Homoni au kwa lugha nyingine zikifahamika kama vichocheo vya mwili, ndiyo kemikali zinazosambaza taarifa za mwili kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Taarifa hizi huviamuru viungo mbalimbali vya mwili nini cha kufanya na kwa wakati gani. (1)
Tunaposema kuwa unasumbuliwa na tatizo la mvurugiko wa homoni (hormonal imbalance) huwa tunamaanisha kuwa, homoni fulani mwilini mwako zipo nyingi sana, au chache sana kulinganisha na kiwango sahihi kinachopaswa kuwepo.
Mabadiliko madogo ya kiwango cha homoni kinachopaswa kuwepo mwilini kinaweza kusababisha matatizo makubwa kwenye afya ya mhusika, pamoja na utaratibu wa kawaida wa maisha yake ya kila siku. (2,3)
Chanzo
Kuna mambo mengi yanayoweza kusimama kama chanzo cha kuvurugika kwa homoni.
Kwa kuwa mwili wa binadamu huwa na homoni nyingi zinazozalishwa na tezi tofauti tofauti, sababu au vyanzo vya tatizo hili hutofautiana pia.
Miongoni mwake ni Matumizi ya baadhi ya madawa, mfano bangi, Matibabu ya saratani, Uvimbe kwenye tezi za pituitary, Mkazo (stress), Ajali, Magonjwa hasa ya kisukari na yale yanayohusisha tezi za thyroid, Umri wa ukomo wa hedhi, Ujauzito na unyonyeshaji, Matumizi ya njia za uzazi wa mpango mfano kitanzi, majira, vijiti au sindano za depo provera.
Aidha, Uzito uliozidi pamoja na mtindo mbaya wa maisha hasa upande wa mlo na vinywaji unaweza pia kuwa chanzo cha kutokea kwa tatizo hili.
Dalili
Dalili za uwepo wa tatizo hili hutofautiana kulingana na aina ya homoni inayosumbua, sehemu ambayo homoni husika hufanya kazi pamoja na jinsia ya mhusika.
Kwa ujumla wake, tatizo hili huwa na dalili za uwepo wa Mvurugio wa mzunguko wa hedhi unaoweza kusababisha hedhi ije kubwa sana, hedhi isionekane kwa miezi kadhaa, hedhi ipotee kabisa au pia ije bila kufuata utaratibu maalum huku ikiambatana na maumivu makali sana.
Kusumbuliwa na matatizo ya usingizi, Chunusi nyingi, Uchovu bila sababu, Kupoteza kumbukumbu haraka, Kichefuchefu, kuharisha pamoja na maumivu ya tumbo yanayotokea bila mpangilio maalumu, Kupoteza hamu ya kula pamoja na ongezeka la ghafla la uzito wa mwili bila sababu maalumu.
Kwa baadhi ya wakawake uke kuwa mkavu pamoja na kupungua au hata kuisha kabisa kwa hamu ya kushiriki tendo la ndoa, kutokwa sana na jasho kila mara, msongo wa mawazo pamoja na ugumba.
Dalili zingine ni kuota kwa ndevu pamoja na nywele kwenye sehemu mbalimbali za mwili (Wanawake), maumivu makali wakati wa tendo la ndoa na kwa wanaume, huwa na dalili ya ziada ya kupunguza hamu na ufanisi kwenye kushiriki tendo la ndoa
Tiba
Mhudumu wako wa afya atauliza maswali kadhaa hivyo ushirikiano wa kutosha unapaswa kutolewa.
Ikiwa ataona inafaa, vipimo vitachukuliwa ili kubaini homoni zinazosumbua kwa wakati huo.
Utaratibu wa aina ya matibabu, dawa pamoja na dozi utategemea na homoni zenyewe, ukubwa wa tatizo na athari zilizopo kwa wakati huo.
Ikiwa homoni zako zitakuwa ni chache, matibabu makuu ni kupewa dawa zenye kuweka sawa homoni hizo, utaratibu ambao kitaalam huitwa Hormone Replacement Therapy ambayo inaweza kufanyika kwa njia ya sindano au vidonge.
Kwa watu wenye homoni nyingi kuliko kiwango cha kawaida, baadhi ya dawa zinaweza kutumika, upasuaji, tiba ya mionzi au mjumuiko wa njia zote unaweza kufanyika.
Baadhi ya dawa zinazoweza kutumika ni Metformin, Levothyroxine na Clomiphene citrate.
Kinga
Mvurugiko wa homoni unaweza kuwa na madhara hasi kwa afya ikiwa hautatibiwa haraka.
Kwa kuwa tatizo hili limekuwa kubwa sana siku hizi kutokana na athari za aina ya maisha tunayoishi, ni muhimu kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kubaini kama lipo, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Baadhi ya mambo yanayoweza kufanyika ili kujikinga na tatizo hili ni Kutunza uziti sahihi wa mwili, kula mlo bora, kufanya mazoezi ya mwili, kudhibiti stress pamoja na kupata muda mwingi wa kupumzika, kufuatilia tiba sahihi ikiwa unaugua magonjwa sugu pamoja na kutokuvuta sigaara.
Tatizo hili hukaribisha magonjwa sugu, pamoja na kudumaza ubora wa afya ya uzazi kwa ujumla wake.
Muhtasari
Kama unapatwa na dalili usizozielewa ni muhimu kufika hospitalini ili upats uchunguzi na tiba. Kwa kuwa homoni za mwili ni balozi mwema anayetoa taarifa mbalimbali zenye kuupa amri mwili wako, ni lazima uhakikishe zipo sawa kila muda.