Ni mzizi ulio na faida kubwa sana kwa afya.
Vyanzo vya kihistoria vinataja asili ya mzizi huu kuwa ni Kusini mwa bara la Asia.
Hupatikana kwenye familia kubwa ya Zingiberaceae.
Virutubisho
Kwa mujibu wa USDA, tangawizi ni mzizi ulio na mjumuiko wa nishati, protini, wanga, nyuzilishe, madini chuma, calcium, phosphorus, magnesium, zinc, selenium, vitamini C, B6, B12 na folate.
Tangawizi huwa pia na kemikali hai za kampaundi za phenolic na terpene ambazo mfano wake ni gingerols, shogaols na paradols.
Matumizi
Tangawizi inaweza kutumika kwa namna nyingi sana.
Watu wengi huitumia ikiwa mbichi, kavu, kama unga, juisi, kiungo kwenye vyakula au pia kwa mfumo wa mafuta.
Ni kiambato muhimu sana kwenye uandaaji wa vyakula na virutubisho vingi.
Katika nyakati fulani, tangawizi hutumiwa viwandani kutengeneza bidhaa za urembo hasa mafuta na lotion.
Kutokana na umuhimu wake kwenye maisha ya binadamu, tumekupa faida za mizizi huu wa maajabu kwenye afya ya binadamu.
Faida hizi siyo za kusadikika, zimethibitishwa kwa tafiti za kisayansi.
1. Kiungulia na Kutapika
Tangawizi hutibu kiungulia kwa ufanisi mkubwa.
Watu wenye changamoto ya kutapika wawapo safarini wanaweza kutumia tangawizi muda mchache kabla ya safari, pia wanaweza kuhifadhi kipande kidogo cha kutafuna kila wanapohisi kutapika wakati safari ikiendelea.
Tangawizi husaidia pia kupunguza changamoto ya kutapika pamoja na kuondoa kiungulia kwa mama wajawazito. (1,2,3,4)
Pia, watu wanaopata matibabu ya saratani maafufu zaidi kama chemotherapy wanaweza kutumia mmea huu kupunguza kutapika.
Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa afya ya mama na mtoto pamoja na sababu za kiusalama, inashauriwa mwanamke mjamzito asitumie zaidi ya 1.5 gramu za tangawizi kwa siku.
2. Hedhi
Baadhi ya wanawake hupitia kipindi cha maumivu makali sana wakati wa hedhi.
Tangu zama za kale, tangawizi imekuwa inatumika katika kukabiliana na changamoto hii.
Majibu ya majaribio kadhaa ya kisayansi yanaonesha kuwa mzizi huu ukitumika siku 2-3 kabla ya hedhi, kisha ukaendelea kutumiwa kwa siku zote za hedhi zilizobaki huwa na uwezo wa kupunguza kabisa maumivu kwa uwiano uleule kama zilivyo dawa zingine za kuondoa maumivu. (5,6,7)
Husaidia pia kupunguza dalili zingine za hedhi hasa tumbo kujaa gesi.
3. Mafuta
Lehemu mbaya ambayo hufahamika zaidi kama Low Density Lipoproteins (LDL) huhusishwa moja kwa moja na magonjwa mengi ya moyo.
Kuna ushahidi wa kutosha kutoka kwenye tafiti zilizofanyika kwa wanyama na binadamu kuwa tangawizi inaweza kupunguza na kuharibu lehemu mbaya hivyo ni muhimu sana kwa watu wenye changamoto hii kutumia tangawizi kama sehemu ya tiba yao. (8,9,10)
Kujaa kwa lehemu mbaya kwenye mishipa ya damu huongeza pia nafasi ya kupatwa na kiharusi na shinikizo kubwa la damu.
4. Saratani
Saratani ni ugonjwa unaosababishwa na kukosekana kwa udhibiti wa taarifa za ukuaji wa seli husika za mwili.
Kemikali za gingerol ambazo hupatikana kwa wingi kwenye tangawizi mbichi huwa na uwezo wa kukinga pamoja na kudhibiti ukuaji wa aina mbalimbali za saratani mwilini (11,12)
Kwa kuwa saratani imekuwa ni miongoni mwa magonjwa makubwa yanayosumbua watu wengi sana nyakati hizi, ni vizuri kama jamii zetu zinaitazama tangawizi kwa jicho la pili kama mojawapo ya silaha muhimu sana ya kinga.
5. Mfumo wa Chakula
Maumivu makali ya tumbo pamoja na kujaa gesi ni changamoto kubwa kwa watu walio na matatizo kwenye mfumo wa chakula.
Changamoto hizi hutokana na kushindwa kusagwa kikamilifu kwa chakula au pia kukawia sana kutolewa nje kwa mabaki ya chakula kisichotumika mwilini kwa njia ya choo. (13,14)
Tangawizi hutibu matatizo haya kwa kuongeza minongeo ya chini ya mfumo wa chakula hivyo kurahisisha utoaji wa choo, kuondoa gesi pamoja na kuwezesha uvunjwaji sahihi wa chakula kwenye mfumo huu.
6. Sukari
Tangawizi siyo tiba ya kisukari, lakini husaidia kwa kiasi kikubwa sana katika kuweka sawa uwiano wa sukari mwilini hasa kwa wagonjwa wenye aina ya pili ya kisukari. (15,16,17)
Watu wenye kisukari wanashauriwa kutumia mara kwa mara kiungo hiki ili kuimarisha afya zao.
7. Sumu na Uvimbe
Harufu na ladha halisi ya tangawizi huchangiwa na uwepo wa mafuta yake ambayo kwa asilimia kubwa huwa ni Gingerol.
Gingerol ndio kemikali kuu inayopatikana kwenye tangawizi.
Kemikali hii huwa na sifa kubwa ya kuondoa sumu mwilini, kulinda seli za mwili pamoja na kuzuia au kutibu aina mbalimbali za uvimbe. (18)
Usiogope ukali na harufu yake, gingerol ndio chanzo cha hayo yote.
8. Maungio ya Mwili
Kama tulivyosema hapo awali, tangawizi huwa na uwezo wa kuzuia pamoja na kutibu aina mbalimbali za uvimbe mwilini.
Sifa hii inaweza kutumika pia katika kueleza kazi ya mzizi huu kwenye kushughulikia tatizo la maumivu ya maungio ya mwili hasa kwenye miguu, mikono na magoti.
Wazee ambao kwao changamoto hizi huja mara nyingi zaidi kuliko vijana wanaweza kutumia mzizi huu kama sehemu ya maisha yao ya kila siku. (19)
Vijana na watu wengine wa rika na jinsia zote wanaweza pia kuitumia kwa kazi hiyo.
9. Uzito
Tafiti nyingi za tangawizi zilizofanyika kwa watu wenye uzito mkubwa zimeonesha majibu chanya yanayotia faraja.
Ifahamike kuwa tangawizi siyo jawabu pekee linaloweza kufanikisha zoezi la kupunguza uzito na viribatumbo, ni lazima pia nidhamu ya mlo na tabia ya mhusika vifanye kazi kwa pamoja.
Utaratibu unaotumiwa na tangawizi katika kupunguza uzito wa mtu haupo wazi sana.
Lakini inaaminika kuwa uwezo wa mzizi huu katika kuingilia mifumo mbalimbali ya mwili hasa ile inayohusiana na uunguzwaji wa nishati ndio hufanikisha zoezi hili. (20,21,22)
Hupendi kuwa kibonge? Tumia tangawizi mara kwa mara.
10. Wanaume
Tangawizi huongeza uzalishwaji wa vichocheo vya kiume, hupunguza uharibifu wa kuta za ndani ya korodani, huondoa sumu pamoja kupanua mishipa ya damu inayoelekea kwenye uume.(23)
Ifahamike kuwa ufanisi wa tendo la ndoa kwa mwanamme pamoja na mambo mengine, hutegemea pia ukubwa wa msukumo wa damu kuelekea sehemu za siri.
Tangawizi hufanya kazi hii zote kwa ufanisi mkubwa sana.
11. Kikohozi na Mafua
Pengine huwa unakunywa tangawizi kwenye kutibu kikohozi na mafua pasipo kuelewa inafanya vipi kazi hii.
Tangawizi hufungua mfumo wa hewa pamoja na kupunguza uzalishwaji wa ute unaoziba mfumo huu.
Huwa pia na sifa ya kupambana na aina mbalimbali za virusi wanaosababisha mafua, pamoja na kuongeza uimara wa kinga mwili. (24,25)
Ni dawa nzuri ya kikohozi na mafua.
12. Kinywa
Husaidia katika kuimarisha afya ya kinywa kwa kupambana na bakteria wabaya wanaopatikana humo.
Kampaundi za gingerols hudhibiti ukuaji wa bakteria hao, hasa wale wanaosababisha maambukizi ya fizi. (26)
Magonjwa ya kinywa na meno ni mabaya, tumia tangawizi ujilinde dhidi yake.
13. Maumivu ya Misuli
Tafiti za afya zinathibitisha kuwa watu wanaotumia tangawizi baada ya kufanya mazoezi hupona haraka maumivu ya misuli yao kuliko wale wasiotumia mmea huu. (27)
Muhtasari
Jambo zuri kuhusu mzizi huu ni jinsi unavyoweza kutumiwa kwa namna tofauti.
Unaweza kutumia kama chai, unaweza kutafuna au pia inaweza kuongezwa kwenye mapishi ya chakula kama sehemu ya viungo.
Uchaguzi ni wako.