Papai: Virutubisho, Faida na Tahadhari kwa Afya

7 Min Read

Hadithi mbalimbali za kale zinaeleza asili ya mapapai kuwa ni nchi ya Mexico.

Tunda hili lililobeba hadithi mbalimbali za kusisimua hupatikana karibia kila sehemu ya dunia.

Kwa lugha ya kisayansi, papai huitwa Carica papaya.

Virutubisho

Papai ni chanzo bora sana cha Vitamini C.

Papai moja lenye ukubwa wa wastani wa 150 g huwa makadirio ya asilimia 224 ya kiasi cha kawaida cha Vitamini C inayohitajika kila siku.

Mgawanyiko mwingine wa virutubisho kwenye kila 150g za tunda hili ni Protini 2g, nyuzi lishe 4 g na wanga 15g.

Folate, vitamini A, magnesium, copper, pathothenic acid, beta carotene, lutein, calcium, potassium, lycopene pamoja na vitamini E ni miongoni mwa virutubisho vinavyopatikana kwenye papai.

Kutokana na uwepo wa virutubisho vingi, papai hutoa faida kubwa kwenye kujenga na kuboresha afya ya binadamu.

Papai hufanya kazi zifuatazo kwenye mwili wa binadamu;

1. Kinga

Vitamini C haiishii kwenye maembe, limao na machungwa pekee. Huwepo pia kwenye papai.

Ni muhimu katika kujenga kinga imara ya mwili, kuwahisha uponaji wa vidonda pamoja na kuhakikisha kuwa mwili unakuwa na afya nzuri kila wakati. (1,2)

Tumia papai upate faida hii.

2. Sumu

Katika harakati za Maisha ya kila siku, binadamu hutumia sumu kutoka kwenye vyakula, vinywaji pamoja na hewa kwa kujua au kutokujua. Sumu hizi siyo rafiki kwa mwili.

Papai huwa na viondoa sumu vingi ambavyo huusaidia mwili katika kuviondoa hivyo kuepusha athari mbaya zinazoweza kutokea kwa afya. (3,4,5)

Baadhi ya athari za uwepo wa sumu nyingi mwilini ni kuugua magonjwa sugu hasa saratani, pamoja na kuzeeka haraka kwa ngozi.

3. Saratani

Kwa mujibu wa National Cancer Institute, mwili wa binadamu hupokea kemikali na sumu nyingi zinazoweza kusababisha aina mbalimbali za saratani.

Uwepo wa lycopene, lutein, beta carotena na zeaxanthin kwenye papai huusaidia mwili katika kupambana na saratani, pamoja na kutoa kinga ili saratani husika zisitokee. (6,7)

Tafiti kadhaa za afya zinasisitiza kuwa papai inaweza kusaidia katika kupambana na saratani ya tezi dume, damu pamoja na mapafu.

4. Uvimbe

Baadhi ya kemikali zilizopo kwenye papai huusaidia mwili katika kupambana na aina mbalimbali za uvimbe. (8)

Virutubisho vya Choline vinavyopatikana kwenye tunda hili huusaidia mwili katika kutengeneza usingizi, mijongeo ya misuli, kujifunza pamoja na kutunza kumbukumbu.

Ni silaha muhimu katika kudhibiti aina mbalimbali za uvimbe mwilini.

5. Mfumo wa Chakula

Kama unasumbuliwa na changamoto ya kujisaidia choo kigumu hauna sababu ya kuwaza mara mbili juu ya chaguo sahihi la kukufanya uondokane na hali hii.

Papai huwa na vimeng’enya vinavyoitwa papain ambavyo husaidia umeng’enywaji wa chakula pia hutumika kwenye viwanda vya kusindika nyama katika kuongeza ladha.

Kiasi kikubwa cha nyuzi lishe pamoja na maji yanayopatikana kwenye papai  pamoja na vimeng’enya vya papain vyote kwa pamoja hufanya kazi ya kuboresha mfumo wa chakula pamoja na kusaidia kuondoa tatizo la choo kigumu. (9)

Hauna haja ya kukaa muda mrefu chooni ukiugulia maumivu makali ya kutoa haja kubwa, jawabu ni tunda hili.

6. Kisukari

Papai ni miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kidogo cha sukari.

Kwa kuwa watu wenye kisukari hushauriwa kutokutumia vyakula vyenye uwezo wa kutengeneza sukari nyingi, papai linaweza kuwa chaguo sahihi kwao.

Sababu nyingine inayofanya papai liwe chaguo zuri kwa watu wenye kisukari ni uwepo wa kiasi kikubwa cha nyuzi lishe. (10,11,12)

Hii inatoa ishara kuwa haiwezi kuufanya mwili utengeneze na kutunza sukari nyingi hivyo ni salama kwao.

7. Moyo

Papai huwa na foliki asidi ambayo hutumika kuzipunguzia sumu amino acid zinazoitwa homocysteine na kuzifanya siziwe na athari kubwa kwa mwili.

Kiasi kikubwa cha homocysteine, amino acids ambazo hupatikana zaidi kwenye nyama huwa ni hatari sana kwa afya ya moyo. (13)

Kwa maana hiyo, papai hufaa kwenye kulinda moyo kwa kuzuia usiugue magonjwa mbalimbali yanayoweza kukabili kiungo hiki.

8. Macho

Hii hutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha viondoa sumu pamoja na vitamini A.

Huwa pia na kampaundi mbili zinazoitwa lutein na zeaxanthin.

Vyote hivi hutakiwa kwenye kuimarisha afya ya macho, kuongeza uoni na kuzuia upofu. Kula papai uboreshe afya ya macho yako.

9. Pumu

Pumu ni ugonjwa unaosumbua watu wengi.

Ni ugonjwa ambao husababisha kuvimba, kupungua ukubwa kwa njia ya hewa pamoja na kufanya ute mwingi uzalishwe humo. Hali hii hufanya mhusika awe na wakati mgumu kwenye kupumua.

Tafiti kadhaa zinathibitisha kuwa papai husaidia kwenye kupambana na ugonjwa huu.

10. Vidonda

Baadhi ya viwanda hutumia sehemu ya viambato na kemikali za papai kutengeneza vipodozi na dawa zinazotumika kwenye kutibu vidonda na kuzuia maambukizi.

Vimeng’enya vya chymopapain na papain ambavyo hupatikana kwenye sehemu kubwa ya utomvu wa papai hufaa kwa kazi hii. (14,15)

Unaweza kutumia kama njia ya kienyeji ya kutibu vidonda vidogo.

11. Mifupa

Huongeza uwezo wa mifupa kwenye kuzalisha uboho (uroto) pamoja na kuongeza ubora wa afya ya mifupa.

Aidha, huboresha mfumo wa uzalishwaji wa damu mwilini.

Unaipenda mifupa yako? Chukua hatua.

Matumizi

Linaweza kutumika kwa kutafuna au juisi au salad.

Kwa watu wanaotumia kama juisi, ni muhimu kutolisaga sana ili kutunza ubora na wingi wa virutubisho vyake.

Tahadhari

Papai bichi huwa na kiasi kikubwa cha nta inayoitwa papain.

Ulaji wa mapapai mengi hasa mabichi unaweza kusababisha vidonda kooni.

Nta hii yenye vimeng’enya vya papain inaweza pia kusisimua misuli ya mji wa uzazi hivyo kusababisha uchungu wa mapema. (16)

Jambo hili linaweza kutokea hasa kwa wanawake wenye mzio na mapapai hivyo ni muhimu sana kuepuka ulaji wa mapapai mabichi ambayo ndiyo hubeba kiasi kikubwa cha papain.

Hata hivyo, papai ni tunda lenye virutubisho vingi.

Siyo mbaya kama mama mjamzito atatumia papai lililoiva vizuri kwa ajili ya kujipatia virutubisho wakati wote wa ujauzito. Hili halina madhara hasi kwa afya.

Share This Article