Cardiopulmonary Resuscitation (CPR) ni njia ya dharura na haraka, inayotolewa kwa mtu aliyepatwa na changamoto ya mshituko wa moyo (Cardiac arrest).
Huhusisha kubonyeza kifua pamoja na kutoa hewa mbadala kwa mhusika ili kutunza mzunguko wa damu kwenye viungo muhimu vya mwili ikiwemo ubongo.
Ikiwa itaanzishwa haraka, CPR huokoa uhai na kupunguza vifo kwa asilimia 50-75 kwa watu wenye mshituko wa moyo.
Kama sehemu muhimu ya kuokoa uhai, huduma hii inapaswa kutambuliwa na kufahamika kwa kila mtu. Iliasisiwa na madaktari watatu ambao ni Elam, Safar, na Archer miaka ya 1950.
Namna inavyofanyika
- Kwa watoto wachanga, tumia vidole viwili
- Watoto wakubwa kidogo, walau chini ya miaka 5 tumia mkono mmoja, au unaweza kutumia mikono miwili.
- Watu wazima tumia mikono miwili.
- Bonyeza kifua kuelekea upande wa kushoto ambapo moyo umelalia zaidi mara 100-120 kwa kila dakika. Kila unapobonyeza kifua hakikisha kimezama ndani, na unapaswa kuruhusu kirudi juu kwanza kabla haujabonyeza tena.
- Kama upo peke yako hakikisha kila baada ya kubonyeza kifua mara 30, mpumulie mdomoni mwake mara 2. Kama mpo wawili unapaswa kubonyeza kifua mara 15 kisha mpumulie mdomoni mara 2.
- Wakati huu, hakikisha mawazo na akili zako zote zipo hapo. Usifanye kazi nyingine zaidi ya hii.
- Hakikisha mgonjwa anazungukwa na hewa ya kutosha.
Kwa kuwa mtu asiye na ujuzi wa elimu ya afya ni ngumu kujua mshituko wa moyo ni nini, hivyo atapaswa kufuata kanuni hizi tatu kama silaha yake ya utambuzi.
- Kukata kauli ghafla
- Kukosekana ghafla kwa mapigo ya moyo, hasa kwa kutazama mishipa inayopatikana sehemu ya juu ya shingo, au kwenye maungio ya kiuno na paja (karibu na sehemu za siri)
- Kuzima kwa upumuaji wa mgonjwa
Kama kuna ndugu karibu yeye ndiye aendelee kuita msaada wa watu wengine wa karibu, pamoja na kufanya taratibu za kumpeleka mgonjwa hospitalini huku wewe ukiendelea kubonyeza kifua.
Badala ya kumpumulia moja kwa moja hasa kwa mtu ambaye hufahamu historia ya afya yake, unaweza kutumia kifaa chochote (mfano puto) chenye uwezo wa kusukuma hewa ya kutosha mdomoni mwa mgonjwa.