Ni kipindi cha kupevushwa na kutolewa kwa mayai ya uzazi.
Kipindi hiki hutawaliwa na mabadiliko makubwa ya kimwili na kihisia.
Dalili za uwepo wa hali hii hutofautiana miongoni mwa wanawake, baadhi yao huwa hawawezi hata kuhisi mabadiliko haya.
Muda wa ovulation pia hutofautiana, wengine wakipata siku hiyo hiyo kila mwezi huku wengine wakipata siku tofauti tofauti.
Kwa kuwa ovulation huwa ni kipindi cha mwanamke kupevusha mayai na kupata ujauzito, ni vizuri kujua dalili zinazoambatana na hali hii.
1. Ute
Ute wa mlango wa kizazi huzalishwa kwa wingi wakati huu, hufanana na ute wa yai la kuku lililopasuliwa. (1,2,3,4)
Kwa baadhi ya wanawake huweza kugundua uwepo wake kupitia nguo zao za ndani, baadhi kwa kuingiza vidole ukeni na namba fulani ya wanawake huwa hawaelewi kabisa juu ya uwepo wa ute huu, kwani huwa hawaoneshi dalili yoyote inayoashiria uwepo wake.
Kazi ya ute huu ni kutoa ulinzi kwa mbegu za kiume pamoja na kusaidia ili ziweze kuogelea vizuri kulifuata yai.
Kutokupata ute huu inaweza kuwa ishara ya kutokutoa mayai yaliyopevuka, pamoja na uwepo wa tatizo la mvurugiko mkubwa wa homoni, hasa ikiwa hedhi yako husumbua kila mwezi.
Kutokupata ute sio hukumu ya mwisho kuwa huwezi kupata ujauzito.
Inawezekana kabisa ukawa mjamzito bila kuwa na ute huu, au pia kama upo mdogo sana japo ni wazi kuwa zoezi hili linaweza kuwa gumu kidogo ukilinganisha na mwanamke anayepata ute.
2. Joto
Utaafikiana na mimi kuwa kabla ya siku ya ovulation, joto la mwili huwa halibadiliki sana na mara nyingi hubaki sawa kila siku.
Siku moja au saa kadhaa kabla ya ovulation joto hushuka kisha hupanda kiasi.
Mwanamke anaweza kuhakiki kwa kuingiza kidole kwenye uke, au kwa kutumia vifaa maalumu. Ataona kuwa hali ya siku hii ipo tofauti kabisa na siku zingine zote. (5,6,7,8,9)
Ongezeko hili la joto linaweza kuendelea kuwepo kwa muda wa siku 3-4 kisha hushuka baada ya kumalizika kwa kipindi hiki.
3. Maumivu
Inawezekana kabisa kuhisi maumivu upande fulani wa sehemu ya chini ya tumbo, na ukifuatilia zaidi utagundua kuwa maumivu haya hutokea siku ileile kwenye mzunguko wako wa hedhi yakibadilisha upande.(10,11)
Hii ni ishara kuwa upande husika ndipo yai linatolewa mwezi huo.
4. Mlango wa Kizazi
Mlango wa kizazi nao huonesha mabadiliko kadhaa.
Mfano, wakati wa ovulation mlango huu huongezeka ulaini wake, hupanda juu kidogo, hupanuka kiasi na huwa mbichi sana. (12)
Dalili hii inaweza kuwa ngumu kidogo kuielewa hasa kwa wanawake wasiofuatilia sana mabadiliko ya sehemu zao za siri.
5. Dalili zingine
- Kuongezeka sana kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa
- Maumivu ya nyonga
- Kuwasha na kuvimba kwa matiti
- Kuongezeka kwa uwezo wa kunusa na kutofautisha harufu mbalimbali za vitu
- Sehemu ya nje ya uke (mashavu) au uke wenyewe kuonekana umevimba.
Dalili hizi pia zinaweza kutumika kuonesha uwepo wa hali hii kwa mwanamke. (13,14,15)
Kutokana na kuwepo kwa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, wanasayansi katika vipindi mbalimbali wameweza kutengeneza vifaa vinavyoweza kumsaidia mwanamke kuufuatilia vizuri mzunguko wake, pamoja na kutambua siku sahihi ya ovulation.
Vifaa hivyo maarufu sana kwa jina la Ovulation-Prediction Kits (OPK’s) unaweza kuvitafuta kwa muda wako ili vikusaidie, hasa kama mzunguko wako unasumbua na pengine huoneshi dalili zozote za ovulation.