Faida na Madhara ya Energy Drinks kwa Afya

3 Min Read

Vinywaji vya kuongeza nguvu au maarufu zaidi kama energy drinks vimepata umaarufu mkubwa sana siku za hivi karibuni.

Hii inatokana na kuongezeka kwa utengenezwaji wake, pamoja na idadi ya watu wanaovutumia kila siku.

Viambato

Energy drinks hutengenezwa kwa kuongeza kiasi kikubwa cha kemikali za caffeine, sukari pamoja na viambato vingine vikiwemo guarana, taurine, na L-carnitine.

Aidha, baadhi yake huwekewa pia glucuronolactone, aina mbalimbali za vitamini B, viondoa sumu pamoja na kiasi kidogo cha madini muhimu ya mwili. (1,2,3)

Faida

Husaidia kuuamsha mwili na kuupa nguvu hasa wakati wa uchovu mkubwa. 

Inaweza pia kusaidia katika kuondoa usingizi na kuongeza utimamu wa mwili hasa kwa watu wanofanya kazi ngumu pamoja na wale wanaofanya kazi zinazochukua masaa mengi kwa siku. (4,5)

Kinywaji hiki kama ilivyo kwa vingine hutumiwa na watu kama sehemu ya kiburudisho.

Madhara

Upande wa pili wa shilingi unaohusisha vinywaji hivi unaweza usiwe mzuri sana kwa afya.

1. Magonjwa ya Moyo

Tafiti kadhaa za afya zinahusisha kinywaji hiki na kutokea kwa baadhi ya magonjwa ya moyo. (6,7,8)

Nchini Marekani, zaidi ya watu 20,000 kila mwaka hufikishwa kwenye kitengo cha wagonjwa wa dharura wakiwa na changamoto zinazosababishwa na utumiaji mkubwa wa vinywaji hivi. (9)

Pia, utafiti wa mwaka 2023 uliofanyika kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), unaohusisha kijana wa miaka 28 aliyekunywa chupa 5 za vinywaji hivi unaonesha kuwa huongeza uwezekano wa kuganda kwa damu kwenye mishipa ya damu kutokana na kuamshwa kwa chembe sahani.

Chukua hatua, linda moyo wako.

2. Shinikizo la Damu

Energy drinks zinaweza kusababisha ongezeko kubwa la shinikizo la damu mwilini. 

Hii inatokana na uwepo wa kiasi kikubwa cha caffeine ambacho hubadili mfumo wa kawaida wa kufanya kazi kwa moyo, kubana mishipa ya damu pamoja na kuufanya mwili uzalishe kiasi kingi cha vichocheo vya cortisol ambayo vyote kwa pamoja huwa na athari hasi mwilini kwa kuongeza shinikizo la damu. (10,11)

3. Changamoto Zingine

Vinywaji hivi vinaweza kuufanya mwili upoteze kiasi kikubwa cha maji, huleta hali ya kuweweseka, huharibu mpangilio wa usingizi, huharibu figo pamoja na kuleta uraibu. (12,13,14)

Baadhi ya tafiti huelezea pia madhara ya vinywaji hivi kwenye kuongeza nafasi ya kuugua ugonjwa wa kisukari. (15,16)

Aidha, vinywaji hivi huwa na asidi nyingi ambayo tafiti zimethibitisha kuwa na uwezo wa kuharibu meno hivyo ni hatari kwa afya ya kinywa. (17,18)

Muhtasari

Jitahidi kunywa kiasi kidogo walau chupa 1 kwa siku kwani matumizi makubwa ya kinywaji hiki ni hatari kwa afya yako.

Pia, haupaswi kuchanganya kinywaji hiki pamoja na pombe au dawa. Utaua figo zako.

Share This Article