Dalili, Maambukizi na Tiba ya Ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB)

4 Min Read

Kifua kikuu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya bakteria na huenezwa kwa njia ya hewa. Mtu mwenye maambukizi ya kifua kikuu akikohoa, kupiga chafya au kutema mate ovyo husambaza vijidudu hivyo hewani, huweza kumwambukiza mtu mwingine.

Kwa mujibu wa WHO, mwaka 2021, takriban watu milioni 1.6 duniani walifariki kwa ugonjwa huu huku watu milioni 10.6 wakiambukizwa.

Bakteria jamii ya Mycobacterium tuberculosis ambao husababisha ugonjwa huu hushambulia mapafu, lakini wanaweza kudhuru pia sehemu zingine za mwili hasa figo, uti wa mgongo na ubongo.

Walau robo ya watu wote wa duniani wanaishi wakiwa na bakteria wanaoweza kusababisha ugonjwa wa kifua kikuu, lakini ni idadi ndogo kati yao ndio huingia kwenye hatua ya kuugua ugonjwa huu. Watu hawa huwa hawana sifa ya kusambaza pamoja na kuambukiza ugonjwa huu kwa wengine hadi pale ambapo ugonjwa halisi utakapowapata.

Dalili za Ugonjwa

Dalili za mgonjwa wa kifua kikuu huanza kuonekana taratibu na hutumia mda mrefu hadi ziwe wazi. 

Jambo hili huchelewesha utafutaji wa matibabu ya haraka pamoja na kuongeza nafasi ya kuambukiza watu wengi zaidi. Miongoni mwa dalili za ugonjwa huu ni kukohoa kwa muda wa wiki 2 au zaidi, maumivu ya kifua, homa za usiku, uchovu usio na sababu maalumu, kutoka jasho kwa wingi usiku, kupungua uzito, kukohoa damu pamoja na kukosa hamu ya kula na mwili kuwa dhaifu

    Uhusiano na VVU

    Watu wenye maambukizi ya VVU huwa na uwezekano mkubwa wa kuugua kifua kikuu walau mara 16 zaidi kuliko wale wasio na maambukizi. Hii ni kutokana na kupungua sana kwa uwezo wa mwili katika kupambana na magonjwa kwa watu hawa.

    Pia, watu wenye lishe duni na magonjwa mengine makubwa yanayopunguza kinga ya mwili huwa kwenye hatari zaidi ya kuugua ugonjwa huu. (1,2,3)

    Ni muhimu kukumbuka kuwa siyo kila mtu mwenye kifua kikuu huwa na maambukizi ya VVU. Hii ni dhana mbovu isiyo na uhalisia wowote wa kisayansi.

    Kinga

    Ugonjwa huu hukingwa kwa kuchoma chanjo ya Kifua kikuu (BCG), ambayo hutolewa mara tu mtoto anapozaliwa au anapofika kliniki kwa mara ya kwanza.

    Iwapo kovu halitajitokeza chanjo irudiwe katika kipindi cha miezi 3, nchini Tanzania hujulikana zaidi kama “kovu la mtanzania” linalopatikana kwenye bega la mkono wa kulia.

    Pamoja na chanjo, ili kupunguza uwezekano wa kuugua ugonjwa huu unapaswa kujenga na kuishi kwenye nyumba zinazoruhusu mzunguko kwa hewa ya kutosha, kuepuka kukaa kwenye misongamano ya watu, watoto wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee kwa miezi sita na umlikiza kwa vyakula vyenye virutubisho, kula vyakula vyenye lishe bora pamoja na utotema mate na makohozi ovyo.

      Tiba

      Tiba ya ugonjwa huu ipo lakini huchukua muda mrefu ikiwa imegawanywa kwenye hatua mbili ambazo kwa pamoja zinaweza kuchukua wastani wa miezi 6 hadi mwaka mzima.

      Inashauriwa mgonjwa awahi matibabu mapema kwenye vituo vya kutolewa huduma za kinga ambapo kwa Tanzania dawa hizo hutolewa bure.

      Muhtasari

      Ili kufanya ugonjwa huu uweze kutibika kabisa pamoja na kuondoa usugu za vimelea, ni muhimu kwa mgonjwa kumeza dawa kikamilifu pasipo kuchoka.

      Aidha, ni muhimu kwa waathirika wa VVU kupima mara kwa mara ugonjwa huu ili uweze kutibiwa haraka ikiwa wataupata ili kuondoa madhara makubwa kiafya, ikiwemo kupoteza maisha.

      Share This Article