Unjiti ni hali inayotokea baada ya mtoto kuzaliwa kabla hajakamilisha wiki 37 za ujauzito. Watoto waliozaliwa kwenye hali hii huitwa njiti.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kila kundi la watoto 10 wanaozaliwa, 1 kati yao huzaliwa na hali ya unjiti. Aidha, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita hadi 2023, takriban watoto milioni 152 walizaliwa wakiwa njiti.
Makundi ya unjiti hugawanywa kwenye makundi makuu matatu kulingana na umri wa kuzaliwa kwa mtoto.
Makundi hayo ni watoto njiti waliopindukia ambao huzaliwa chini ya wiki 28 za ujauzito, watoto njiti wa kati ambao huzaliwa kati ya wiki 28 na kabla ya wiki 32 na watoto njiti wa kawaida wanaozaliwa kati ya wiki 32-37.
Hali hii huathiri dunia nzima, lakini maeneo ya Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini mwa Bara la Asia ndio hutoa idadi kubwa ya visa hivi.
Sababu za Kuzaliwa Njiti
Mwanamke kujifungua kabla ya wakati husababishwa na mambo mengi huku mara nyingi ikichangiwa na sababu zisizo wazi.
Aidha, sababu za kitabibu kama vile uwepo wa maambukizi makali mwilini mwa mama mjamzito, zinaweza kuchangia kuanzishiwa kwa uchungu wa mapema hivyo kujifungua mtoto njiti. Mambo mengine ni Kisukari, Shinikizo kubwa la damu (Presha) pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa, Pombe na Sigara.
Pia, changamoto za kitabibu kama vile mabadiliko ya homoni, kukaa vibaya kwa kondo la uzazi, kupasuka kwa chupa ya uzazi pamoja na kufunguka mapema kwa mlango wa kizazi, kuwa na ujauzito wa mtoto zaidi ya mmoja na kuwa chini ya miaka 18 na zaidi ya miaka 35 huchangia kutokea kwa hali hii.
Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), wanawake wenye ujauzito ambao haujakamilisha wiki 37 wanapaswa kufika mapema hospitalini kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ikiwa watakuwa wanapatwa na maumivu ya mara kwa mara ya tumbo yanayofanana na yale ya hedhi, kupatwa na hisia ya kushuka kwa mtoto, maumivu ya kiuno na mgongo pamoja na kuongezeka kwa majimaji yanayotoka kwenye uke ambayo yanaweza kuwa ni ishara ya kupasuka mapema kwa chupa ya uzazi.
Hizi zinaweza kuwa ni ishara muhimu za kuwahi kwa uchungu wa uzazi, hivyo msaada wa haraka unahitajika ili kunusuru uhai wa mama na mtoto.
Kinga
Hakuna njia sahihi inayoweza kutumika kama kinga ya kumfanya mwanamke asijifungue watoto njiti kwa kuwa kama tulivyofafanua awali, hali hii mara nyingi husababishwa na mambo yasiyofahamika.
Hata hivyo, baadhi ya tabia njema na mtindo bora wa maisha vinaweza kumfanya mwanamke apunguze nafasi ya kupatwa na hali hii.
Baadhi ya mambo yenye msaada mkubwa katika kuepusha hali hii ni kula mlo bora kabla na wakati wa ujauzito, kunywa maji ya kutosha walau lita 2 za maji wakati wa ujauzito, kutumia kiwango kidogo cha Aspirin kisichozidi gramu 80 kwa siku kama una historia ya shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito, kuacha kutumia dawa bila ushauri wa mfamasia au daktari, kuepuka unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara pamoja na madawa ya kulevya pamoja na kunguza stress (Msongo)
Muhtasari
Mwanamke aliyeanza kuonesha dalili za kupata uchungu wa mapema anaweza kusaidiwa kutokana na dalili atakazokuwa anaonesha wakati huo, pamoja na chanzo cha kutokea kwa hali hiyo ikiwa itagundulika.
Baadhi ya njia hizo ni kupewa dawa za homoni, kushonwa kwa mlango wa kizazi ikiwa utakuwa umelegea na kutanuka kabla ya muda wake halisi (Cerclage) pamoja na mama mjamzito kupata muda mwingi wa kupumzika (bed rest).