Kuna mambo mengi hutokea wakati wa ujauzito ambayo wanawake wengi huwa hawajawahi kuyasikia kabla.
Matumizi ya foliki asidi yanaweza kuwa ni kitu kipya, ambacho wengi huanza kutumia pasipo kufahamu kazi yake.
Foliki asidi na folate ni aina za vitamimi B 9, ambazo pamoja na kazi zingine, huusaidia mwili kwenye kutengeneza vinasaba, chembechembe za damu pamoja na kuboresha afya ya mama mjamzito, pamoja na mtoto aliyeko tumboni.
Mwongozo
Inashauriwa kuwa, kila mwanamke aliye kwenye umri wa kushika ujauzito atumie walau micrograms 400 za foliki asidi kila siku, pamoja na kuongeza ulaji wa vyakula na virutubisho vyenye vitamini hii.
Matumizi ya foliki asidi husaidia kumkinga mtoto aliyeko tumboni ili asipatwe na matatizo kwenye utengenezwaji wa uti wa mgongo na ubongo, hasa kwa kuzaliwa akiwa na mgongo wazi pamoja na kichwa kikubwa chenye ubongo usio kamili, au chenye fuvu ambalo halijatengenezwa vizuri.
Muda Sahihi
Ni muhimu kama mwanamke ataanza kutumia foliki asidi mapema, walau miezi 3 kabla hajapata ujauzito ili kuuandaa mwili wake vizuri.
Hii ni kwa sababu changamoto katika utengenezwaji wa viungo vya mtoto hutokea mapema sana, kabla hata mwanamke hajagundua kuwa ni mjamzito.
Kwa kuwa mwanamke mjamzito hukabiliwa pia na changamoto kubwa ya upungufu wa damu, foliki asidi mara nyingi huunganishwa pamoja na madini ya chuma (FEFO) ili kufanya kazi kwa pamoja.
Kwa mwanamke anayetumia FEFO, yaani muunganiko wa madini ya chuma na foliki asidi hana haja ya kunywa tena foliki asidi maana huipata moja kwa moja humo.
Pamoja na umuhimu wa virutubisho hivi, tafiti zinaonesha kuwa wanawake wengi hawavitumii kutokana na sababu mbalimbali zikiwepo za kimazingira, uwepo wa magonjwa mengine pamoja na ukosefu wa elimu ya kutosha.
Muhtasari
Mboga za majani hasa spinachi, broccoli, maharage, mayai, vyakula jamii ya karanga na parachichi ni baadhi ya vyakula vyenye kiasi kikubwa cha foliki asidi.
Unaweza pia kuipata kwa kununua dawa na virutubisho vyenye vitamini hii.