Neno sahihi kwa kiingereza ni Syphils.
Ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na viini vya bakteria vijulikanavyo kama Treponema pallidum.
Uambukizwaji
Husambazwa kwa njia ya mgusano wa via vya uzazi yaani ngono kupitia uke, mdomo pia sehemu ya haja kubwa.
Pia, watoto wachanga wanaweza kupata ugonjwa huu kutoka kwa mama zao kupitia kondo la uzazi. (1,2,3)
Ugonjwa huu unaweza kudhuru uume, uke, mlango wa uzazi, sehemu ya haja kubwa, mrija wa mkojo, ubongo, midomo, mfupa, figo na ini.
Usipotibiwa unaweza kusababisha utasa, ugumba au kutokuwa na uwezo wa kurutubisha kwa wanawake na wanaume. (4,5)
Ugonjwa wa kaswende hukua kwa hatua kuu nne.
1. Hatua ya Kwanza
Huonekana wiki 3-4 baada ya kuingiliwa na vimelea vya ugonjwa huu. (6)
Huanza kuonekana kwa mchubuko mdogo wa mduara ambao mara nyingi huwa hauna maumivu.
Mchubuko au kidonda hiki hutokea kwenye eneo mahsusi ambapo vimelea vya ugonjwa vilitumia kuingia mwilini.
Inaweza kuwa mdomoni, sehemu siri au sehemu ya haja kubwa.
Mchubuko huu ambao unaweza kudumu hadi miezi 3 kabla haujapotea huwa ni chanzo kikubwa cha kusambaa kwa ugonjwa huu wakati wa kushiriki tendo la ndoa.
2. Hatua ya Pili
Hii ni hatua ya kati.
Ngozi huanza kutengeneza mabaka na koo huanza kusumbuliwa na vidonda. (7,8)
Dalili zingine za hatua ya pili ya ugonjwa wa kaswende ni;
- Maumivu ya kichwa
- Uchovu
- Homa
- Kupungua kwa uzito wa mwili
- Kunyonyoka kwa nywele
- Maumivu kwenye maungio ya mifupa
3. Hatua ya Tatu
Ni hatua ambayo ugonjwa hujificha, huacha kuonesha dalili zozote za uwepo wake.
Dalili zilizokuwa zinaonekana awali hupotea, lakini bakteria wa ugonjwa huendelea kuwepo mwilini wakizaliana na kuongezeka.
4. Hatua ya Nne
Hii ni hatua ya mwisho ya ugonjwa wa kaswende.
Mara nyingi huanza kuonekana baada ya kupita miaka 3-15 tangu vimelea vya kwanza viingie mwilini. (9,10,11)
Hatua hii ni hatari kwa uhai na huambatana na dalili zifuatazo
- Upofu
- Kupotea kwa uwezo wa kusikia
- Matatizo ya mfumo wa fahamu hasa ubongo na uti wa mgongo
- Kuharibika kwa mifupa
- Kupoteza kumbukumbu
- Homa ya uti wa mgongo
Tiba
Unaweza kutibiwa kwa kutumia madawa za viuavijasumu hasa Benzathine Penicillin G, doxycycline na ceftriaxone kulingana na hatua husika.
Mhudumu wa afya ataelezea matumizi ya dawa pamoja na dozi sahihi kwa kadri atakavyoona inafaa.
Kinga
Ni rahisi sana kujikinga na ugonjwa huu kwa kuwa njia za kuambukizwa kwake zipo wazi.
Kuwa mwaminifu, tulia na mpenzi mmoja pia tumia kinga.
Wakati wa matibabu, ni vizuri ukijizuia wewe na mwenzi wako kushiriki tendo la ndoa ili kuepuka nafasi ya kuambukizana tena. Inafaa msubiri hadi ugonjwa upone.
Watu wote walioshiriki tendo la ndoa na mgonjwa ndani ya miezi 12 wanapaswa kujulishwa ili wapimwe, ikibainika kuwa na ugonjwa na huu matibabu yataanza mara moja. Watu wote walioshiriki tendo la ndoa na mhusika ndani ya siku 90 za nyuma wanapaswa kujulishwa ili wao pia waanze tiba mara moja.
Kaswende ya ujauzito
Ukiwa na ujauzito ni lazima pia utapimwa uwepo wa ugonjwa wa kaswende kwa sababu huongeza nafasi ya kuharibika kwa ujauzito kabla ya kufikia wiki 20, kufariki kwa mtoto kabla ya kuzaliwa pamoja na kujifungua kabla ya wakati.
Ugonjwa huu unaweza kuambukizwa mtoto akiwa tumboni hivyo kumfanya azaliwe akiwa na homa kali, degedege, manjano, vidonda, changamoto za ukuaji pamoja na upungufu mkubwa wa damu.
Athari za ugonjwa huu huenda mbali zaidi kwa kusababisha kuharibika kwa meno, mifupa, macho, masikio na ubongo wa mtoto. (12,13)
Mama mjamzito anapaswa kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huu, pamoja na kupata matibabu sahihi ikiwa atagundulika kuwa na maambukizi yake.
Muhtasari
Uwepo wa ugonjwa wa kaswende wakati wa ujauzito ni chanzo namba mbili kinachofanya watoto wengi wafie tumboni, kujifungua kabla ya wakati pamoja na kujifungua watoto wenye uzito mdogo.
Wanaume wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja pamoja na wafanyakazi wa afya wanao hudumia wagonjwa wa kaswende huathirika pia na ugonjwa huu. (14)
Jikinge, lakini pata tiba sahihi baada ya kuambukizwa ugonjwa huu.