo hatari sana linalotokea wakati wa ujauzito ambalo husababishwa na uwepo wa shinikizo kubwa la damu.

Changamoto hii inaweza pia kutokea muda mchache baada ya kujifungua.

Kifafa cha mimba hutanguliwa na uwepo wa ongezeko la shinikizo la damu wakati wa ujauzito. Shinikizo hili kubwa lisipo dhibitiwa vizuri hukomaa na kuendelea kuwa kubwa zaidi. Athari yake ni kusababisha kifafa cha mimba.

Dalili

Uwepo wa shinikizo kubwa la damu huenda sambamba na uwepo wa dalili hizi ni uwepo wa protini kwenye mkojo, kupungua kwa uwezo wa macho katika kuona, maumivu makali ya kichwa, kuishiwa na pumzi mara kwa mara, maumivu chini ya mbavu, kuvimba sana kwa mwili pamoja na kupungua sana kwa haja ndogo.

    Wakati huu, afya ya mtoto huathirika kwa kuwa mwili wa mama huwa hauwezi kumpatia virutubisho na hewa ya kutosha.

    Pia, baadhi ya wanawake hupatwa na Degedege, kifafa pamoja na Kuzimia.

    Nani Yupo Hatarini?

    Wanawake wenye shinikizo la juu la damu huwa kwenye hatari kubwa ya kupatwa na kifafa cha mimba.

    Aidha, makundi haya pia huwa yapo hatarini;

    • Kuwa na miaka chini ya 20, au zaidi ya miaka 40
    • Kuwa na ujauzito wenye watoto zaidi ya mmoja
    • Ujauzito wa kwanza
    • Kisukari
    • Magonjwa ya figo
    • Kuwa na uzito mkubwa
    • Kutoka kwenye familia yenye historia hii

    Wanawake wenye changamoto ya upungufu wa damu wapo pia kwenye hatari ya kupatwa na kifafa cha mimba. Ni muhimu kufahamu mambo haya ili kujua uwezekano wa kupatwa na hali hii.

    Athari

    Humfanya mtoto azaliwe akiwa na afya duni kwa kuwa hupokea hewa na virutubisho vichache kutoka kwa mama yake.

    Ni chanzo kikubwa cha kuzaliwa kwa watoto njiti, watoto wenye kifafa, mtindio wa ubongo pamoja na matatizo ya kuona na kusikia.

    Kifafa cha mimba kinaweza pia kusababisha kifo kwa mama na mtoto, kiharusi, upofu pamoja na kuvuja kwa damu nyingi wakati na baada ya kujifungua.

    Ugunduzi

    Uwepo wa shinikizo la juu la damu pamoja na protini kwenye mkojo ni viashiria muhimu sana katika kutambua uwepo wa hali hii.

    Vipimo vingine vya damu, mkojo au ultrasound vinaweza kufanywa kwa kadri ambavyo daktari ataona inafaa.

    Vyote hivi hugunduliwa mapema wakati wa mahudhurio ya Kliniki za uzazi.

    Tiba

    Tiba yake hutegemea na aina ya dalili zinazo onekana.

    Baadhi ya dawa kama hydralazine na magnesium sulfate zinaweza kufaa wakati huu.

    Ikiwa muda wa kujifungua utakuwa umefika, upasuaji wa haraka unaweza kufanyika ili kunusuru uhai wa mama na mtoto.

    Muhtasari

    Unaweza kujikinga na kifafa cha mimba kwa kutunza vizuri uzito wa mwili, kuacha kuvuta sigara pamoja na kufanya mazoezi mara kwa mara.

    Ikiwa una kisukari, ugonjwa wa figo au shinikizo la juu la damu ni lazima umeze vizuri dawa zako.

    Magonjwa haya huongeza hatari ya kutokea kwa kifafa cha mimba.

    Share This Article