Faida na Hasara za Chuchu Bandia kwa Mtoto

3 Min Read

Kabla hujaamua kumpa mwanao chuchu bandia ni vema ukazijua faida na hasara zake.

Chuchu bandia zimekuwa zinatumika sana katika kurahisisha uleaji wa watoto, hasa wale wakorofi.

Huwasaidia wazazi kupata uhuru kidogo wa kufanya kazi zingine kama kupika, usafi wa nyumba au hata kukamilisha biashara na kazi zao zingine.

Faida

Chuchu bandia huwa na faida nyingi. Miongoni mwa faida hizo ni;

  • Husaidia kupunguza vifo vya ghafla vya watoto hasa wawapo usingizini.
  • Hutuliza watoto wakorofi.
  • Humbembeleza mtoto na kumsaidia katika kupata usingizi haraka.
  • Huwapunguzia nafasi ya kusumbuliwa na mabadiliko ya hali ya hewa wawapo angani katika nyakati ambazo usafiri wa ndege unatumika.

Madhara

Upande wa pili wa shilingi unaohusisha matumizi ya chuchu bandia unaweza usiwe mzuri sana.

Haya ndiyo madhara yake;

  1. Kuongeza uwezekano wa mtoto kupata maambukizi kwenye sehemu ya kati ya sikio ikiwa chuchu hiyo haisafishwi au kutunzwa kwenye mazingira safi
  2. Kwa baadhi ya watoto husababisha kuota kwa meno yaliyopishana.
  3. Husababisha mtoto akatae kunyonya maziwa ya mama. Hii hutokea kwa watoto wanaoanzishiwa matumizi ya chuchu bandia kabla hata hawajafikisha umri wa mwezi mmoja.
  4. Huleta matatizo katika kutenganisha chuchu halisi ya mama yake na ile ya bandia. Inaweza kumsababishia apate upungufu wa virutubisho muhimu ambayo hupatikana kwenye maziwa ya mama pekee
  5. Husababisha kujaa kwa gesi tumboni kwa watoto wanaonyonya haraka. (2,3,4)

Faida za chuchu bandia huanza kupungua kadri mtoto anavyozidi kuwa mkubwa.

Baadhi ya watoto huacha kutumia chuchu hizi baada ya kufikisha miaka 2, wengine huendelea kusubiri hadi miaka 4 ndipo waache kabisa kuzitumia.

Muhimu

Ni muhimu kukumbuka mambo yafuatayo wakati wa kumpatia mtoto chuchu bandia

  • Usimlazimishe aitumie hasa kwenye nyakati ambazo hataki
  • Usiweke kitu chochote kwenye chuchu bandia kama sehemu ya kumvutia mtoto aitumie (mfano asali, sukari n.k)
  • Nunua chuchu bandia yenye ukubwa unaoendana na kinywa cha mtoto
  • Mtoto anapokuwa analia, tumia njia zingine kwanza kumbembeleza kama nyimbo, massage pamoja na kumpiga piga mgongoni. Chuchu bandia iwe ni chaguo la mwisho baada ya kushindwa kwa njia hizi
  • Hakikisha kwanza kama mtoto hana njaa kabla hujampatia chuchu bandia

Kwa kuwa umefahamu faida na hasara za chuchu bandia, tunaamini kuwa sasa utakuwa tayari kufanya maamuzi sahihi katika kuamua matumizi yake kwa mwanao.

Ikiwa utaamua kutumia, hakikisha unafuata ushauri wa kiusalama hasa katika kutunza usafi pamoja na kufuata masharti sahihi ya umri wa matumizi kwa mtoto.

Share This Article