Usijiachie sana katika kuzungumza au kufanya matendo fulani unapokuwa na mwanao mwenye kati ya umri wa miaka 0-3 ukijua kuwa hafahamu kitu.
Tafiti zinaeleza kuwa hu ni umri ambao tabia na mienendo ya wazazi huwa na athari za moja kwa moja kwenye ukuaji wa mtoto.
Miaka 0-3 ni umri ambao ubongo wa watoto hukua kwa kasi kubwa, pamoja na kujifunza mambo mbalimbali.
Vitendo wanavyofanya wazazi huviona na kuvihifadhi, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa tabia na mienendo yao ya baadae.
Mfano mdogo ni wazazi kugombana, kupigana au kushiriki tendo la ndoa mbele ya mtoto mwenye umri huo huku anawaona moja kwa moja, au tabia ya wazazi kubaki uchi au kuvaa nguo zao za ndani mbele ya watoto wao hasa wale wenye jinsia tofauti huku wanaona.
Huu ni wakati ambao mtoto anaweza kujengewa utu, upendo, tabia njema, utii pamoja na kuheshimu binadamu wenzake kuliko wakati mwingine wowote.
Chuki, majivuno pamoja na tabia zote mbovu anaweza kuzipata pia wakati huu.
Ni muhimu kwa wazazi kuwa makini, tabia nyingi za watoto ni matokeo ya maneno na matendo yao wenyewe. Hawasemi, lakini huona.