Ni uvimbe unaotokea kwenye ini ambao huambatana na utengenezwaji wa makovu.
Tatizo hili linaweza kuwa la muda mfupi ikiwa litadumu kwa kipindi kisicho zidi miezi 6, lakini linaweza kuwa sugu ikiwa litaendelea kuwepo kwa zaidi ya miezi 6.
Walau takriban watu milioni 500 duniani ni waathirika wa ugonjwa huu.
Visababishi
Virusi maalumu vya homa ya ini vinavyo patikana kwenye aina kuu 5 tofauti ndivyo huhusika kwa kiasi kikubwa katika kusababisha tatizo hili.
Huwekwa kwenye makundi A, B, C, D na E.
Pombe, vimelea vingine vya magonjwa, madawa, pamoja na aina mbalimbali za sumu ni visababishi vingine vya tatizo hili.
Aina za Ugonjwa
Kuna aina kuu 5 za ugonjwa wa homa ya Ini ambazo ni homa ya ini aina A, homa ya ini aina B, homa ya ini aina C, homa ya ini aina D pamoja na homa ya ini aina E.
Aina A
Husababishwa na vimelea vya virusi wa homa ya ini aina A (HAV).
Ni ugonjwa wa muda mfupi, huwa haudumu kwa muda mrefu.
Mtu anaweza kupata ugonjwa huu kwa kunywa maji, au kula vyakula vilivyo changanyikana na kinyesi chenye virusi wa ugonjwa huu. Hupatikana zaidi kwenye maeneo yenye mazingira machafu.
Aina B
Husababishwa na vimelea vya virusi wa homa ya ini aina B (HBV).
Ni ugonjwa ambao mara nyingi hudumu kwa muda mrefu.
Mtu anaweza kupata ugonjwa huu kupitia damu pamoja na mazao yake.
Mazingira na hali hatarishi zinazoweza kusababisha maambukizi ya ugonjwa huu ni kupokea damu ya mtu mwenye ugonjwa, wafanyakazi wa afya kwa kuwa hukutana na damu mara kwa mara, kushirikiana vitu vyenye ncha kali, kufanya usafishaji wa damu kupitia huduma ya figo za nje, maarufu kama dialysis, mama kwa mtoto wakati wa kujifungua, wakati wa ngono ya aina yoyote ile kutoka kwenye majimaji ya uke, au shahawa za mwanaume pamoja na kwenye mazingira yaliyo na udhibiti mkubwa hasa magerezani na vituo vya wagonjwa wa akili.
Aina C
Husababishwa na vimelea vya virusi wa homa ya ini aina C (HCV). Ni ugonjwa ambao mara nyingi hudumu kwa muda mrefu.
Uambukizwaji wa aina hii ya homa ya ini hufanana na ule wa homa ya ini aina B.
Aina D
Ni aina ya ugonjwa wa homa ya ini ambao hutokea kwa watu wenye homa ya ini aina B.
Husababishwa na vimelea vya virusi wa homa ya ini aina D (HDV).
Hii inamaanisha kuwa, mtu asipokuwa na homa ya ini aina B hawezi kupata homa ya ini aina D. Huambukizwa kwa njia ya damu na mazao yake yaliyobeba virusi wa homa ya ini aina B.
Aina E
Husababishwa na vimelea vya virusi wa homa ya ini aina E (HEV).
Ni ugonjwa ambao mara nyingi hudumu kwa muda mfupi.
Huambukizwa kwa kunywa maji au vyakula vilivyochanganyikana na masalia ya vinyesi vya watu walio na ugonjwa huu.
Dalili
Kuna aina kuu 5 za ugonjwa wa homa ya ini kama tulivyoziona. Pamoja na utofauti hizi, ugonjwa huu mara nyingi huwa na dalili zinazofanana.
Dalili hizi huwa hazionekani mapema, hutokea baada ya kuharibika kwa ini. Miongoni mwa dalili hizo ni uchovu pasipo sababu, kujisaidia mkojo mweusi, maumivu chini ya tumbo, kupungua sana kwa uzito wa mwili, umanjano wa macho na ngozi, kukosa hamu ya kula pamoja na shinikizo la juu la damu kwenye ini.
Dalili hizi mara nyingi huonekana kwa watu wenye homa ya ini aina B na C kwa kuwa aina hizi hudumu kwa muda mrefu, pia huwa na athari kubwa kwa afya kuliko aina zingine.
Tiba
Homa ya ini aina A huwa haihitaji matibabu. Hudumu kwa muda mfupi na huondoka yenyewe.
Hata hivyo, mgonjwa hushauriwa aache kunywa pombe, aongeze muda wa kupumzika, anywe maji mengi pamoja na kumeza dawa za kuondoa dalili zitakazokuwa zinamsumbua ambazo mhuudumu wa afya atampatia.
Homa ya ini aina B na C hutibiwa kwa kutumia dawa za virusi. Ikiwa hali itakuwa mbaya zaidi, upandikizaji wa ini unaweza kufaa zaidi.
Homa ya ini aina D hutibiwa kwa kutumia dawa za interferon alpha.
Hata hivyo, mgonjwa hushauriwa aache kunywa pombe, aongeze muda wa kupumzika, anywe maji mengi pamoja na kumeza dawa za kuondoa dalili zitakazokuwa zinamsumbua ambazo mhuudumu wa afya atampatia.
Homa ya ini aina E mara huwa haina matibabu sahihi, kwa kuwa hudumu kwa muda mfupi hupona yenyewe. Kula vizuri, kupata muda wa kupumzika, kupunguza unywaji wa pombe pamoja na kutumia dawa za ribavirin inaweza kusaidia.
Ni muhimu kufuata masharti sahihi ya umezaji wa dawa pamoja na kuanza kwa wakati ili kusaidia uponaji wa haraka.
Kinga
Baadhi ya aina za ugonjwa wa homa ya ini husababishwa na uchafu ulipo kwenye maji na vyakula unaotokana na mabaki ya vinyesi.
Kutunza usafi ni njia kuu ya kujikinga na ugonjwa huu.
Ukiondoa aina C, mtu anaweza kupata chanjo za kuzuia aina A na B za ugonjwa wa homa ya ini. Kwa sasa, nchi ya China imeanza pia kutoa chanjo ya aina E.
Inashauriwa kupunguza matumizi ya pombe, kuacha kushiriki ngono zembe pamoja na kushirikiana vitu vyenye ncha kali ambavyo hurahisisha usambazwaji wa baadhi ya virusi vya ugonjwa huu.
Muhtasari
Ugonjwa wa homa ya ini hasa aina B na C usipotibiwa vizuri unaweza kusababisha saratani ya ini, kujaa kwa maji kwenye sehemu ya chini ya tumbo, kuharibika kwa figo pamoja na kifo.
Kwa wagonjwa, inashauriwa kuwa makini sana na matumizi ya pombe, supplements pamoja na baadhi ya dawa ambao huongeza ukubwa wa tatizo.
Ugonjwa wa homa ya ini hasa aina B huwa ni hatari sana kwa afya. Huwa na uwezo mara 50-100 wa kushambulia na kuambukiza kuzidi VVU.
Ni muhimu kupata tiba sahihi kwa wakati sahihi, pamoja na kufuata ushauri wa daktari na mfamasia katika uchaguzi wa vyakula na dawa unazotumia kila siku.