Umewahi kusikia wanaume wakijadiliana kuwa mtu akinywa dawa za kupunguza maumivu aina ya paracetamol (Panadol) pamoja na Energy Drinks huongeza nguvu za kiume? Umewahi pia kujaribu kuona kama kinachosemwa kina ukweli?
Vinywaji vya kuongeza nishati mwilini (Energy Drinks) hutengenezwa kwa kutumia viambata vingi kama caffeine, Maji, aina mbalimbali za Vitamini B, Sukari, viondoa sumu Pamoja na kiwango kidogo cha Madini.
Aidha, huwa pia na kemikali zinazosisimua na kuamsha mwili kama vile Guarana, taurine na L-carnitine. Kemikali hizi huongeza pia upumuaji, mapigo ya moyo pampja na shinikizo la damu.
Kwa upande mwingine, Paracetamol ni dawa iliyoanza kutumika tangia mwaka 1893 kushusha homa na kutuliza maumivu ya mwili.
Uhalisia
Panadol na Energy Drinks siyo dawa za kuongeza nguvu za kiume, ni mchanganyiko hatari kwa afya ya binadamu. Panadol ni dawa inayotajwa na tafiti kuwa na uwezo mkubwa wa kuharibu ini la binadamu. Aidha, matumizi ya mara kwa mara ya Panadol yanaweza kuharibu figo
Kutokana na uwepo wa kiwango kikubwa cha Caffeine na kemikali zinazosisimua na kuamsha mwili, energy drinks huongeza msukumo wa damu mwilini, huongeza mapigo ya moyo Pamoja na kuufanya moyo ufanye kazi kubwa kuliko kawaida.
Kwakuwa ufanisi wa tendo la ndoa Pamoja na mambo mengine hutegemea msukumo wa damu mwilini, mtumiaji wa kinywaji hiki hujihisi kuwa na nguvu kwa muda mfupi pasipo kufahamu madhara yake.
Hii inaweza kusababisha kupanuka kwa moyo, kuharibika kwa ini na figo Pamoja na kupasua au kuziba mishipa ya damu hivyo kusababisha kifo, au hata athari za muda mrefu kwenye afya ya mtumiaji.
Madhara haya huchukua muda kuonekana, japo kwa baadhi yanaweza kuonekana ndani ya muda mfupi hivyo ni muhimu kuepuka matumizi ya mchanganyiko huu.
Panadol na Energy Drinks haviongezi nguvu za kiume. Huo ndio uhalisia.