UHALISIA: Utando Mweupe (Vernix) Anaozaliwa nao Mtoto si Shahawa

4 Min Read

Vernix ni utando mweupe unaotengenezwa kwenye ngozi ya mtoto kwenye kipindi cha mwisho cha ujauzito.

Huundwa na maji kwa asilimia 80, mafuta kwa asilimia 10 na protini kwa asilimia 10. (1)

Utando huu kwa nyakati nyingi umekuwa chanzo cha unyanyasaji kwa wanawake kutokana na uwepo wa dhana potofu tatu ambazo ni mwanamke mjamzito kushiriki tendo la ndoa hadi siku za karibu kabisa za kujifungua, kuzini nje ya ndoa pamoja na mwanamke kupenda kula aina fulani ya vyakula na vinywaji wakati wote wa ujauzito.

Uhalisia

Dhana zote hizi hazina ukweli wowote.

Tofauti na jinsi inavyoaminika mitaani, utando huu hautokani na matumizi ya aina fulani ya chakula au kinywaji, kuzini, uwepo wa ugonjwa au hata mama mjamzito kushiriki tendo la ndoa hasa siku za mwisho kabisa za ujauzito wake.

Watoto waliozaliwa wakati sahihi huwa na kiasi kikubwa cha utando huu huku waliozaliwa kwa kupitiliza siku zao wakizaliwa na utando kidogo sana. (2,3,4)

Vernix siyo shahawa, wala haina uhusiano wowote na kitu hicho

Kazi Zake

Vernix caseosa hufanya mambo kazi kuu 5 ambazo ni;

  • Kuzuia maambukizi ya magonjwa ya ngozi kwa watoto wakati akiwa tumboni na baada ya kuzaliwa.
  • Kupunguza msuguano kati ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
  • Kutunza joto bora kabisa linalofaa kwa ajili ya ukuaji wa siku za mwanzo za mtoto.
  • Kuipatia ngozi ya mtoto unyevu unaostahili.
  • Kuzuia ngozi ya mtoto isiharibike na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kwa kuwa mtoto huelea kwenye mfuko wa uzazi uliojaa maji (maji ya uzazi) kwa miezi mingi sana, huwa ni lazima utando huu utengenezwe ili kuilinda ngozi ya mtoto kwanza akiwa bado anaelea tumboni kisha baada ya kuzaliwa. (5,6,7,8)

Kuoga

Hakuna sheria inayolazimisha kumuosha mtoto moja kwa moja baada tu ya kuzaliwa na kuukwangua uchafu huu.

Kumuacha mtoto na utando huu kwa muda kidogo kabla ya kumuogesha huwa na faida nyingi kwa afya yake.

Mtoto anaweza tu kufutwa kwa kitambaa kisafi ili kuondoa damu iliyomchafua wakati wa kuzaliwa. (9,10)

Wauguzi huwatenganisha watoto na mama zao baada tu ya kujifungua kwa ajili ya uchunguzi na usafi (kumuogesha).

Uchunguzi ni jambo la muhimu na lazima, lakini kumuogesha mtoto siyo lazima. Unaweza kuamua mwenyewe mtoto aogeshwe lini kwa mara ya kwanza.

Ushauri

Shirika la Afya Duniani (WHO) hushauri kusubiri walau kwa saa 24 ndipo mtoto aogeshwe kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, umuhimu wa kuchelewa kumuogesha mtoto hupungua hasa ikiwa ngozi yake imechangangikana na choo chake cha kwanza.

Katika mazingira haya, kumuogesha mtoto mapema tu baada ya kuzaliwa kwake huwa ni jambo la lazima.

Kutokana na umuhimu wa utando huu pamoja na mazingira halisi yanayo zunguka utengenezwaji wake, ni wazi kuwa mwanamke amekuwa mhanga wa jambo lililo nje ya uwezo wake kwa muda mrefu.

Sasa ni muda sahihi wa kuacha kuwanyanyasa na kuwatuhumu kwa mambo ambayo hayana ukweli wowote.

Badala ya kuendelea kuelekeza mzigo wa lawama kwa wanawake, ni muhimu sasa kwa jamii nzima kujifunza na kufahamu umuhimu wa utando huu kwa afya za watoto. 

Share This Article