Ujauzito: Muda Sahihi wa Kujifungua

4 Min Read

Tumezoea kusikia mtaani wakisema mtoto huzaliwa baada ya miezi 9 ya kubeba ujauzito. Kisayansi hii imekaaje?

Ujauzito wa mwanamke hugawanywa kwenye vipindi vitatu vilivyo na tofauti ya wiki 12. Kitaalam, huitwa trimesters.

Kipindi cha kwanza huanza baada ya kutungwa kwa ujauzito hadi kufikia wiki ya 12, kipindi cha pili huanzia wiki ya 13-27 na kipindi cha tatu huanzia wiki ya 28-40.

Vipindi hivi hutofautiana kwa sifa, tabia na namna ya ukuaji wa mtoto.

Umri Sahihi wa Ujauzito

Kisayansi, mtoto huzaliwa muda wowote kati ya wiki ya 37-42, hivyo mwanamke huwa na wiki 5 za kusubiria mtoto azaliwe pindi muda huu unapofika.

Ikitokea mwanamke kajifungua kabla ya wiki 37, mtoto huchukuliwa kuwa njiti, yaani hajakomaa. Pia, ujauzito uliozidi wiki 42 huchukuliwa kama ujauzito uliopitiliza, na mwanamke hupaswa kuanzishiwa uchungu ikiwa bado atakuwa hajapata dalili za kujifungua mwenyewe.

Makadirio ya Kujifungua kwa Ultrasound

Kupitia kipimo cha ultrasound, mwanamke anaweza kuambiwa tarehe ya matazamio ya kujifungua kwake, tarehe ambayo kitaalam huitwa Estimated Date of Delivery (EDD). 

Hata hivyo, ni takriban 5% pekee ya wanawake ndio hujifungua kwenye siku hiii kama ambavyo kipimo kimesema. Katika hali ya kawaida, mwanamke anaweza kujifungua muda wowote kwa wastani wa wiki 2 nyuma au wiki 2 mbele zaidi ya tarehe hii ya matazamio.

Wanawake wanapaswa kujiandaa kikamilifu kwa kutambua kuwa inapofikia wiki ya 37, muda wowote wanaweza kujifungua.

Inapotokea siku ya kujifungua kwa mujibu wa makadirio ya kipimo imepita hawapaswi kuwaza, kusikitika wala kuhuzunika kuwa mtoto atakuwa amepatwa na jambo baya, hiyo ni tarehe ya makadirio tu na inaweza isitimie kwenye uhalisia.

Watoto wengi huzaliwa lini?

Kwa mujibu wa taasisi ya National Centre for Health Statistics, takriban 90% ya watoto huzaliwa wakiwa wamekomaa kwa kufuata takwimu zifuatazo;

  • 57.5% huzaliwa kati ya wiki 39-41
  • 26% huzaliwa kati ya wiki 37-38
  • 7% huzaliwa kati ya wiki 34-36%
  • 6.5% huzaliwa kati ya wiki 41 na kuendelea
  • 3% huzaliwa kabla ujauzito haujafikisha wiki 34

Kuhesabu Umri wa Ujauzito

Wanawake wajawazito hushauriwa kutumia hesabu ya wiki badala ya miezi ili kufahamu vyema maendeleo ya ujauzito wao pamoja na muda sahihi wa kujifungua.

Mathalani, ikiwa mwanamke atatumia hesabu ya miezi, anaweza kuchanganyikiwa ikiwa ujauzito wake utafikia miezi 10, wakati kwa hesabu za wiki ingekuwa bado yupo kwenye muda sahihi.

Kwa hesabu za kliniki ya mama na mtoto, ujauzito huhesabiwa kuanzia tarehe (siku) ya kwanza ya hedhi ya mwisho hivyo ni muhimu kwa mama mjamzito kutunza vyema kumbukumbu ya siku hii ili kurahisisha zoezi la upigaji wa hesabu katika kupata umri sahihi wa ujauzito na matarajio ya siku ya kujifungua.

Muhtasari

Mwanamke hutumia takriban siku 280 kulea ujauzito tangu siku kutungwa kwake hadi siku ya kujifungua.

Hii ni wastani wa wiki 40 ambazo kitaalam huchukuliwa kama muda sahihi wa mwanamke kujifungua.

Hata hivyo, muda wowote kuanzia wiki ya 37-42 huchukuliwa kama kawaida, na mwanamke hupasws kujiandaa kikamilifu kwani uchungu wa uzazi unaweza kutokea wakati wowote.

Share This Article