Kwa karne nyingi sana, binadamu wameishi wakipambana kutafuta namna bora ya kujikinga na maradhi mbalimbali.
Pamoja na ukweli kuwa tabia mbalimbali za kutengeneza chanjo za kiasili zilianza zaidi ya miaka 500 iliyopita, bado uwanda wa sayansi utaendelea kumkumbuka Edward Jenner, ambae Mei 14, 1796 alitoa chanjo ya kwanza ya kitaalam kwa kijana wa miaka 8.
Miaka 80 baadae, Louis Pasteur anaongeza ufahamu wa chanjo kwa kutengeneza chanjo ya kichaa cha mbwa (Rabies) ambayo ilionesha mafanikio makubwa.
Maendeleo kwenye ugunduzi wa aina mbalimbali ya chanjo yalizidi kushika kasi duniani kote.
Leo dunia inajivunia kuwa na chanjo nyingi zenye ufanisi mkubwa katika kudhibiti magonjwa, kupunguza ukubwa wa maambukizi pamoja na kuokoa uhai.
Ufuatao ni utaratibu wa utoaji wa chanjo kwa watoto na wajawazito
1. Kifua Kikuu
Chanjo ya Kifua Kikuu (BCG) hutolewa baada ya mtoto kuzaliwa au anapofika kliniki kwa mara ya kwanza.
Sindano hiyo huchomwa kwenye bega za mkono wa kulia na iwapo halitatokea chanjo husika hufaa irudiwe katika kipindi cha miezi 3.
Huitwa kwa jina maarufu la “Kovu la mtanzania”
2. Polio
Chanjo yake hutolewa kwa njia ya matone ya kumeza kwa utaratibu ufuatao-
- Chanzo ya kwanza, mara tu mtoto anapozaliwa
- Chanjo ya pili, mtoto akifikisha umri wa wiki 6
- Chanjo ya tatu, mtoto akifikisha umri wa wiki 10
- Chanjo ya nne, mtoto akifikisha umri wa wiki 14
3. Pepopunda (Tetanus)
Chanjo ya ugonjwa huu hutolewa kwa wanawake wote wenye umri wa kushika ujauzito pamoja na wale wenye ujauzito tayari ili kuwakinga wao, pamoja na kumkinga mtoto wakati wa ujauzito.
Dozi kamili huhusisha sindano tano ambazo hutolewa kwa utaratibu ufuatao-
- Chanjo ya kwanza hutolewa muda wowote, haidumu sana mwilini
- Chanjo ya pili hutolewa wiki 4 baada ya chanjo ya kwanza, hudumu kwa miaka 3
- Chanjo ya tatu hutolewa miezi 6 baada ya chanjo ya pili, hudumu kwa miaka 5
- Chanjo ya nne hutolewa mwaka mmoja baada ya chanjo ya tatu, hudumu kwa miaka 10
- Chanjo ya tano hutolewa mwaka mmoja baada ya chanjo ya 4, hudumu kwa miaka 20
Ikithibitika kuwa mama aliwahi kupata chanjo tatu za pepopunda utotoni, itahesabiwa ameshapata dozi mbili za chanjo ya Pepopunda, hivyo itabidi aendelee na dozi zingine za chanjo ya Pepopunda ili kukamilisha ratiba.
4. Kifaduro
Ugonjwa huu hukingwa kwa chanjo yenye mchanganyiko wa chanjo za kuzuia dondakoo, Pepopunda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo na kichomi yaani DTP-HepB-Hib ambayo kwa sasa hujulikana kama Pentavalent.
Hutolewa kwa awamu tatu ambazo ni
- Chanjo ya kwanza, umri wa wiki 6
- Chanjo ya pili, umri wa wiki 10
- Chanjo ya tatu, umri wa wiki 14
5. Dondakoo
Ugonjwa huu hukingwa kwa chanjo yenye mchanganyiko wa chanjo za kuzuia dondakoo, Pepopunda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo na kichomi yaani DTP-HepB-Hib ambayo kwa sasa hujulikana kama Pentavalent.
Hutolewa kwa awamu tatu ambazo ni
- Chanjo ya kwanza, umri wa wiki 6
- Chanjo ya pili, umri wa wiki 10
- Chanjo ya tatu, umri wa wiki 14
6. Homa ya Ini
Ugonjwa huu hukingwa kwa chanjo yenye mchanganyiko wa chanjo za kuzuia dondakoo, Pepopunda, Homa ya ini, Homa ya uti wa mgongo na kichomi yaani DTP-HepB-Hib ambayo kwa sasa hujulikana kama Pentavalent.
Hutolewa kwa awamu tatu ambazo ni
- Chanjo ya kwanza, umri wa wiki 6
- Chanjo ya pili, umri wa wiki 10
- Chanjo ya tatu, umri wa wiki 14
7. Homa ya Uti wa Mgongo na Kichomi
Homa ya uti wa mgongo na kichomi husababishwa na vimelea aina mbalimbali.
Moja ya vimelea hivyo ni bacteria aina ya “Haemophilus influenzae” ambao wapo katika makundi sita (a, b, c, d, e na f), magonjwa ya homa ya uti wa mgongo na kichomi husababishwa na Kundi b (Hib).
Magonjwa haya yameenea duniani kote na kwa kiwango kikubwa katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania. Magonjwa haya yanaathiri zaidi watoto wenye umri dhini ya miaka mitano.
Njia muhimu ya kujikinga na magonjwa haya ni kupata hanjo ya DTP-HepB- Hib au Pentavalent. Chanjo hii ipo kwenye mchanganyiko wa chanjo ya dondakoo, kifaduro, pepopunda na homa ya ini.
Njia nyingine za kupunguza uwezekano wa kupata maambukizi ya Hib ni pamoja na kujenga au kukaa kwenye nyumba zenye hewa ya kutosha na kuepuka msongamano.
Hutolewa kwa awamu tatu ambazo ni
- Chanjo ya kwanza, umri wa wiki 6
- Chanjo ya pili, umri wa wiki 10
- Chanjo ya tatu, umri wa wiki 14
8. Surua
Ugonjwa wa surua kwa watoto huzuilika kwa chanjo ya surua. Mtoto hupata sindano mbili za kumkinga na surua ambazo hutolewa kwenye bega la kushoto akamilishapo umri wa miezi tisa na marudio baada ya mtoto kutimiza miezi 18.
Iwapo kuna mlipuko wa surua, watoto wenye umri wa miezi 6 na kuendelea inafaa wapatiwe chanjo hata kabla ya kukamilisha miezi tisa, lakini ni lazima irudiwe chanjo hiyo anapokalisha umri wa miezi tisa.
Aidha, ni lazima mtoto apatiwe matone ya vitamin ‘A’ kila anapopata chanjo ya surua.
9. Nimonia na Homa ya Uti wa Mgongo Unaosababishwa na Streptococcus Pneumoniae
Njia muhimu ya kuzuia magonjwa ya Nimonia yanayosababishwa na vimelea vya Streptococcus pneumoniae ni kupata chanjo.
Njia nyingine za kupunguza maambukizi ya Nimonia ni pamoja na usafi wa mazingira, kunawa mikono, lishe bora, unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita na nyongeza ya virutubisho vya zinc uchangiaji katika kupunguza kuenea kwa ugonjwa.
Chanjo husika hutolewa sambamba na chanjo ya Pentavalent hivyo mzazi au mlezi anapaswa kumpeleka mtoto akapate chanjo ya Nimonia akamilishapo umri wa wiki sita.
10. Kuharisha Kunakosababishwa na Rotavirus
Magonjwa ya kuhara yasababishwayo na Rotavirus huzuilika vizuri zaidi kwa chanjo ya Rotavirus pamoja na kunyonyesha maziwa ya mama pekee kwa miezi sita.
Aidha, kuimarisha usafi wa mazingira na kunawa mikono kwa sabuni husaidia kupunguza mambukizo ya magonjwa ya kuhara.
Mzazi uhakikishe mtoto anakamilisha chanjo mbili kwa utaratibu uliowekwa ili apate kinga kamili.
- Chanjo ya kwanza itatolewa kati ya umri wa wiki 6 hadi wiki ya 10
- Chanjo ya pili itatolewa kati ya wiki ya 10 hadi wiki ya 32
- Mtoto akishazidisha umri wa wiki 15 hataanzishwa chanjo
- Mtoto akizidisha umri wa wiki 32 hatapatiwa dozi ya pili ya chanjo
Muhtasari
Chanjo hizi hutolewa kwenye kliniki za uzazi pamoja na wakati wowote ambao mhusika atapangiwa kuipata kwa mujibu wa ratiba, kanuni na taratibu za uchanjaji.
Hutolewa bila malipo yoyote.