Punyeto ni tendo analofanya mtu, likihusisha kujisisimua sehemu zake za siri ili afikie utimilifu wa kihisia.
Tofauti na jinsi ambavyo watu wengi hudhani, tendo hili halijali jinsia ya mtu.
Katika utafiti mmoja uliofanyika nchini Marekani ukihusisha vijana wa kike na kiume wenye umri kati ya miaka 14-17, asilimia 73.8 ya wavulana wote waliofanyiwa utafiti walikiri kupiga punyeto mara kadhaa, huku asilimia 48.1 ya wasichana wote waliofanyiwa utafiti wakikiri pia kufanya tendo hili.
Kwa watu wazima wenye umri kati ya miaka 57-64, asilimia 63 ya wanaume hupiga punyeto, huku wanawake wakiwa ni asilimia 32.
Wanaume hupiga punyeto, wanawake nao pia hupiga.
Uzushi
Starehe hii inayofanywa kwa siri kubwa, isiyohitaji gharama wala mwenza imekuwa inasigiziwa mambo mengi ambayo hayana mashiko kisayansi.
Sayansi sio siasa. Ikiwa hauna utafiti wa kutosha, kitu pekee unacho shauriwa kufanya ni kufunga mdomo wako.
Kwa maana hiyo, tunapenda kubainisha kuwa mambo haya sio ya kweli kuhusu punyeto;
- Haipunguzi nguvu za kiume
- Haisababishi upara
- Haifanyi uume upungue ukubwa
- Haileti upofu
- Haisababishi kukauka au kusinyaa kwa ngozi
- Haisababishi saratani ya tezi dume uzeeni
Uvumi mkubwa uliopo mtaani kuhusu mambo haya hukolezwa na utashi binafsi, usio na uthibitisho wowote wa kisayansi.
Ni vipi tendo hili lisababishe ugumba, kupungua kwa nguvu za kiume au kudumaa kwa uume wakati mifumo ya mwili, vichocheo vya kusisimua mwili, pamoja na vile vinavyotolewa baada ya kufika kileleni ni vilevile ambavyo mwili hutoa wakati wa tendo halisi la ndoa?
Bila shaka, kama punyeto ingekuwa inasababisha mambo haya, tendo halisi la ndoa lingekuwa linafanya hivyo pia.
Madhara Yake
Kwa watu waliosoma fizikia watakuwa wanakumbuka kanuni ya tatu ya mwendo, iliyotungwa na Isaac Newton. Ni kuwa, kila jambo linalofanyika huwa na nguvu mbili zinazopingana.
Haya ndio madhara ya punyeto;
1. Majuto
Dhana hii imejikita kwenye msingi wa dhamiri zetu, juu ya uwepo wa mambo mema na mabaya.
Kiimani, jambo hili ni baya sana. Kwa kuwa sisi sio makasisi, mitume au manabii, hatutaweza kuingia huko kwa undani.
Baada ya kushiriki tendo hili, mara nyingi mhusika hujiona ni mkosefu sana, akitawaliwa na hisia za kujiona mkosefu.
Hukosa amani, na mara nyingi dhamiri yake humshitaki.
2. Uraibu
Umewahi kumsikiliza mvutaji wa sigara akielezea ugumu anaopitia katika kuacha kuvuta?
Punyeto ni zaidi ya sigara. Hutengeneza uraibu mkubwa, pia humfanya mhusika awe na utegemezi.
Kwa kuwa mara nyingi tendo hili huhusisha matumizi ya picha, sauti pamoja na video za ponografia, uraibu huwa haukwepeki.
Mawazo ya kujiambia “nifanye leo tu” “leo tu ndio mwisho” “nipige ya mwisho” “mara moja tu sirudii” hujirudia mara kwa mara.
Ni ngumu kuacha ukizoea.
3. Kutokuridhika
Ni rahisi kuridhika na tendo moja halisi la ndoa kuliko kupiga punyeto tano.
Wapiga punyeto huwa hawaridhiki haraka.
Furaha yao hudumu muda mfupi hivyo huhitaji kufanya mara kwa mara ili kutimiza mahitaji yao.
4. Kuvimba na Kuchubuka
Kutokana na kufanya jambo hili mara kwa mara ndani ya muda mfupi, hasa kwa kutumia vitu ambavyo mara nyingi huwa sio vilaini ukilinganisha na uke, nafasi ya kuvimba kwa kichwa cha uume ni kubwa.
Uvimbe wa aina hii huisha wenyewe tu baada ya siku chache.
Wanawake pia huwa kwenye hatari ya kupatwa na michubuko ukeni hasa pale wanapotumia zana za ngono kama vile vidole na dildo.
5. Msisimko
Watu wengi wanaopiga punyeto hutumia nguvu kubwa kwenye kusugua uke kwa kutumia vidole, vibrators au vifaa vingine.
Vivyo hivyo kwa wanaume, ni lazima kichwa cha uume kisisimliwe kwa kutumia nguvu kubwa ili kiweze kuleta mhemko sahihi wa kihisia.
Matendo haya hupunguza msisimko wa via vya uzazi, hutengeneza usugu.
Watu hawa wanaweza kushiriki tendo la ndoa pasipo kuridhika kwa kuwa furaha wanayopata hapa huwa hailingani na ile wapatayo kwa kujisisimua wao wenyewe.
6. Kujitenga na Jamii
Unakumbuka tulisema kuhusu uraibu pamoja na changamoto za kisaikolojia?
Punyeto hufanya mhusika asione umuhimu wa kuwa na mahusiano na binadamu mwenzake kama ambavyo tamaduni zetu zimetukuza na kutufundisha.
7. Uchovu
Watu hawa hutumia nguvu nyingi sana kubadili mawazo kuwa uhalisia.
Jambo hili huwafanya wachoke sana maana huupa ubongo kazi ya ziada kwenye kufanya tafsiri ya starehe yao.
Faida Zake
Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni.
Tafiti nyingi zinabainisha faida za punyeto kwenye kuboresha afya ya uzazi, kuondoa msongo wa mawazo, wasiwasi, kupunguza maumivu ya mwili pamoja na kuboresha usingizi.
Ni tendo zuri kwa watu waliotengwa na jamii, pia ni njia ya kujikinga na ujauzito usio tarajiwa pamoja na magonjwa ya zinaa.
Hata hivyo, ushiriki wa tendo hili kwa kutumia ponografia unaweza kuleta athari mbaya kwa afya, ikiwemo kuathirika kisaikolojia pamoja na kushindwa kushiriki kikamilifu tendo la ndoa.
Muhtasari
Tendo hili linaweza kuwa kero kwa mhusika hasa katika safari nzima ya kuliacha.
Zungumza na daktari wako, mtaalamu wa saikolojia, kiongozi wako wa dini au mtu mwingine yeyote unaye muamini sana ili akusaidie ushauri.
Dhana ya ubaya wa jambo hili huwa na mizizi ya kiimani. Hoja yetu sisi imejikita kwenye misingi ya sayansi.
Ufanye au usifanye? Ni wewe, Mungu wako na imani yako.