Mojawapo kati ya matunda ambayo hayapaswi kukosekana nyumbani kwako ni parachichi.
Tunda hili limesheheni virutubisho vingi vinavyofaa kwa kila rika na umri.
Virutubisho
Hubeba kiasi cha kutosha cha vitamini C, E, K, B6, niacin, asidi za foliki pamoja na madini ya magnesium, manganese, potassium, nyuzi lishe pamoja na mafuta mazuri.
Aidha, huwa pia na viondoa sumu vya kutosha pamoja na asidi ya mafuta ya omega 3.
Parachichi huwa na faida zifuatazo kwa afya;
1. Ujauzito na Kunyonyesha
Mwanamke mjamzito huhitajika kupata virutubisho vya kutosha ili kujilinda mwenyewe, pamoja na kumlinda mtoto aliye tumboni.
Mfano, ni muhimu kupata virutubisho vya asidi ya foliki ili kumkinga mtoto asizaliwe na tatizo la mgongo wazi pamoja na kumfanya awe na mfumo bora wa fahamu.
Tunda hili hufaa kwa kuwa huondoa magonjwa ya asubuhi kwa wajawazito, kuondoa changamoto ya choo kigumu, kuongeza uzalishwaji wa maziwa pamoja na kutoa uhakika wa virutubisho vya kutosha kwa mama na mtoto. (1,2,3)
Tunda hili linafaa sana kwa mwanamke mjamzito pamoja na yule anaye nyonyesha.
2. Macho
Tunda hili huboresha afya ya macho.
Hupunguza kasi ya kuzeeka kwa tishu za macho, huongeza uoni pamoja na kupunguza athari za mionzi mikali ya mwanga wa jua inayoweza kuathiri afya ya macho.
Mambo haya ni muhimu sana hasa kwa wazee, watu wenye changamoto za macho pamoja na wale wenye magonjwa makubwa hasa kisukari.
Uwepo wa viondoa sumu vya beta carotene, lutein na zeaxanthin ndio siri kubwa ya uwezo huu. (4)
Imarisha afya ya macho yako kwa kula parachichi.
3. Saratani
Tafiti nyingi za kisayansi zinaeleza kuwa baadhi ya kemikali zinazopatikana kwenye parachichi huathiri mfumo wa taarifa za seli za saratani.
Huzifanya zitengeneze taarifa hasi ambazo hupelekea zijiue zenyewe.
Aidha, hudhibiti ukuaji wake pamoja na kuleta ahueni kwa mgonjwa. (5,6)
Kwa kuwa watu wanaotumia tiba za mionzi hupatwa na changamoto ya kutapika pamoja na kupata maudhi mengi, tunda hili husaidia pia kupambana na maudhi hayo.
4. Mfumo wa Chakula
Huwa na kiasi kikubwa cha nyuzi lishe.
Ni tunda zuri kwa kuboresha mfumo wa chakula, kupunguza uwezekano wa kuugua saratani ya utumbo mkubwa pamoja na kutibu changamoto ya choo kigumu.
5. Sonona
Folate huhusishwa na kutibu changamoto za sonona.
Huusaidia mwili kwenye kutengeneza norepinephrine, serotonin na dopamine ambazo hupunguza dalili za sonona pamoja na kuzuia isitokee kwa watu ambao bado hawajapata. (7)
Pamoja na sonona, folate husaidia pia kupambana na changamoto mbalimbali za magonjwa ya akili.
6. Sumu
Parachichi huwa na utajiri mkubwa wa viondoa sumu.
Kuna vitamini C na E pamoja na carotenoid lutein.
Vyote hivi huharibu sumu zinazoweza kuwa hatari kwa afya ya binadamu. Huzilinda pia seli za mwili ambazo ndio kitovu cha uhai wa binadamu.
7. Uzazi
Vitamini E hufahamika zaidi kama vitamini inayopambana na ugumba na utasa.
Husaidia pia kwenye kuzuia ujauzito usiharibike pamoja na kuongeza uzalishwaji wa ute rafiki kwa mwanamke ambao huwezesha mbegu za kiume ziweze kuogelea vizuri.
Kwa namna ya kipekee kabisa, huboresha afya ya uzazi wa mwanaume kwa kuongeza ubora wa mbegu za kiume. (8)
Watu wanaopitia changamoto ya kupata watoto wanaweza kutumia tunda hili mara kwa mara.
8. Moyo
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa watu milioni 19.7 hufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa ya moyo.
Parachichi huboresha afya ya moyo.
Hii hutokana na uwepo wa mafuta mazuri yanayofaa kwa afya ya binadamu.
9. Uzito Mkubwa
Kuna nambo mengi sana yanayochangia kutokea kwa ongezeko kubwa la uzito wa mwili.
Kwenye orodha ya mambo hayo hauwezi kusahau kutaja mchango wa lishe ambayo huchangia kiasi kikubwa cha nishati kuliko ile inayo hutajika na mwili.
Tafiti nyingi zinalitaja parachichi kama tunda zuri linalofaa kwenye kusaidia mwili utunze uzito sahihi unaofaa. (9,10,11)
Aidha, imethibitika kuwa huwa na kemikali na virutubisho vyenye uwezo wa kuchoma mafuta mabaya yaliyo jikusanya tumboni pamoja na kuzuia kutokea kwa kiribatumbo.
10. Magonjwa Sugu
Parachichi ni nyumba ya virutubisho vingi.
Ni silaha muhimu kwenye kupambana na magonjwa yasiyo ambukiza kama kisukari, shinikizo la juu la damu pamoja na magonjwa ya mfumo wa moyo na damu.
Muhtasari
Wengi huwaza, mafuta yanayopatikana kwenye parachichi ni mazuri kwa afya?
Je, hayaongezo uzito wa mwili na kusababisha magonjwa?
Mafuta haya ni mazuri.
Tumia tunda hili kila unapopata nafasi. Litakufaa kwa afya yako