Benjamin Mkapa Waanza Kubadili Chembe Nyekundu Kutibu Seli Mundu

2 Min Read

Hospitali ya Benjamin Mkapa kupitia kliniki ya magonjwa ya damu imeanza huduma za kubadilisha chembe nyekundu za damu kwa wagonjwa wa seli mundu.

Dkt Stella Malaghale ambaye ni mkuu wa kliniki hiyi amesema huduma hii imeanza rasmi baada ya kupata mashine maalumu inayoitwa apheresis ambapo Juni 15 huduma hiyo ilitolewa kwa mgonjwa wa kwanza.

Huduma hii ya kibingwa itakuwa inatolewa kwa mgonjwa mara moja kila baada ya miezi 3 ili kumpunguzia changamoto nyingi za ugonjwa huu ikiwemo umanjano, maumivu makali ya mwili, upungufu wa damu pamoja na maambukizi ya mara kwa mara ya magonjwa.

Ugonjwa huu wa kurithi huathiri walau watu milioni 20 duniani huku kiasi cha watoto 11000 kila mwaka wakizaliwa nchini Tanzania.

Kwa muundo wake, chembechembe nyekundu za damu huundwa na aina moja ya protini inayoitwa hemoglobin.

Protini hii ndiyo hubeba hewa na kuisafirisha kwenda sehemu mbalimbali za mwili.

Kwa watu wenye afya nzuri, hemoglobin huwa ni laini, ina umbo la duara na huwa inaweza kubadilika umbo lake kirahisi.

Tabia hizi ndiyo huruhusu iweze kupenya kirahisi na kusafiri kila sehemu ya mwili pasipo uwepo wa pingamizi lolote.

Kwa watu wenye ugonjwa huu hali haipo hivyo. Hemoglobin huwa ngumu, ina umbo la mwezi mchanga au herufi C na huwa haibadiliki kirahisi.

Share This Article