UHALISIA: Mwanamke Mjamzito Anaruhusiwa Kula Mayai

3 Min Read

Mayai ni chakula chenye virutubisho vingi vinavyofaa kwa afya ya binadamu. Kwa mujibu wa idara ya Kilimo ya Marekani (USDA), mayai huwa na maji, protini, nishati, mafuta, wanga Pamoja na Madini chuma, Calcium, Magnesium, Copper, Zinc, Potassium, Fluoride na Selenium. Aidha, huwa pia na aina mbalimbali za vitamini muhimu kwa afya Pamoja na viondoa sumu vya Lutein na Zeaxanthin.

Pamoja na uwepo wa virutubisho hivi, kwa miaka mingi mayai yamekuwa yanatajwa kama chakula kisichofaa kwa wanawake wajawazito. Mathalani, Jamii ya Tanzania hasa ile inayopatikana vijijini imeendelea kuamini dhana hii hadi sasa kwa kuamini kuwa mayai huchochea wanawake kujifungua Watoto wenye kichwa kikubwa au wasio na nywele.

Mayai yanapatikana kila sehemu. Ni muhimu kufahamu uhalisia wa madai haya ili kuilinda jamii dhidi ya madhara yanayoweza kutokea kwa wanawake wanaotumia chakula hili.

Uhalisia

Mayai si chakula kibaya kwa wanawake wajawazito, hayawezi kusababisha kupata mtoto mwenye kichwa kikubwa au asiye na nywele.

Taasisi ya Australian Eggs inabainisha kuwa mwanamke mjamzito huhitaji kupata vyakula  yenye utajiri wa virutubisho muhimu ili kuboresha afya yake Pamoja na afya yam toto aliyeko tumboni na yai ni chakula kinachoweza kukidhi hitaji hilo.

Mayai huwa na aina tofauti 13 za Vitamini na madini muhimu, aside za Omega 3 pamoja na viondoa sumu. Yai moja linatosha kutoa 90% ya mahitaji ya kila siku ya Protini kwa mama mjamzito inayosaidia kujenga misuli ya mama na mtoto Pamoja na kuwezesha usafirishaji mzuri wa damu na hewa mwilini.

Huwa na Choline ambayo Pamoja na virutubisho vingine husaidia kutengeneza mfumo imara wa neva za fahamu na uti wa mgongo wa Mtoto.

Mwongozo wa Kituo cha udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC) hushauri wanawake watumie vyakula vyenye wingi wa Asidi ya Foliki ili kuimarisha uti wa mgongo na kuepusha mtoto kuzaliwa na tatizo la Kichwa kikubwa na mgongo wazi. Mayai ni chakula sahihi kwakuwa huwa na kiwango cha kutosha cha kirutubisho hiki.

Mayai huwa na Vitamini A inayosaidia utengenezwaji wa Ngozi imara ya mtoto Pamoja na kuboresha afya yake ya macho. Aidha, huwa na madini ya iodine ambayo tafiti zinabainisha upungufu wake huongeza nafasi ya kujifungua mtoto aliyefariki au hata kuharibika kwa ujauzito kabla ya wiki ya 20.

Kwa ujumla wake, mayai ni chakula bora kwa mama mjamzito. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kuwa wanawake wenye kisukari au wale walio na mafuta mengi kweye mishipa ya damu hushauriwa kutokutumia mayai mengi, na kiwango kinachoshauriwa ni yai moja kwa siku.

Tahadhari

Mayai huwa na bakteria hatari jamii ya Salmonella wanaoweza kuwa hatari kwa mlaji ikiwemo wanawake wajawazito. Bakteria hawa husababisha sumu ya chakula inayoweza kusababisha kuharisha, maumivu makali ya tumbo na kuharibika kwa ujauzito au hata kupoteza Maisha kwa wanawake wajawazito hivyo ni muhimu kuepuka ulaji wa mayai mabichi yasiyochemshwa wala kupikwa ili kujilinda.

Share This Article