Ukitaka ufurahie utamu wa tikiti maji, liweke kwanza kwenye friji.
Huu ni msemo maarufu sana mtaani ulio na ukweli kwa kiasi fulani.
Virutubisho
Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), sehemu kubwa ya tikiti maji huundwa na maji. Hii inasadifu jina lake.
Huwa pia na protini, nyuzi lishe, sukari, nishati, madini chuma, calcium, magnesium, potassium, zinc, copper, asidi ya foliki, vitamini A na vitamini B12 pamoja na viondoa sumu vingi.
Unapotumia tunda hili unakuwa na uhakika wa kupata faida nyingi kwa afya.
Baadhi yake ni hizi;
1. Mazoezi
Unafanya mazoezi kila siku?
Usiwaze mara mbili ni tunda gani linakufaa.
Tikiti maji husaidia kupunguza maumivu ya misuli pamoja na kurejesha utimamu wa mwili baada ya kushiriki mazoezi magumu. (1,2)
Uwepo wa kemikai za L-citruline nguvu kubwa iliyo nyuma ya mafanikio haya.
2. Presha
Kemikali za l-citrulline, l-arginine pamoja na viondoa sumu vya lycopene husaidia kudhibiti ongezeko la shinikizo la damu.
Aidha, huulinda moyo pamoja na mishipa ya damu kwa kuharibu mafuta mabaya. (3,4)
Ni tunda zuri kwa kila mtu, lakini zaidi kwa wagonjwa wa shinikizo la juu la damu.
3. Mfumo wa Chakula
Zaidi ya asilimia 90 ya tikiti maji huwa ni maji.
Huwa pia na nyuzi lishe zinazofaa kwa afya ya binadamu.
Huboresha mfumo wa chakula pamoja na kutibu changamoto ya choo kigumu.
4. Sumu
Ukiulizwa utaje tunda lenye viondoa sumu vingi kwanini isiwe tikiti maji?
Huwa na kiasi kikubwa sana cha viondoa sumu vitamini C, carotenoids, lycopene na cucurbitacin E.
Huzilinda seli za mwili dhidi ya aina mbalimbali za sumu zinazo hatarisha maisha ya binadamu.(5,6)
Utake nini kingine?
5. Saratani
Saratani ni mojawapo ya magonjwa yanayo ondoa uhai wa watu wengi duniani.
Kwa mwaka 2020 pekee, zaidi ya watu milioni 10 duniani walipoteza uhai kutokana na ugonjwa huu.
Lycopene huharibu sumu za oxygen huru pamoja na kulinda vinasaba vya seli ili visibadilike kuwa saratani.
Husaidia katika kupambana na aina mbalimbali za saratani mwilini.
Ni muhimu ukitumia tunda hili.
6. Chanzo cha Maji
Karibia kila kazi inayofanyika mwilini huhitaji maji.
Waswahili husema usipoyanywa, basi utayaoga. Tikiti maji ni chanzo bora sana cha maji.
Tunda hili ni muhimu hasa kwa watu ambao kwa tabia ya asili huwa ni wavivu kunywa maji. Linafaa pia kwa wanawake wajawazito ambao kwa kiasi kikubwa huchukia maji. (7)
Usipokunywa nyumbani kwako au ukaamua kula tikiti maji, basi tutakutundikia hospitalini ukiwa kitandani.
7. Viagra Asili
Huwa na amino acid zinazojulikana kama citrulline ambazo hupanua mishipa ya damu hasa ile inayopatikana kwenye viungo vya uzazi vya mwanamme.
Hufanya kazi kama zilivyo viagra hivyo huitwa viagra asili.
Tunda hili linaweza kusaidia kuboresha afya ya uzazi kwa wanaume walio na matatizo katika kushiriki tendo la ndoa.
8. Uvimbe
Tikiti maji huwa na viambato vinavyo dhibiti uvimbe.
Hii inatokana na uwepo wa vitamini C, lycopene na viondoa sumu vinigine. (8,9)
Hufanya hivyo kwa kuharibu kemikali zinao amsha msisimko wa uvimbe mwilini.
9. Ngozi
Unatumia vipodozi gani kutunza afya ya ngozi yako? Vinakusaidia?
Jaribu kutumia tikiti maji.
Vitamini A na vitamini C hutoa mchango mkubwa katika kutibu chunusi, kuzuia kuzeeka kwa ngozi, kutokea kwa makunyazi pamoja na kuzifufua upya seli za ngozi.
10. Uzito
Tikiti maji husaidia kutunza uzito wa mwili.
Katika utafiti mmoja uliofanyika kwa wiki 4 mfululizo kwa watu 33 waliokuwa na uzito mkubwa, majibu yalionesha kupungua kwa uzito wa mwili. (10)
Hii ilihusisha pia kutokea kwa uwiano mzuri kati ya urefu na uzito.
11. Ubongo
Umewahi kusikia kuhusu choline?
Huboresha miondoko ya misuli ya mwili, huongeza uwezo wa ubongo kwenye kufikiri na kutunza kumbukumbu, huongeza ufanisi wa mfumo wa usafirishwaji wa taarifa za mwili pamoja na kutengeneza ubongo imara kwa watoto.
Muhtasari
Inaaminika kuwa tunda hili lililimwa kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 5000 iliyopita Kaskazini mashariki mwa bara la Afrika.
Ni tunda tamu, linafaa kwa kila mtu.
Jitahidi ulipate.