Mwanamke Kujifungua kwenye Maji

2 Min Read

Kuna njia nyingi zinazoweza kutumika katika kufanikisha zoezi la kujifungua salama kwa mwanamke.

Mojawapo ya njia hizo ni kujifungulia kwenye chombo kilichojazwa maji.

Katika mazingira ya kawaida, maji haya hupaswa kuwa yametulia, pia yasiwe mengi sana.

American College of Obstetricians and Gynecologists (ACOG), hawashauri kufanyika kwa njia hii kwa kuwa bado hakuna tafiti nyingi zinazoonesha wingi wa faida zake kuliko madhara.

Hata hivyo, taasisi hii inatambua uwepo wa faida ya kupunguza muda wa uchungu wa kuzaa kwenye hatua ya kwanza ya uchungu huo.

Njia hii hurahisisha kufunguka kwa mlango wa kizazi pamoja na kupunguza maumivu kwa kiasi kidogo.

Pamoja na uwepo wa faida hizi, changamoto ya aina hii ya kujifungua ni kuongezeka kwa hatari ya mtoto kuambukizwa magonjwa hasa yale yanayosababishwa na bakteria kutokana na kuvuta matone ya maji yaliyo changanyikana na uchafu, nimonia kali, kuharibika kwa kitovu, ugumu katika kudhibiti joto la mtoto, kifafa pamoja na kutokea kwa changamoto kwenye mfumo wa upumuaji.

Aina hii ya kujifungua huwa haishauriwi kabisa kwa wanawake ambao ujauzito wao haujafikisha wiki 37 pamoja na wale waliojifungua kwa upasuaji kwenye ujauzito wa awali.

Hata hivyo, wanawake walio na maambukizi kwenye damu (au ngozi), wenye joto zaidi ya digrii 38 za sentigredi, wenye damu nyingi zinazovuja ukeni, kama mapigo ya moyo ya mtoto hayapo huru, wenye historia ya kuzaa mtoto aliyetanguliza mabega pamoja na ujauzito wenye mtoto zaidi ya mmoja (mapacha) hawashauriwi kujifungua kwa njia hii.

Ni muhimu kwanza kufahamu hatua zote za kufuata kabla haujaamua kwenda na njia hii kwenye kujifungua.

    Uelewa wa kina pamoja na maandalizi mazuri huhitajika ili kuifanikisha. 

    Share This Article