Chanzo, Dalili na Athari za Kuharisha kwa Watoto

3 Min Read

Kuharisha ni changamoto inayoweza kutokea kwa mtu yeyote yule. Watoto, watu wazima na wazee wote wanaweza kupatwa na changamoto hii.

Fikiria ambavyo mtu mzima huhangaika anapokuwa anaharisha. Hali ipoje kwa watoto?

Takwimu

Kwa mujibu wa Kituo cha Udhibiti na Kinga ya Magonjwa cha Marekani (CDC), katika kila vifo vya watoto 9 vinavyotokea duniani, kimoja kati yake husababishwa na Kuharisha.

Ni ugonjwa wa pili unaoongoza duniani kwa kuua watoto wengi zaidi wenye umri chini ya miaka 5.

Sababu za Kuharisha

Kwa ufupi, kuharisha ni kitendo cha kujisaidia choo kilaini sana kuliko kawaida walau mara 3 kwa siku. Mara nyingi, choo hiki huwa na ute au maji maji.

Tatizo hili linaweza kusababishwa na mambo mengi ikiwemo maambukizi yanayosababishwa na virusi, bakteria au vimelea vingine. Watoto hupata maambukizi haya kwa kuweka kinywani mikono yao baada ya kugusa uchafu, vyakula au maji yaliyochanganyikana na uchafu.

Pia, allergy (mzio) wa maziwa au dawa anazotumia, hasa antibayotiki (Viuavijasumu), kunywa kiasi kikubwa cha juisi za matunda pamoja na kula sumu kunaweza kusababisha tatizo la kuhara.

Madhara

Madhara makubwa ya kuharisha kwa watoto ni kupoteza maji mengi mwilini pamoja na chumvi muhimu. Kitendo hiki cha hatari kinaweza kumfanya mtoto apatwe na homa kali na kutapika.

Dalili muhimu za kuonesha uwepo wa hali hii ambayo kitaalam huitwa dehydration ni kujisaidia haja ndogo mara chache kuliko kawaida, kuwa mkali sana, mwenye kuweweseka, kukauka kwa midomo, kulia bila kutoa machozi, au kutoa machozi kidogo sana, kukauka kwa ngozi na ulimi, kujisaidia choo cheusi, au chenye damu pamoja na kuwa na macho makavu

    Matibabu

    Kuharisha kwa kiasi kikubwa husababishwa na virusi. Ni namna nzuri ya kutoa sumu za vimelea vya magonjwa. Hata hivyo, tendo hili ni hatari kwa afya kwa kuwa husababisha upotevu mkubwa wa maji mwilini.

    Matibabu hutofautiana kulingana na umri wa mtoto, lakini kwa kawaida hujumuisha mambo yafuatayo;

    • Ongeza unyonyeshaji
    • Punguza kumpa juisi za matunda, zinaweza kuongeza ukubwa wa tatizo
    • Kama anakula vyakula mbadala, mpatie nafaka 
    • Mpatie Oral Rehydration Salt (ORS), zinapatikana kwenye maduka ya dawa na hospitali
    • Kama ana homa, mpatie dawa za kuituliza
    • Msafishe matako yake kwa maji mengi kila baada ya kujisaidia ili asipatwe na allergy (Mzio). Mpake mafuta mgando sehemu ya haja kubwa ili kupunguza maumivu.
    • Anywe maji ya kutosha ikiwa umri wake unaruhusu

    Muhtasari

    Watoto wanaoharisha wasipewe vyakula vinavyoweza kuongeza ukubwa wa tatizo mfano maziwa ya ng’ombe na vile vyenye sukari nyingi.

    Pia, katika mazingira fulani, daktari anaweza kushauri aongezewe maji au kupatiwa dawa maalum hasa za antibayotiki (viuavijasumu) kwa kadri atakavyoona inafaa. 

    Kwa kuwa baadhi ya aina za kuhara huwa ni nyepesi kusambaa kirahisi na kuleta madhara makubwa zaidi, mama anashauriwa kusafisha mikono yake kwa maji na sabuni kila mara baada ya kumsafisha mtoto pamoja na kumbadilishia nepi haraka kila mara anapojisaidia.

    Share This Article