Stafeli: Virutubisho na Faida kwa Afya

5 Min Read

Stafeli ni tunda ambalo rejea za kihistoria zinalitaja kuwa na asili ya Afrika na Marekani ya Kusini.

Kisayansi, tunda hili huitwa Annona muricata.

Virutubisho

Kwa mujibu wa USDA, stafeli ni tunda lenye nishati, protini, mafuta, wanga, nyuzilishe, sukari, madini chuma, calcium, magnesium, phosphorus, zinc na copper.

Huwa pia na vitamini C, beta carotene, choline na folate.

Tutazame faida zake kwa afya ili siku nyingine unapokula uelewa umuhimu wake kwenye afya yako;

1. Mfumo wa Chakula

Tunda la stafeli huwa na zaidi ya 80% ya nyuzilishe zinazotakiwa kila siku, kirutubisho muhimu kwenye kuboresha mfumo wako wa chakula.

Pamoja na kazi zingine, nyuzilishe hulainisha choo na kupunguza hatari ya kuugua saratani ya utumbo mkubwa. (1,2,3)

Kila mara unapopatwa na changamoto ya kukaa chooni kwa muda mrefu ukiugulia maumivu makali, likumbuke tunda hili.

2. Kudhibiti Uvimbe

Mwili wa binadamu hujilinda kwa namna nyingi ikiwemo kuamsha kinga za mwili ambazo hukabiliana na tishio lolote kwa kutengeneza uvimbe joto (Inflammation).

Hali hii inaweza kuchangiwa na vimelea vya magonjwa, mzio au kemikali hai zenye sifa kubwa ya kuharibu seli za mwili zinazofahamika kama free radicals.

Kwa kuwa tunda hili huwa na kiwango kikubwa cha viondoa sumu, uwezo wake wa kudhibiti uvimbe hauwezi kutiliwa shaka.

3. Kuzuia Saratani

Tafiti nyingi zinazohusiana na uwezo wake wa kudhibiti saratani zimefanyika maabara pasipo kuhusisha moja kwa moja mwili wa binadamu.

Lakini, kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Saratani ya Uingereza (CRUK), stafeli huwa na uwezo wa uwezo wa kuua aina fulani ya seli za saratani ya ini na matiti.

Taarifa hiyo inaelezea pia uwezo wa stafeli kwenye kutibu saratani ya tezi dume kupitia utafiti wa panya.

Hadi sasa hakuna taarifa nyingi za kitafiti kwenye eneo hili. Maelezo yaliyopo sasa yanahitahi kupimwa na kuthibitishwa kwa tafiti nyingi zaidi.

4. Bakteria

Tafiti za afya zinafafanua uwezo wa stafeli kwenye kupambana na aina mbalimbali za bakteria. 

Faida hizi hazipatikani kwenye tunda pekee, bali hata kwa kutumia kemikali zinazopatikana kwenye majani yake.

Katika utafiti mmoja, kemikali zinazopatikana kwenye stafeli ziliweza kuua aina mbalimbali za bakteria wanaosababisha kuoza kwa meno. (4)

Pia, utafiti mwingine ulionesha mafanikio makubwa katika kupambana na bakteria wanaosababisha kipindupindu. (5)

Pamoja na uwepo wa faida hizi, ni muhimu kukumbuka kuwa majaribio haya yalifanyika maabara, hivyo tafiti zaidi zinahitajika kuyathibitisha.

5. Shinikizo la Damu

Shinikizo kubwa la damu linaweza kusababisha magonjwa ya moyo, kiharusi pamoja na changamoto zingine kwa afya.

Sababu mojawapo zinazofanya kutokea kwa shinikizo kubwa la damu ni uwepo wa sodium nyingi mwilini.

Stafeli huwa na kiwango cha kutosha cha madini ya potassium ambayo huusaidia mwingi kutoa nje kiasi cha ziada cha madini ya sodium pamoja na kuimarisha afya ya mishipa ya damu.

Unaweza kulitumia kila mara ili likupe faida hii.

6. Kisukari

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban watu milioni 422 duniani wapo na tatizo la kisukari. Pia, wastani wa watu milioni 1.5 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo yenye uhusiano na ugonjwa wa Kisukari.

Katika utafiti mmoja uliofanyika kwenye panya, kemikali za stafeli zilifanikiwa kushusha chini kiwango cha sukari mara 5 zaidi kuliko panya ambao hawakupewa kemikali hizo. (6)

Pia, utafiti mwingine ulionesha kuwa tunda hili linaweza kushusha sukari kwa hadi asilimia 75. (7)

Ni tunda zuri lenye faida kubwa kwa watu walio na ugonjwa wa kisukari.

7. Uchafu Ukeni

Maambukizi ya fangasi jamii ya Candida kwa kiasi kikubwa huwafanya wanawake watokwe na uchafu wenye harufu mbaya ukeni.

Tafiti nyingi za afya zinaelezea uwezo wa kemikali zinazopatikana kwenye majani ya mti wa stafeli katika kupambana na fangasi hawa. (8)

Mfano, katika utafiti mmoja uliofanyika mwaka 2020, kampaundi za terpenoids  zinazopatikana kwenye majani ya mstafeli zilikuwa na uwezo wa kudhibiti fangasi wa candida kuzidi dawa za ketoconazole na nystatin. (9)

Watafiti hawa wanaweka bayana kuwa kampaundi hizo zinaweza kutumika katika kubuni dawa mpya za kupambana na fangasi hao wenye kero nyingi kwa afya ya uzazi, hasa kwa wanawake.

Muhtasari

Tunda hili ni tamu sana, pia halina gharama kubwa.

Japokuwa upatikanaji wake wakati mwingine huwa siyo mrahisi, jitahidi ulitumie kila unapopata nafasi.

Kazi kwako.

Share This Article