Mbegu za Chia: Faida, Virutubisho na Tahadhari

5 Min Read

Kisayansi huitwa Salvia hispanica ambazo asili yake inatajwa kuwa ni nchi za Mexico na Guatemala.

Virutubisho

Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), mbegu za chia ni chanzo bora sana cha Protini, wanga, nishati, madini chuma, calcium, phosphorus, zinc, copper, selenium na folate.

Huwa pia na virutubisho vya asidi ya mafuta ya Omega 3 na 6, vitamini mbalimbali muhimu, viondoa sumu na nyuzilishe.

Udogo wa mbegu hizi haufanani na ukubwa wa faida zake mwilini. Twende sambamba.

1. Huondoa Sumu Mwilini

Wingi wa viondoa sumu vinavyopatikana kwenye mbegu za chia hutumiwa na mwili kwenye kuondoa sumu za aina mbalimbali hasa zile zinazoua seli za mwili. 

Tendo hili huwa na faida katika kuulinda mwili dhidi ya magonjwa sugu hasa yale yanayohusisha mfumo wa damu na moyo, ubongo na saratani. (1,2,3,4)

Baadhi ya viondoa sumu hivyo ni chlorogenic acid, caffeic acid, myricetin, quercetin, na kaempferol ambavyo huwa pia na faida nyingine ya kuepusha uzee wa haraka usio endana na umri.

2. Mifupa

Mbegu za chia huwa na madini muhimu yanayofaa katika kuimarisha afya ya mifupa. Mfano wa madini hayo ni calcium na phosphorus.

Hufanya pia kazi ya kuboresha misuli ya mwili na usambazwaji wa taarifa muhimu za mwili. (5,6,7)

Watoto, watu wazima na wazee wanaweza kutumia mbegu hizi kwa ajili ya kutunza mifupa yao.

3. Mfumo wa Damu na Moyo

Uwepo wa quercetin hupunguza hatari ya kuugua magonjwa ya mfumo wa damu na moyo. (8,9)

Huwa pia na mafuta ya asidi za Omega 3 na 6 ambazo tafiti kadhaa zinathibitisha uwezo wake katika kulinda moyo dhidi ya ugonjwa wa kubadilika kwa mapigo ya moyo pamoja na mshituko wa moyo. (10,11)

Kwa mujibu wa Taasisi ya Moyo ya Marekani (AHA), mafuta ya Omega 3 hupunguza pia shinikizo la damu pamoja na kupunguza uvimbe.

4. Mfumo wa Chakula

Huwa na faida ya kuboresha mfumo wa chakula kwa kurahisisha mmeng’enyo wa vyakula na kukinga dhidi ya changamoto ya choo kigumu.

Husaidia pia kupunguza uzito wa mwili kwa watu wenye uzito mkubwa bila kuathiri wale wenye uzito wa wastani unaotakiwa kwa afya.

Hili linaweza kufanikiwa kutokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha protini na nyuzi lishe ambazo humfanya mhusika ajisikie kushiba kwa muda mrefu hivyo kupunguza ulaji.

Hata hivyo, mbegu hizi hazina maajabu makubwa katika kupunguza uzito ikiwa nidhamu kubwa haitawekwa kwenye ulaji wa jumla na ushiriki wa mazoezi.

5. Kukabiliana na Lehemu

Rejea ya mwaka 2021 ya tafiti zaidi ya 10 inaonesha kuwa mbegu za chia husaidia kupambana na kushusha lehemu mbaya zisizo takiwa mwilini (LDL) lakini huongeza lehemu nzuri zinazotakiwa mwilini (HDL).

Hii inatoa maana kuwa chakula hiki kinaweza kuwasaidia watu wenye mlundikano wa mafuta mengi yasiyofaa kwenye mishipa ya damu. 

6. Hushusha Sukari

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takriban watu milioni 422 wanaishi na ugonjwa wa kisukari Duniani. Watu wengine takriban milioni 1.5 hupoteza maisha yao kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kisukari.

Utafiti wa mwaka 2017 unaonesha kuwa mbegu za chia zinaweza kusaidia kushusha sukari hasa baada ya kupata mlo wenye kiasi kikubwa cha wanga.

Tafiti zingine zilizofanyika kwa wanyama zinaonesha kuwa mbegu hizi zinaweza kupunguza usugu wa vichocheo vya Insulin kwenye kudhibiti sukari mwilini pamoja na kuongeza uwezo wa mwili kwenye kuweka sawa uwiano wa sukari kwa ujumla. (12,13,14)

Unasubiria nini kuanza matumizi ya mbegu hizi?

7. Faida Zingine

Huwa na madini chuma ambayo husaidia usafirishwaji wa hewa ya Oxygen mwilini pamoja na kuongeza wingi wa damu.

Manganese husaidia ukuaji bora pamoja na kuratibu mifumo mbalimbali ya mwili ili ifanye kazi kwa ufanisi mkubwa.

Chanzo kizuri cha protini kinachohitajika mwilini kufanya kazi mbalimbali ikiwemo kuponya majeraha ya seli na tishu zilizoumizwa. Huwa na aina zote 9 za amino acids ambazo hutengeneza msingi wa protini zote zinazohitajika kwenye mwili wa binadamu.

Muhtasari

Kuna namna nyingi za kutumia mbegu za chia. Unaweza kuziongeza kwenye salad, yogurt au smooth.

Baadhi huziloweka kwanza kwenye maji kabla ya kuzitumia. Yote haya ni sawa.

Mbegu hizi huwa na usalama mkubwa, hata hivyo, kundi dogo la watu huwa na mzio (Allergy) unaoweza kusababisha wapatwe na baadhi ya maudhi yasiyo na maana nzuri kwa afya.

Ikiwa utapatwa na changamoto zozote zile baada ya kutumia mbegu hizi unashauriwa kufika hospitalini haraka kwa uchunguzi na matibabu.

Share This Article