Ni uvimbe wa mishipa ya damu inayopatokana kwenye sehemu ya chini ya utumbo mpana pamoja na sehemu ya haja kubwa.
Uvimbe huu mara nyingi husababisha maumivu makali na kuvuja kwa damu. Bawasiri inaweza kubakia ndani, au ikachomoza nje kwenye sehemu ya haja kubwa.
Hali hii husababisha ugumu katika kujisaidia kutokana na aina ya maumivu ambayo hutengenezwa wakati huo.
Visababishi
Mishipa ya damu inayopatikana kwenye sehemu ya haja kubwa huwa na uwezo wa kutanuka na kuvimba pale inapo kabiliwa na mgandamizo mkubwa kutoka sehemu ya chini ya utumbo mkubwa.
Mgandamizo huu unaweza kusababishwa na ujauzito, kubeba mizigo mizito, kutumia nguvu kubwa wakati wa kujisaidia haja kubwa, uwepo wa tatizo la choo kigumu au kuhara kwa muda mrefu, kuwa na uzito mkubwa, kushiriki ngono kinyume cha maumbile pamoja na kutokula vyakula vyenye maji na nyuzi lishe za kutosha.
Dalili
Bawasiri inaweza isioneshe dalili zozote lakini miongoni mwake ni uvimbe wa rangi ya zambarau kwenye sehemu ya haja kubwa, maumivu makali wakati wa kujisaidia haja kubwa, kujisaidia choo chenye damu, au kutokwa na damu baada ya kujisaidia haja kubwa pamoja na uwepo wa vidonda kwenye tundu la haja kubwa.
Kuna namna nyingi za kufanya uchunguzi wa tatizo hili.
Mtaalamu wa afya anaweza kutumia vifaa maalumu, au anaweza kuchunguza kwa kutazama sehemu husika.
Tiba
Unaweza kupunguza maumivu ya bawasiri kwa kujikanda kwa maji yenye joto la kiasi, hasa ikiwa bawasiri hii ipo nje ya tundu la haja kubwa.
Matumizi ya dawa za kupunguza maumivu hushauriwa pia wakati huu.
Kunywa maji mengi pamoja na kutumia dawa na virutubisho vinavyorahisisha choo husaidia sana katika kuikabili hali hii.
Mboga za majani huwa na nyuzi lishe za kutosha, pia matunda kama parachichi, ndizi mbivu na papai yanaweza kulainisha choo hivyo kupunguza adha ya maumivu.
Matibabu ya kukaa kwenye maji ya moto yaliyo kwenye chombo maalumu maarufu zaidi kama sitz bath hutumika pia. Inashauriwa mgonjwa asizidishe dakika 10 ili kuepusha kuunguza eneo hilo.
Ikiwa njia zote zitashindikana, upasuaji ndiyo suluhisho la mwisho. Hata hivyo, njia hii inapaswa kufanyika hospitalini, mgonjwa hashauriwi kujikata mwenyewe akiwa nyumbani.
Kinga
Inashauriwa kunywa maji ya kutosha kila siku, kuongeza ulaji wa matunda na mboga za majani pia kujihusisha na mazoezi mepesi ambavyo kwa ujumla huupunguzia mwili nafasi ya kupatwa na changamoto ya choo kigumu.
Muhtasari
Katika mazingira machache, tatizo la bawasiri linaweza kusababisha mhusika apoteze damu nyingi pamoja na kupata maambukizi mwilini mwake.
Ni muhimu sana kupata ushauri wa kitabibu pale hali hii inapotokea ili kuepusha madhara makubwa zaidi yanayoweza kujitokeza.