Uzito mkubwa husababishwa na kukosekana kwa uwiano sahihi kati ya nishati inayoingizwa mwilini kupitia chakula na vinywaji, na nishati inayotumiwa na mwili katika kujiendesha.
Katika hali ya kawaida, wingi wa nishati inayoingizwa mwilini hupaswa kufanana na ile inayotumika.
Kukosekana kwa uwiano huu husababishwa na ulaji wa vyakula vyenye nishati nyingi iliyobebwa kwenye mafuta na sukari, pamoja na kubadilika sana kwa mitindo ya maisha ya binadamu inayofanya kupungua kwa utimamu wa mwili kupitia kazi, mazoezi na aina ya usafiri.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kumekuwa na ongezeko la uwepo wa watu wenye uzito mkubwa mara 3 zaidi kwa kipindi cha miongo minne sasa, huku mwaka 2016 pekee idadi ya watu wazima wenye changamoto hii duniani wakiwa ni bilioni 1.9.
Uzito mkubwa (na kitambi) huathiri afya ya binadamu kwa kiasi kikubwa.
Baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na uwepo wa hali hii ni;
1. Kisukari
Ugonjwa wa kisukari hutokea baada ya kiasi cha sukari kuwa nyingi kwenye damu kuzidi kiwango kinachotakiwa.
Katika kila wagonjwa 10 wa kisukari, 8 kati yao huwa na uzito mkubwa.
Kupunguza asilimia 5-7 ya uzito huo wa ziada pamoja na kushiriki mazoezi mara kwa mara hupunguza hatari ya kupata ugonjwa huu wa kisukari.
2. Presha
Watu wenye uzito mkubwa huwa na hatari kubwa ya kuugua ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, maarufu zaidi kama presha.
Kutokana na kuongezeka kwa kiasi cha mafuta mwilini, mishipa ya damu hupungua ukubwa wake, jambo ambalo hufanya msukumo wa damu uwe mkubwa kuliko kawaida.
3. Moyo
Moyo ni kiungo kinacho athirika sana inapotokea uzito wa mwili umekuwa mkubwa kuliko kiwango kinachotakiwa.
Nguvu yake ya kusukuma damu huwa ni lazima iongezeke zaidi.
Shambulio la moyo, kupanuka kwa moyo, maumivu ya kifua, kubadilika kwa utaratibu wa kawaida wa mapigo ya moyo pamoja na kifo cha ghafla ni mojawapo ya mambo yanayoweza kumpata mtu mwenye uzito mkubwa.
4. Uzazi
Uwiano sawa wa vichocheo vya mwili huwa ni kiini cha uhai na ubora wa afya ya uzazi.
Wanawake wenye uzito mkubwa huwa na kiasi kikubwa cha vichocheo vya leptin mwilini.
Wingi usio wa kawaida wa vichocheo hivi huharibu uwiano wa vichocheo mwilini hivyo kudumaza ubora wa afya ya uzazi na kusababisha ugumba.
Kwa wanaume, uzito mkubwa huhusishwa na kupungua kwa vichocheo vya kiume, mbegu za kiume dhaifu pamoja na kupungua kwa uwezo wa kurutubisha yai la mwanamke.
Aina hii ya uzito ni kikwazo kikubwa kwenye ubora wa afya ya uzazi.
5. Ujauzito
Uzito mkubwa huchangia kwa nafasi kubwa sana kutokea kwa changamoto nyingi wakati wa ujauzito pamoja na kujifungua.
Huhusishwa moja kwa moja na kisukari cha ujauzito, kifafa cha mimba pamoja na kuongeza nafasi ya kujifungua kwa upasuaji.
6. Athari Zingine
Uzito mkubwa huathiri karibia kila sehemu ya mwili.
Mfano, ugonjwa wa kiharusi huwapata sana watu wenye uzito mkubwa, pia baadhi ya saratani, ugonjwa wa ini pamoja na maungio ya mwili huwa na nafasi kubwa ya kutokea kwa watu wenye uzito mkubwa kuliko wale wenye uzito wa kawaida.
Kama unaishi na changamoto hii unaweza kuitibu (au kuidhibiti) kwa kutumia mbinu nne ambazo ni mlo, mazoezi, kubadili mtindo wa maisha pamoja na kutumia dawa.
Ushauri
Pamoja na faida zake kiafya, zoezi la kupunguza uzito linapaswa lifanyike kwa kufuata miongozo sahihi.
Kupunguza uzito mkubwa sana ndani ya muda mfupi huongeza nafasi ya kutengenezwa kwa mawe kwenye mfuko wa nyongo, kupoteza kiasi kikubwa cha maji, kuvurugika kwa uwiano wa madini na chumvi mwilini, kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi, kudhoofika kwa misuli ya mwili, uchovu mkubwa, kizunguzungu pamoja na maumivu makali ya kichwa.
Kupunguza walau paundi 10 (4.5 kg) za uzito wako kwa mwezi ndiyo kiwango sahihi kinacho shauriwa na wataalamu wa afya.