Mfumo wa uzazi wa mwanamme huundwa kwa viungo vingi.
Mojawapo ya viungo hivyo ni tezi dume.
Huwa na kazi ya kuzalisha majimaji yenye virutubisho vinavyohitajika kwenye kuboresha afya ya mbegu za kiume, pamoja na kurahisisha usafirishwaji wake baada ya kutolewa nje wakati wa tendo la ndoa. (1,2,3)
Ni kiungo chenye maana kubwa kwa afya.
Kuvimba
Tezi dume hupitia hatua mbili za ukuaji.
Ukuaji wa kwanza hutokea wakati wa kubalehe ambapo huongezeka ukubwa wake mara mbili zaidi.
Hatua ya pili ya ukuaji huanza kutokea kwenye umri wa miaka 25 na huendelea karibia kipindi chote cha maisha ya mwanamme. (4,5)
Kuvimba kwa tezi dume hutokea kwenye hatua hii ya pili ya ukuaji wake.
Sababu za Kuvimba
Ifahamike kuwa uvimbe huu sio saratani.
Hivyo, kuvimba kwa tezi dume na saratani ya tezi dume ni magonjwa mawili tofauti japo katika mazingira fulani yanaweza kuonekana kwa pamoja.
Sababu zinazopelekea kutokea kwa tatizo hili huwa hazipo wazi sana.
Hutokea kupitia mchakato wa kawaida wa ukuaji wa tezi dume, ambao katika mazingira ya kawaida huwa ni endelevu.
Nadharia
Kuna walau nadharia nne zinazoelezea sababu za kutokea kwa changamoto hii.
Kuongezeka kwa vichocheo vya dihydrotestosterone kunakosababishwa na umri mkubwa, kusisimka upya kwa taarifa msingi za ukuaji wa kiungo hiki zilizo kuwepo tangu siku za mwanzo kabisa za ujauzito, kuongezeka kwa namba ya seli shina za tezi dume pamoja na kuongezeka kwa vichocheo vya estrogen ni nadharia zinazoelezea sababu zinazo pelekea kuvimba kwa tezi dume.
Nadharia hizi hutumika kutokana na namna ambavyo ugonjwa huu umetokea kwa mhusika.
Vihatarishi
Wanaume wenye hali hizi wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupatwa na changamoto hii;
- Umri zaidi ya miaka 40
- Historia ya uwepo wake kwenye familia au ukoo
- Uzito mkubwa
- Magonjwa ya moyo
- Kisukari
- Kutokufanya mazoezi
Dalili
Kuvimba kwa tezi dume huambatana na uwepo wa dalili nyingi.
Baadhi ya dalili hizo ni kwenda haja ndogo mara kwa mara, kupungua kwa uwezo wa kudhibiti mkojo, kupungua kwa kasi na nguvu ya kutoka kwa mkojo, maumivu wakati wa haja ndogo, pia baada ya kufika kileleni wakati wa tendo la ndoa, kubadilika kwa rangi na harufu ya mkojo, kushindwa kutoa mkojo wote wakati wa haja ndogo pamoja na uwepo wa damu kwenye mkojo.
Dalili hizi huwa hazisumbui sana mwanzoni, pengine zinaweza zisionekane kabisa.
Kadri tatizo linavyozidi kuwa kubwa ndivyo dalili pia huongezeka.
Athari
Uvimbe huu husababisha kuziba kwa njia ya mkojo.
Hii inaweza kufanya mhusika augue ugonjwa wa UTI mara kwa mara, kuharibika kwa kibofu cha mkojo na figo pamoja na kutokea kwa mawe kwenye figo.
Matibabu
Baada ya kufanyika kwa vipimo na kuthibitisha uwepo wake, matibabu yataanza mara mara.
Yanaweza kufanyika kwa kubadili mtindo wa maisha, matumizi ya dawa au kwa kupitia upasuaji. (6)
Ushauri
Mtindo wa maisha unapaswa kubadilika wakati huu.
Mgonjwa anashauriwa kupunguza matumizi ya pombe pamoja na vinywaji vyenye caffeine, kufanya mazoezi, kuongeza ulaji wa mboga za majani, vitamini D, madini ya zinc pamoja na kula vyakula laini ili kuzuia kutokea kwa tatizo la choo kigumu ambalo linaweza kuongeza maumivu pamoja na athari za ugonjwa huu. (7)
Uvimbe wa tezi dume unatibika.